Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Shein Atuma Salamu za Rambirambi Kwa Mtawala wa Sharjah Sheikh Khalid Bin Sultan.


Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) Mhe.Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, kulia akiwasikilisha Salamu za rambirambi kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt. Ali Mohamed Shein kwa Mtawala wa Sharjah Sheikh Khalid bin Sultan Mohammed Al Qasimi,hafla hiyo imefanyika katika makazi yake Sharjah.

MTAWALA wa Sharjah Sheikh Sultan Bin Mohammad Al Qasimi   amepokea salamu za rambirambi kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alizozituma kwa Mtawala huyo wa Sharjah kufuatia kifo cha mwanawe Sheikh Khalid bin Sultan bin Mohammad Al Qasimi.

Akipokea salamu hizo za rambirambi zilizowasilishwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) Balozi  Mbarouk Nassor Mbarouk, Sheikh Sultan Bin Mohammad Al Qasimi alitoa shukurani zake kwa Rais Dk. Shein pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kwa kumpa pole kufuatia msiba huo wa mwanawe.

Kwa mujibu wa maelezo ya Balozi Mbarouk akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu akiwa ofisini kwake mjini Abudhabi alisema kuwa Kiongozi huyo wa Sharjah ameleza kufarajika na salamu hizo za rambirambi alizozituma Dk. Shein huku akisifu na kupongeza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Sharja na Zanzibar na kuahidi kuuendeleza.

Rais Dk. Shein, alimtumia salamu za rambirambi Sheikh  Sultan Bin Mohammad Al Qasimi kufuatia kifo cha mwanawe Sheikh Khalid bin Sultan bin Mohammad Al Qasimi kilichotokea London, nchini Uingereza Julai 1, mwaka huu.

Katika salamu hizo, Dk. Shein alieleza kuwa amepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kifo cha mtoto wa kiongozi huyo na kwa niaba yake binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar, wanatoa salamu zao za pole kwa familia, ndugu na wananchi wote wa Sharjah na Taifa zima za Umoja wa Falme nchi za Kiarabu kwa jumla.

Salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira familia ya Sheikh Al Qasimi wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu Sheikh Khalid bin Sultan bin Mohammad Al Qasimi katika kipindi hiki kigumu cha msiba huku akimuomba Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema peponi, Amin.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.