Habari za Punde

Jumuiya ya Kiislamu ya Muzdalifat Wakishirikiana na Shirika la H,H,R,D Kutoka Marekani Wakabidhi Vifaa Tiba


Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akimpandisha Mtoto Sulhia Idi Nassor ambae ni Mlemavu katika kigari katika hafla ya makabidhiano ya Vifaa Tiba vilivyotolewa na Jumuiya ya Kiislamu ya Muzdalifat wakishirikiana na Shirika la H,H,R,D kutoka Marekani hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Wizara hio Mnazi mmoja Zanzibar.
Picha na Yussuf Simai Maelezo- Zanzibar.


Na.Khadija Khamis Maelezo Zanzibar.
WAZIRI wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed, amesema Serikali itaendelea kutoa huduma bora za matibabu kwa jamii  ili kuhakikisha wanapata huduma zinazostahiki  hapa nchini.
Aliyasema hayo wakati akipokea msaada wa vifaa mbali mbali vya tiba kutoka Taasisi ya Muzdalifa chini ya ufadhili wa shirika la kusaidia huduma za jamii iliyopo Marekani (HHRD) ghafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Alisema hatua hiyo itasaidia upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi ili kuepusha kufuata matibabu nje ya nchi.
Waziri Hamad, alisema ni jambo la faraja kwa Taasisi ya Muzdalifa kuunga mkono Serikali kwa kuwasogezea huduma za tiba kwa wananchi ili kwenda sambamba na mikakati ya serikali katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora bila malipo.
Aidha alisema kuwa kuna baadhi ya taasisi hupata misaada kama hiyo lakini haiwafikii walengwa kwa kujimilikisha wao wenyewe kwa maslahi yao.
Hivyo ameipongeza taasisi hiyo kuwa wasimamizi wazuri ambao wanapokea msaada  mbali mbali na kuwafikia walengwa.
Alisema kuwepo na utaratibu maalum wa kuorodhesha mahitaji ya vifaa vya tiba vinavyohitajika ili kuweza kuziba pengo la mahitaji yaliyopo.
“Tusipoorodhesha mahitaji yetu ya vifaa tutasababisha wingi wa vifaa ambavyo hatuvihitaji na kuvitumia kwa fujo” alisema Waziri.
Hivyo ameishukuru taasisi hiyo kwa kuwaletea msaada huo na kuahidi kuwafikia walenga na kuwa pamoja na serikali.
Hata hivyo, aliwataka wazee na walemavu kueleza changamoto zao zinazowakabili ili kuweza kufanyiwa kazi na serikali pamoja na taasisi zinazojitolea.
Nae Mwenyekiti wa taasisi ya Muzdalifa, Shekh Abdalla Ghadhal, amesema taasisi yake itaendelea kushirikiana na serikali kwa kuwapatia vifaa vya matibabu kwa wananchi kila wapatapo misaada kwa wahisani.
Misaada  ya vifaa  vya tiba vilivyotolewa  na taasisi ya Muzdalifa ambavyo vimegharimu jumla ya dola 124 za kimarekani.
Vifaa vyenyewe vikiwemo  vitanda vya uchunguzi, magongo na viti vya walemavu, pempasi, viti vya kubebea wagonjwa, sabuni,  vifaa vya usafi, nguo za wagonjwa, glavz,  na vyenginevyo.
Alisema Muzdalifa inaendelea kupokea misaada mbali mbali ya huduma za jamii hivi karibuni takriban kontena 8 kutoka Malesia ambayo itawanufaisha wananchi wa Zanzibar.
Alisema misaada yenyewe ikiwemo nguo, komputa, sabuni na vitu vya kuchezea watoto.
Kwa upande wake Naibu Katibu wa Jumuiya ya wazee, (JUWAZA II) Kombo Mohammed Khamis, amesema jumuiya yao inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo usafiri wa kuwapelekea huduma za matibabu wazee na walemavu ambao wako katika masafa ya mbali hali ambayo inaikwaza jumuiya hiyo.
“Hatuna vitendea  kazi katika ofisi yetu ikiwemo komputa, vifaa vyengine vya kufanyia kazi ili kufanya kazi zatu kwa ufanisi zaidi” alisema.
Hivyo ameziomba Taasisi mbali mbali zenye uwezo kuwasaidia  kwa kuimarisha utendaji kwa taasisi hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.