Habari za Punde

Makamu wa Pili wac Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Ujenzi wa Tangi la Maji Kijiji cha Kitope leo.

Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Tangi hilo la kuhifadhia Maji safi na salama Kitope Mbaleni Bwana Jackson Maro Kulia ya Balozi Seif akielezea hatua zinavyoendelea za Ujenzi wa Tangi la Kuhifadhia Maji safi katika Kijiji cha Kitope Mbaleni.
Mwakilishi wa Taasisi ya Kiraia ya Tanzania Youth Icon {TYI} Bwana Abdullah Miraji Othman akisema changamoto wanazopambana nazo kwenye Ujenzi wa Mradi huo wa Tangi la kuhifadhia Maji safi na Salama Kitope Mbaleni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kitope Mbaleni mara baada ya kuutembelea Mradi wa Ujenzi wa Tangi la Maji safi na salama Kijiji hapo.Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Visiwa vya Zanzibar vinaweza kupata mtikisiko mkubwa wa uchafuzi wa Mazingira iwapo Watu wataachiliwa kuendelea kuchimba Mchanga kiholela pamoja na matumizi yasiyo  na Mpango  ya Rasilmali nyengine za Mawe na Kokoto.
Alisema Serikali imelazimika kuandaa utaratibu maalum wa upatikanaji wa Rasilmali hizo muhimu katika harakati za Ujenzi wa Majengo na Miundombinu mbali mbali kufuatia athari kubwa iliyokwishajitokeza kwenye mashimo ya mchanga ambayo baadhi yake huchipuka maji ya chumvi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo mapema asubuhi alipofanya ziara fupi ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Tangi kubwa la Kuhifadhia Maji safi na salama katika Mtaa wa Kitope Mbaleni baada ujenzi wake kusua sua kutokana na ukosefu wa nyenzo za kutekeleza Mradi huo ikiwemo Mchang, Kokoto na Mawe.
Alisema Nchi hivi sasa imeharibika kutokana na mashimo mengi yaliyochimbwa kwa ajili ya kupata Mchanga wa Ujenzi hali inayoashiria lazima zipatikane mbinu mbadala za kukabiliana na changamoto hiyo ya uchafuzi wa Kimazingira inayoweza kuleta maafa hapo baadae.
Balozi Seiif alifahamisha kwamba Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo, Wataalamu, Taasisi pamoja na Jumuiya za Kiraia zinafanya jitihada za makusudi katika kuona Ujenzi utakaobuniwa wa Majengo ya Taasisi za Umma na Binafsi yanazingatia mfumo wa kutumia Mchanga kidogo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Taasisi ya Kiraia ya Tanzania Youth Icon {TYI} pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} kupitia Wadau wao wa Maendleo kwa uwamuzi wao wa Kujenga Tangi hilo litakalofaidisha Wananchi waliomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.
Alisema Kitope ni eneo lenye usumbufu wa huduma za Maji safi na salama kwa muda mrefu tokea kuharibika kwa Tangi la zamani la kuhifadhia Maji na Wananchi wanaozunguuka eneo hilo wamekuwa wakipata changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo muhimu kwa ustawi wao.
Mapema Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Tangi hilo la kuhifadhia Maji safi na salama Kitope Mbaleni Bwana Jackson Maro alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Tangi hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji zaidi ya Lita 50,000.
Mhandisi Maro alisema kazi hiyo imeanza rasmi kwa hatua ya msingi karibu Wiki Tatu sasa, lakini imeshindwa kuendelea kama ilivyopangwa kutokana na ukosefu wa upatikanaji wa wakati wa Rasilmali ya Mchanga, Kokoto pamoja na Mawe.
Naye Mwakilishi wa Taasisi ya Kiraia ya Tanzania Youth Icon {TYI} Bwana Abdullah Miraji Othman alisema juhudi zimefanywa na Taasisi yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar{ ZAWA} za kuandika Barua katika Taasisi zinazosimamia Rasilmali zisizorejesheka lakini bado upatikanaji wa Rasilmali hizo umekuwa mdogo.
Bwana Miraji alitahadharisha kwamba Mradi wa Ujenzi huo umepangwa kukamilika ifikapo Tarehe 31 Disemba Mwaka huu vyenginevyo Wafadhili waliojitolea kuwezesha Mradi wa Ujenzi huo  wataondoa Fedha zote walizozitenga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.