Habari za Punde

Wanaadamu Wapaswa Kumshukuru Mwenyezi Mungu Kwa Kuwaoa Zawadi ya Neema Baadhi ya Mataifa IDuniani Imekosekana.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Dini uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Jijini Zanzibar leo.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Katiba za Serikali zote Mbili Nchini Tanzania ile ya Jamuhuru ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetoa uhuru kwa Wananchi wake kuwa na Haki ya kuabudu dini waitakayo ilimradi wanatii Sheria.
Alisema Katiba hizo hazijaegemea upande wa Dini yoyote ile huku zikitoa fursa za Waumini wa dini tofauti kufanya mambo yao ikiwemo siku za mapumziko ya Kidini zinazowafaidisha Watu wote.
Akiufungua Mkutano wa Kimataifa wa Siku Mbili wa Taasisi za Dini wa Amani baina ya Watu huko Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Baozi Seif Ali Iddi alisema hivi sasa vipo vikundi vinavyovaa joho la Dini na kuhatarisha Amani sehemu mbali mbali Duniani.
Balozi Seif alisema Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na Viongozi wa Dini katika kuhakikisha Jamii inaendelea kuishi kwa furaha, upendo na Amani jambo ambalo daima itaendelea kuongeza na kuunga mkono jitihada hizo.
Alieleza kwamba ni jambo la kupendeza kuona Viongozi hao wa Dini tofauti bila ya kujali itikadi za Dini zao hukusanyika pamoja na kuwa na dhamira moja ya kudumisha Amani kwa kuhubiri mambo yanayowaongoza salama Wafuasi wao mahali popote pale.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa kuendelezwa Mikutano kama hiyo sehemu mbali mbali Duniani kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuimarisha uhusiano mwema kati ya Dino na nyengine pamoja na kuhakikisha Amani iliyopo inadumishwa kwa Waumini wa Dini zote kufuata maandiko yaliyomo kwenye Dini zao.
“ Nikiri kwamba nimeguswa sana na dhumuni la Mkutano huu lenye lengo la kushajiishana katika kutunza na kuhifadhi Amani kwa Watu wote, na ushirikishwaji wa Jamii katika kudumisha Amani hiyo”. Alisisitiza Balozi Seif.
Alisema Wanaadamu wanapaswa kumshukuru Mwenyezi kwa kuwapa zawadi ya neema ambayo katika baadhi ya Mataifa Duniani imekosekana akitolea Mfano Nchi za Libya, Syria na Misri.
Balozi Seif aliwaeleza Viongozi hao wa Dini na Wanavyuoni wapatao 70 kutoka Afrika, Asia na Ujerumani kwamba wazo na Mkutano huo kufanyika Zanzibar linatokana na sifa ya muda mrefu ya uvumilivu wa Kidini ingawa zaidi ya asilimia 90% na Wananchi wanafuata na kuamini Dini ya Kiislamu.
Alisema uvumilivu wa Kidini Visiwani Zanzibar umekuwepo kwa muda mrefu sana hali ambayo imewafanya Wananchi wake pamoja na tofauti zao za Kidini lakini wanaishi kama familia Moja.
Alieleza kwamba Kihistoria muingiliano wa Waumini wa Kiislamu na Kikristo kwa Zanzibar umeanza tokea Mwaka 1840 pale Mjerumani Dr. Johanne Krapf alipotembelea Zanzibar na kuomba ruhusa ya kujenga Kanisa katika Mtaa wa Mombasa.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Miaka 30 baadae Bishops Steere na Tozer waliingia Zanzibar na kujenga Kanisa la Anglikana Mkunazini, ujenzi uliochangia kipande cha Ardhi na Jamii ya Wahindi, na Sultan wa wakati huo Seyyid Bin Barghash.
Alisema Zanzibar ina Historia zaidi ya Miaka 170 ya muingiliano wa Kidini kiasi ambacho fedha ya mwanzao ya Zanzibar wakati wa Uhuru ilikuwa na dhamira ya uvumilivu wa Kidini ikionyesha alama ya Kanisa la Anglikana na Katoliki, Msikiti wa Sunni na Shia na Nyumba ya Ibada ya Hindu.
Mapema akitoa Taarifa ya Mkutano huo Katibu wa Muungano wa Makanisa ya Evangelica kutoka Ujerumani Dr. Jochen Motte alisema Uongozi wa Kanisa hilo utaendelea kushirikiana na Mataifa, Taasisi na Mashirika mbali mbali Duniani yaliyojitolea kusimamia suala la Amani.
Dr. Jochen alisema zipo Nchi zenye mtafaruku wa uwepo wa Amani ambazo Watumishi wake hupangiwa kupelekwa kutoa huduma za Kijamii na kutangaza Amani baina ya Watu kwa lengo la kuirejesha Dunia kuwa mahala patukufu pa Ibada kwa wana wa Mungu.
Naye kwa upande wake Askofu Dr. Alex Gehaz Malasusa alisema faida ya Aamani huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la Uchumi na kuimarika kwa Ustawi wa Jamii.
Dr. Alex alisema hali hiyo hutokana na wanajamii kupata fursa pana zaidi ya kujikita katika shughuli mbali mbali za Maendeleo ya Kiuchumi na hatimae pato la Taifa kukuwa kutokana na uimarishaji wa Miundombinu ya Sekta tofauti unaotokana na kuwepo kwa Amani.
Askofu Dr. Alex Gehaz Malasusa kwa niaba ya wenzake aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Watu wake kwa ukarimu wao kwa Wageni hao waliopata furaha na faraja wakati wa uwepo wao Zanzibar.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuufungua Mkutano huo wa Dini wa Siku Mbili Mshauri wa Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alisema Maandiko ya Vitabu Vitukufu vya Dini wakati wote yamekuwa yakisisitiza umuhimu wa kudumishwa suala la Amani.
Sheikh Soraga alisema Jamii hushindwa kufanya Ibada sambamba na kuendeleza harakati zao za Kimaisha za kuwapatia kipato halali halali endapo panakosekana lulu ya Amani.
Mkutano huo wa Kimataifa za Taasisi za Kidini umeandaliwa kwa pamoja na Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Wakf na Mali ya Aamana Zanzibar, Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar na Kanisa Katoliki Dayosisi ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.