Habari za Punde

Wananchi wa Mtaa wa Kwahani Wapongezwa Kwa Uzalendo Wao Uwepo wa Ujenzi wa Mradi wa Mji Mpya.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Nd. Iddi Haji Makame akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Kisasa utakavyofanyika katika Mtaa wa Kwahani.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uzalendo wa Wananchi wa Kwahani kwa kuonyesha moyo wao thabiti uliorahisisha kukubali kupisha uwepo wa Mradi wa Ujenzi wa Mji Mpya na wa Kisasa katika Makaazi yao ya asili.
Pongezi hizo alizitoa wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua eneo linalotarajiwa Kuengwa awamu ya kwanza ya Majengo hayo ambayo yatakapomalizika ndani ya kipindi cya Mwaka Mmoja watarejea katika Makaazi yao Mapya.
Balozi Seif Alisema Mradi huo umekuja katika ile azma ya Serikali Kuu kuimarisha majengo ya Kisasa katika Mitaa ya Ng’ambo katika mpango Maalum unaojuilikana kwa jina la Ng’ambo tuitakayo ambayo zoezi hilo limeanza katika Mtaa wa Kwahani ndani ya Manispaa ya Mjini.
Alisema Wananchi wa Mtaa wa Kwahani sio Wageni kwenye zoezi kama hilo la kuhama makaazi yao kwenda sehemu nyengine kutokana na sababu mbali mbali za Kibinaadamu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatahadharisha Wananchi hao kuwa makini katika kipindi hichi na fitna pamoja na chokochoko zinazoweza kupikwa na baadhi ya Watu waliozoea kufarakanisha Wananchi kwa malengo yao binafsi ya kuvuruga Maendeleo ya Jamii Nchini.
Balozi Seif alisema kuhama kwao kwa muda ni kwa ajili ya kupisha uendelezaji wa Mradi huo muhimu na mara baada ya kukamilika watarejea katika nyumba zao mpya watakazokabidhiwa na Serikali na kufaidi Matunda ya Uhuru wao.
Hata hivyo Balozi Seif pia akawakumbusha Wananchi ambao bado hawajahama katika eneo hilo kuelekwa kwamba mali ikeshalipwa fidia ni kwa muhusika kupisha maamuzi yanayofuatia kuchukuliwa.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar Nd. Iddi Haji Makame alisema Mradi huo utakuwa na Majengo Matano yatayojumuisha Nyumba  70 ambapo katika Kiwango hicho Nyumba 50 zitalipwa fidia kwa Wananchi waliovunjiwa.
Ndugu Iddi alisema Ujenzi huo utakwenda sambamba na uwepo wa Milango ya Duka 59 ambayo kati ya hiyo Milango 11 italipwa Fidia kwa Wananchi waliovunjiwa Maduka yao kupisha Ujenzi huo.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha alimueleza Balozi Seif  kwamba Nyumba 20 na Milango ya Duka 48 takayobakia baada ya zoezi la kulipa Fidia Serikali itaangalia utaratibu wa matumizi mengine hapo baadae.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mjini Bibi Marina Joel Thomas alisema hivi sasa lipo changamoto kubwa la uchimbwaji wa mchanga hasa wakati wa usiku baada ya kusafishwa  kwa eneo hilo la Kwahani
Bibi Marina alisema ni vyema katika kukabiliana na  changamoto hiyo licha ya Serikali ya Wilaya kuagiza uwepo wa ulinzi Shirikishi lakini ipo haja ya kuzunguushwa uzio wa eneo hilo ili kunusuru uchafuzi wa mazingira.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifanya ziara fupi ya kuangalia harakati za uchimbwaji wa Mchanga kwa ajili ya shughuli za ujenzi  katika Shimo la Panga Tupu Maarufu Kitupa.
Shimo la Pangatupu ndilo linalotoa huduma ya Mchanga kwa wakati huu kufuatia lile la  Chechele kufungwa Miezi Mitatu iliyopita baada ya kukamilisha utaratibu wa uchimbaji Kimazingira.
Msimamizi Mkuu wa Mshimo ya Mchanga ya Pangatupu Nd. Hassan Ishak Bakari alimueleza Balozi Seif  kwamba shimo hilo limeanza huduma Tarehe 1 Julai 2019 baada ya Wananchi 25 waliokuwa na mazao yao kulipwa fidia.
Hata hivyo Nd. Hassan alisema licha ya Vigezo vya mazingira vinavyoelekeza uchimbaji usipindukie Mita Tatu chini lakini eneo hilo litalazimika kuchimbwa chini ya kigezo hicho kutokana na mchanga wake umechanganyika na udongo ambao haufai kwa kupigia matofali.
Alisema wasimamizi kutoka Taasisi za Kilimo, Misitu na Mazingira wanaendesha  zoezi hilo kwa mujibu wa taratibu zilizoainishwa na Serikali kwa kumruhusu kupata huduma ya Mchanga Mwananchi au Kampuni iliyofanya maombi na kukamilisha taratibu zote husika.
Msimamizi Mkuu huyo wa Mshimo ya Mchanga ya Pangatupu alifahamisha kwamba alieleza kwamba uchimbaji wa sasa unaendeleza taratibu za kuheshimu suala la Mazingira hali inayokwenda sambambva na usafishaji wa maeneo ya machimbo kuzingatia kuiacha Miti mikubwa kama Miembe.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Rajab Ali Rajab alisema hivi sasa yapo maombi Matano waliyowasilishwa ya maeneo yanayopendekezwa kuchimbwa Mchanga ndani ya Wilaya hiyo.
Nd. Rajab alisema licha ya kupendekezwa kwa eneo jipya Mbadala la Kiombamvua baada ya kumalizika kwa Pangatupu, lakini maamuzi ya eneo lipi linalostahiki ni jukumu la Serikali Kuu.
Hata hivyo Nd. Rajab alisema jukumu la Uongozi wa Serikali ya Wilaya ni kusimamia zoezi la fidia kwa Wananchi watakaohusika kulipwa fidia ya Mali zao kwenye eneo wanalotumisha kwa shughuli zao kama litakubalika kutumiwa kwa zoezi kama hilo.
Akitoa shukrani zake kufuatia ziara hiyo ya kuangalia mazingira halisi ya zoezi la Uchimbwaji wa Mchanga Mapangutupu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taarifa yoyote mpya itakayohusiana na maombi ya utumiaji wa Shimo jipya la Mchanga lazima lifikishwe Serikali Kuu.
Balozi Seif alisema tahadhari lazima ichukuliwe katika kuendesha zoezi la uchimbaji wa mchanga kwa vile Zanzibar tayari iko katika hali hatarishi ya uchafuzi wa mazingira kwa kuzunguukwa na mashimo yaliyotokana na kazi hiyo inayopaswa kuendeshwa Kitaalamu zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.