Habari za Punde

ujenzi wa barabara ya Uzi

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmou akishirikiana na baadhi ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi katika ujenzi wa Barabara ya Uzi Mkoa wa Kusini Unguja.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud akipokea Jiwe Kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini Rajab Ali kwa ajili ya kushiriki ujenzi wa Barabara ya Uzi Mkoa wa Kusini Unguja.
Mwananchi wa Uzi Hilali Mohamed Ali akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu changamoto za barabara ya Uzi Mkoa wa Kusini Unguja.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
Na Mwashungi Tahir - Maelezo.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mbele  maendeleo kila upande ili kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani  ndani ya nchi yao bila ya matatizo.
Hayo ameyasema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud huko katika njia ya Uzi wakati alipokuwa akishirikiana na wananchi  katika ujenzi wa barabara hiyo .
Amesema Serikali imeweka malengo ya kujenga daraja katika sehemu hiyo ili iweze kurahisisha usumbufu uliopo hivi sasa na kuwafanyia wananchi wa Uzi na Ng’ambwa kuweza kutumia barabara hiyo kwa vizuri.
Pia amewataka wananchi wa vijiji hivyo kuacha kasoro zilokuwepo na kujenga mashirikiano kwani umoja na mshikamano ukiweza kuimarika wataweza kuishi kwa amani na utulivu .
Aidha amewataka viongozi wa jimbo hilo kuwa karibu na wananchi katika kuzitatua changamoto zinazowakabili ndani ya kisiwa hicho kwa kukaa pamoja na kuzipatia ufumbuzi.
Ayoub amewaomba wananchi wa vijiji hivyo kuacha mara moja shughuli za magendo  na uvuvi haramu kwani kunachangia kuhujumu uchumi na kuua mazao ya baharini.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kati Hamida Mussa Khamis amesema ujenzi wa  barabara ya Uzi na Ng’ambwa ni kuunga mkono kutokana na  jitihada zinazofanywa na wananchi  kwa lengo la kuondosha changamoto ilioko.
Amesema utengenezaji wa barabara hiyo utakapokamilika kutakuwa katika hali nzuri na  kutaweza kuleta mabadiliko katika harakati za usafiri na kupatikana maendeleo kwa haraka.
Kwa upande wa Mkandarasi Shaya Mohamed Haji amesema watu wa Uzi wana shida ya barabara kwa muda mrefu hivyo wanashukuru kwa viongozi mbali mbali kufika katika ujenzi huo kwa lengo la kutia nguvu katika kukamilisha njia hiyo.
Ayoub  ameahidi kutoa saruji mifuko mia amewakabidhi vifaa vya kukamilishia ujenzi huo ikiwemo kuwapatia mifuko ishirini ya saruji na thamanini atawakabidhi baadae  nyundo pamoja na mawe gari mbili  kwa lengo la kukamilisha ujenzi huo.
Nao wananchi walioshiriki kwenye ujenzi huo wamewashukuru viongozi hao kwa vifaa walivyopatiwa  kwani barabara hiyo ikikamilika kutaweza kuwarahisishia wagonjwa na akinamama wakati wa kwenda mjini kujifungua . 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.