Habari za Punde

Ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili Lafanyika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Mzee Mwinjuma Kirobo kutoka Kikundi cha Wajasiri Amali cha Tulikotoka kutoka Bweleo akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi Kikundi hicho kinavyoendelea na uratibu wa kuhifadhi vitu vya Aslimu vilivyokuwa vikitumiwa na Waswahili wa enzi zilizopita.
Balozi Seif na viongozi wengine wa Serikali wakikagua Vitabu mbali mbali vilivyoandikwa kwa Lugha ya Kiswahili na Waandishi Mahiri waliobobea kwenye Maonyesho ya Kongamano la Kimataifa la Kiswahili.
Balozi Seif akiangalia baadhi ya Vitabu vya Kiswahili na kuridhika na kazi kubwa ilivyofanywa na Magwiji wa Lugha ya Kiswahili kutoka pembe mbali mbaliza Dunia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikabidhiwa Kasha la Mswahili kwa ajili ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein kutoka kwa Uongozi wa Baraza la Kiswahili Zanzibar.
Balozi Seif  pamoja na Viongozi wengine wa Kitaifa na Baraza la Kiswahili wakiwaonyesha Washiriki wa Kongamano wa Tatu la Kimataifa la Kiswahili nakala ya Kitabu akichokizindua kilichotungwa na Gwiji wa Kiswahili wa uandishi wa Vitabu Duniani Mzee Haji Gora Haji na kupewa jina la Shuwari.
Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar {BAKIZA} Dr. Mohamed Seif Khatib akitoa salamu za kuwakaribisha Waswahili kutoka pembe zote za Dunia waliohudhuria Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili hapo Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano la Tatu la Siku Mbili la Kimataifa la Kiswahili kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Mabaraza, Taasisi pamoja na Wataalamu wanaoshughulikia Kiswahili wana wajibu wa kusimama kidete kuhakikisha kuwa Lugha ya Kiswahili inaendelezwa na kutumiwa katika usahihi wake kulingana na Utamaduni wa Waswahili kwa vile Lugha ni kipengele muhimu cha Utamaduni wa Jamii.
Washirika hao lazima waone fahari ya mafanikio ya Lugha ya Kiswahili kwamba sasa imekuwa sio Lugha ya Waswahili wazawa wachache peke yao bali imeshaenea kuwa Lugha ya Kimataifa yenye utambulisho wa kujivunia kama nembo ya Afrika.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alitanabahisha hayo wakati akilifungua Kongamano la Tatu la Siku Mbili la Kimataifa la Kiswahili katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Alisema hiyo ni hatua muhimu ya kupanda hadhi kwa Lugha ya Kiswahili jambo ambalo halitotokea kwa sadfa, bali litatokana  na dhamira ya dhati ya Watu wenye mapenzi na Lugha hii adhimu na wanaoishughulikia.
Alisema Lugha ya Kiswahili kama zilivyo Lugha nyengine Duniani ina Utamaduni wake uliopevuka na kuimarika pamoja kusheheni masuala mbali mbali ya Mila, Desturi na Silka za Waswahili mambo ambayo ni rasilmali kubwa inayohitajika kuenziwa.
Dr. Shein alisema kutokana na mahitaji makubwa ya Lugha ya Kiswahili kukidhi kama daraja la mawasiliano katika shughuli mbali mbali za Kitaifa na Kimataifa, Lugha hii sasa imekuwa ni bidhaa inayouzika katika soko la Kimataifa kwa vile tayari hutumika kupitishia maafira tofauti.
Alieleza kwamba Wataalamu na watumiaji wa Lugha ya Kiswahili wanayo nafasi ya kuzitumia njia za kisasa za Teknolojia ya Mawasiliano, ili kuchangamkia fursa zilizopo za soko la Lugha hiyo kwa upande wa Fasihi na Isimu katika Mataifa mbali mbali Duniani kwa lengo la kujiongezea kipato.
Alifahamisha kwamba hadhi ya Lugha ya Kiswahili hivi sasa ni bidhaa muhimu katika kukuza Maendeleo ya Kiuchumi na Kiutamaduni Ulimwenguni. Hivyo inachopaswa kuzingatiwa kwa sasa ni jinsi gani itakavyopangwa Mikakati ya kuzitumia fursa zinazotokana na Kiswahili.
Rais wa Zanzibar alieleza kwa lengo la kuzidi kupiga hatua za kuiendeleza Lugha ya Kiswahili na kuweza kuzitumia fursa tofauti zinazozidi kujitokeza za kunufaika na Lugha hii adhimu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiagiza Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar {SUZA} kifanye maandalizi ya kuanzisha Skuli ya Tafsiri na Ukalimali.
Alisema hatua hiyo itawezesha kuandaliwa mapema Wataalamu waliobobea  wa fani za tafsiri na ukalimali wanaohitajika kwa wingi katika maendeleo mbali mbali ya Mawasiliano ikiwemo katika Mikutano ya Kimataifa ambako Lugha ya Kiswahili tayari inatambulika hivi sasa.
Dr. Shein alielezea matumaini yake kwamba jambo hilo kwa Zanzibar ni stahiki yake na linawezekana kutokana na uzoefu uliopo wa kuwasomesha Wageni Lugha ya Kiswahili kwa kipindi kirefu katika iliyokuwa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar {TAKILUKI}.
“ Serikali pamoja na kuongeza vifaa na vivutio vyengine maalum vya kuwafanya wageni imeshakiagiza Chuo Kikuu cha SUZA kuiimarisha Skuli hiyo ya Kiswahili na Lugha za Kigeni kuwa Kitivo Kikuu cha kuifanya Zanzibar kuwa Center of Exicellence wanaotaka kujifunza lugha washawishike kujiunga”. Alisisitiza Dr. Shein.
Alisema kama lilivyowezekana suala la kuanzisha Shahada ya Uzamivu na Uzamili za Kiswahili jambo hili litawezekana kwa vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kukata pua, kuunga wajihi katika kulifanikisha suala hilo kama ilivyowahi kufanya katika kufanikisha masuala mengine yenye maslahi kwa Taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alibainisha kwamba katika kuiendeleza na kuikuza Lugha ya Kiswahili kuna umuhimu mkubwa  kwa Wataalamu waliopo Nchini kuandika Kazi mbali mbali zitakazowasaidia kuongeza maarifa yao na kupanda daraja.
Alisema Wataalamu waliopo hivi sasa ambao wamepanda na kupata hadhi ya kuwa Maprofesa wamefikia daraja hiyo kwa kuandika vitabu na machapisho mengi ambayo yanaendelea kuwa hazina kubwa ya kupata maarifa mapya na kufanya marejeo.
“ Nimefurahi kuona kuwa Baraza la Kiswahili Zanzibar {BAKIZA} limezikusanya kazi za washiriki wa Kongamano la kwanza na kuwa Jarida Maalum la kupata maarifa na Taaluma ya Lugha ya Kiswahili”. Alisema Dr. Ali Mohamed Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alielezea matumaini yake ya kuuthamini uamuzi wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar pamoja na Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa kuendelea kuandaa Kongamano hilo kwa mara nyengine.
Alisema uamuzi wao unatoa fursa kwa Wataalamu Wakongwe wa Lugha ya Kiswahili kutoka sehemu mbali mbali Duniani kukutana na Wataalamu wachanga wanaochipukia katika fani mbali mbali za Lugha hii.
Dr. Shein alifahamisha kwamba huo ni mpango mwema na muhimu kwa Wataalamu wachanga wa Lugha kujifunza na kuchota maarifa kutoka kwa Wataalamu waliobobea kwenye Lugha ya Kiswahili.
Rais wa Zanzibar alitoa rai kwa Wataalamu wa Lugha ya Kiswahili  kuwa na tahadhari katika kuwasaidia wale wanaojitahidi kujifunza Lugha hiyo hasa katika Ukanda wa Nchi za Kusini Mashariki na Bara la Afrika {SADC} kwa vile wazungumzaji na watumaji wapya wa lugha hiyo wameongezeka hivi sasa.
Alisema Waswahili waliobobea  Kiswahili wanapaswa kuwakosoa na kuwaelimisha Waswahili wapya walioamua kujifunza Lugha hiyo kwa utaratibu mzuri ili kuepuka makosa yanayoweza kuigwa na Waswahili hao wapya wanaojifunza.
Dr. Shein alitanabahisha kwamba hivi sasa yapo matamshi yaliyoibuka katika matumizi ya Lugha ya Kiswahili yanaendelea kuingizwa katika mtindo wa kuichafua Lugha hiyo jambo ambalo litawarithisha watumiaji wapya wa Lugha hii   kufanya makosa bila ya kujijua.
“ Pasipozingatiwa kila Mtu anaweza kuibuka na Kiswahili chake cha siku ya leo badala ya kusema leo, kusema juzi kati badala ya kusema majuzi au juzi ya kijomba, siku hizi kuna mdada, mkaka, sijui kama hakuna mbibi na mbabu”. Alitanabahisha Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wanakongamano hao wa Kiswahili kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari mimeshayapokea Maazimio yote 19 yaliyofikiwa na wana Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika Mwaja uliopita hapa Zanzibar.
Alisema yale Maazimio yanayohusu uamuzi wa kufanywa na Serikali hivi sasa yanafanyiwa kazi na kuwekewa utaratibu wa kutekelezwa ambayo Mawili kati yao ni kuanzishwa Kitivo cha Utamaduni wa Mswahili na Sanaa Zanzibar pamoja na Utungaji wa Istilahi Mpya za Kiswahili.
Dr. Shein aliwahakikishia Wanakongamano hao kwamba Viongozi wa Mabaza ya Kiswahiuli ya Zanzibar na Tanzania {Bakiza na Bakita} wameshakutana na kuweka Mikakati sambamba na mipango ya kuweza kufanikisha jambo hilo muhimu kwa faida na maslahi ya Waswahili.
Akitoa Taarifa ya Kongamano hilo la Tatu la Kimataifa la Kiswahili Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar Bibi Mwanahija Ali Juma alisema mara kwa mara Baraza hilo limekuwa likithamini Waandishi Wakongwe wa Vitabu na kuwaonyesha mwanga wa ukomavu Waandishi wa Vitaba wachana.
Bibi Mwanahija alisema mfumo huo ulioanzishwa na Uongozi wa Baraza la Kiswahili Zanzibar kwa kushirikiana na lile na Tanzania pamoja na Taasisi zinazosimamia Kiswahili Kimataifa utasaidia kuijengea uwezo na uimara mkubwa zaidi Lugha ya Kimataifa kwa vile tayari imeshaingia ndani ya Lugha kubwa Duniani.
Katibu Mtendaji huyo wa Baraza la Kiswahili Zanzibar aliwataka na kuwahimiza Waandishi wote wa Vitabu Zanzibar kutochapisha Vitabu vyao kabla ya kupitiwa na Uongozi wa Baraza hilo kwa uhakiki utakaothibitisha machapisho yanayokubalika katika Jamii ya Kiswahili.
Bibi Mwanahija alielezea faraja yake kutokana na Taasisi mbali mbali Nchini zikitanguliwa na Serikali Kuu kwa kukubali kuyapokea na kuanza kuyafanyia Kazi Maazimio ya Wanakongamano ya Miaka iliyopita nyuma jambo linaloleta faraja kwa Taasisi zinazosimamia Lugha hiyo adhimu Duniani.
Akitoa salamu Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahilio Zanzibar Dr. Mohamed Seif Khatibu alisema ushiriki wa Viongozi Wakuu sambamba na wale Waandamizi wa Serikali, Taasisi za Umma wakiwemo Taasisi za Kiraia kwenye Makongamano ya Kiswahili umeonyesha haiba katika muendelezo wa Lugha ya Kiswali.
Dr. Mohamed Seif alisema ushiriki huo umekuwa chachu ya kuongezeka kwa Washiriki wa Makongamano kutoka maeneo mbali mbali Duniani ambao umeonyesha kupanda kutoka Washiriki 147 Mwaka 2017, 237 Mwaka 2018 na kufikiaWashiriki 270 Mwaka 2019.
Mwenyekiti huyo wa Baraza la Kiswahili Zanzibar {BAKIZA} alionyesha cheche za furaha kutokana na Kongano hilo la Tatu ya Kimataifa la Kiswahili kuambatana na uzinduzi wa Vitabu Vipya vya Shuwari kilichotunmgwa na Msanii Gwiji wa Kiswahili Duniani Mzee Haji Gora pamoja na kile cha Mazimioa ya Makongamano.
Naye Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Amani Karume akimkaribisha Mgeni Rasmi kwenye uzinduzi wa Kongamano hilo alisema Zanzibar imepata Heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Kongamano hilo kwa mara ya Pili ikithibitisha chimbuko la Lugha hiyo katikia Visiwa vya Marashi ya Karafuu.
Balozi Karume alisema Mikutano hii ya mara kwa mara ikiendelea kufungua mianya ya kuongezeka kwa fursa za Kiuchumi hasa kwa Wanajumuiya ya Afrika Mashariki Kiswahili kinazidi kuchanja mbuga katika medani ya Kimataifa.
Waziri wa Vijana alitolea mfano Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Mataifa ya Kusini na Mashariki mwa Bara la Afrika katika Mkutano wao uliofanyika Miezi ya hivi karibuni Dar es salaam Tanzania walioridhia rasmi Lugha la Kiswahili kuwa Rasmi katika Mikutano ya Jumuiya hiyo.
Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar alimpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa T\anzania Dr. John Pombe Joseph Magufuli kwa hotuba yake kwenye Mkutano huo wa Sadc aliyoitoa kwa Lugha ya Kiswalihi akionyesha uzinduzi Rasmi wa Lugha hiyo katika Vikao vya Jumuiya hiyo.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alipata fursa ya kutembelea maonyesho ya Washiriki wa Kongamano hilo la Tatu la Kimataifa la Kiswahili.
Balozi Seif alionyesha faraja yake kutokana na kuridhika na upeo wa Wanataalumawa Lugha ya Kiswahili katika Utunzi wa Vitabu mbali mbali vinavyotumika katika Elimu ya Sekondari sambamba na Vyuo Vikuu vya ndani na Nje ya Nchi.
Ujumbe wa Mwaka huu wa Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili lililifanyika kwa mara ya Pili Visiwani Zanzibar na kuandaliwa na Baraza la Kiswahilio Zanzibar Bakiza linasema:- “ Fursa za Soko la Kiswahili Duniani katika Maendeleo ya Fasihi na Isimu”.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.