Habari za Punde

Matukio ya Uhalifu Yamepungua Zanzibar - Masauni


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amezungumza hali ya usalama visiwani Zanzibar akisema imeimarika huku akisisitiza kuwa msimamo wa kuzuia mikutano yote ya siasa isiyofuata utaratibu upo pale pale.

Katika maelezo yake Masauni alisema muda wa siasa ukifika watu wataruhusiwa kuendesha mikutano mbalimbali yenye lengo la kueleza kwa wananchi walichokifanya kwa muda waliopewa nafasi baada ya kuchaguliwa na kuteuliwa katika nafasi mbalimbali.

Ameeleza hayo akitoa taarifa ya usalama na uhalifu visiwani hapa Zanzibar katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana katika mahojiano na kituo kimoja cha redio.

Katika mazungumzo hayo Masauni alianza kuzungumzia mauaji ambapo alisema mwaka 2018 jumla ya matukio 40 ya mauaji yalitokea tofauti na mwaka jana ambapo matukio hayo yalipungua na kufikia 35 huku akisema kazi imefanyika kuyadhibiti hadi kufikia idadi hiyo.

Alisema Serikali kupitia jeshi la polisi na pande zote zinazohusika zimeanza harakati kuweza kudhibiti matukio hayo yanayosababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo imani za kishirikina.

Matukio ya Udhalilishaji
katika kipindi cha mwaka 2019 Januari hadi Disemba matukio ya udhalilishaji yalionekana kuongezeka baada ya matukio 35 kuripotiwa tofauti na mwaka 2018 ambapo matukio 15 yaliripotiwa na jitihada mbalimbali zinafanyika ikiwepo utolewaji elimu kupitia askari wa Shehia na Ofisi ya Polisi Jamii na wadau huku sababu mbalimbali ikiwemo imani za kishirikina, jamii kukosa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya makosa hayo, watu kushindwa kuzuia matamanio,ukuaji wa matumizi ya mitandao,kutotolewa adhabu stahiki na kwa muda muafaka kwa wakosaji na kuwepo mmomonyoko wa maadili.

“Matukio haya ya udhalilishaji ikiwepo kubaka, kulawiti na kunajisi serikali tumeyaundia mkakati maalumu ikiwemo kamati maalumu iliyoundwa ikisheheni wataalamu wa udhibiti uhalifu kutoka jeshi la polisi wakiwemo wapelelezi, wataalamu wa madawati ya jinsia, tunataka kuona kadhia hiyo ya udhalilishaji inaisha Zanzibar na kumekuwepo na tabia ya familia za mtendaji na mtendewa wa matukio ya udhalilishaji kuficha mtuhumiwa huku wakiyamaliza mambo hayo katika ngazi ya familia ambapo sio sahihi lazima watuhumiwa wakamatwe na wafikishwe mahakamani na wakithibitika basi sheria ichukue nafasi yake, hatuwezi ona watoto wakiaribiwa sasa tutakua na taifa gani ambalo watu wake wamearibika” alisema Masauni

Wizi wa watoto wachanga
Akizungumzia matukio ya kuibiwa watoto wachanga, Naibu Waziri Masauni alisema mwaka 2018 jumla ya watoto wachanga 2 waliibiwa na baada ya juhudi za jeshi la polisi kudhibiti vyanzo mbalimbali vya matukio hayo ikiwemo wapiga ramli mwaka 2019 hakuna mtoto mchanga aliyeibiwa

“Nilishawaagiza viongozi wa jeshi la polisi kushirikiana na masheha wa shehia mbalimbali kuhakikisha wanagundua maeneo yenye waganga wanaowadanganya wananchi kupata utajiri kwa njia haramu ikiwemo viungo vya watoto wachanga, nalipongeza jeshi lilifanya msako na kusambaratisha hao wanaojiita wataalamu wanaowadanganya wananchi wetu” alisema Masauni

Madawa ya Kulevya
Kutokana na kuwepo kwa tatizo la biashara haramu ya dawa za kulevya, Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Ulinzi na Usalama liko mbioni katika kudhibiti biashara hiyo

“Jeshi liko makini katika kudhibiti mtandao wa biashara hiyo ambayo tumeona siku za nyuma vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa wakiaribika kwa dawa za kulevya, na kuna mpango maalumu uko katika utekelezaji na tayari umeanza kutoa matokeo chanya ambapo mwaka 2019 watuhumiwa 496 wametiwa mikononi, tumekamata pia Cocaine gramu 960.65, Heroine Kilogramu 10.2 na gramu 806.102 imekamatwa, Bangi Kilogramu 659.6 na gramu 649.775 ilikamatwa,vijana wetu wamezamia kwenye utafunaji mirungi lakini nayo tushakamata kilogramu10.6 na gramu 096.648 pamoja na vidonge vya Valium gramu 10.30” alisema Masauni

Usalama Barabarani
Kumekuwepo kwa upungufu wa makosa yanayohusiana na suala la usalama barabarani ambapo mwaka 2018 makosa 31,524 yaliripotiwa tofauti na mwaka 2019 ambapo makosa 23,166 yaliripotiwa

“Serikali kupitia Baraza la Usalama Barabarani kupitia Wakuu wa Trafiki nchi nzima hapa nazungumzia Zanzibar lakini hata kule Bara wamekua na programu mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha watumiaji wa barabara wanakua salama ili kuweza kuondoa vifo vya uzembe vinavyosababishwa na waendesha vyombo vya moto,baraza pia limekua likitoa elimu mashuleni na tumeona sasa kuna upungufu wa matukio takribani asilimia 26 japo tunapambana ndani ya mwaka huu kuondosha kabisa na mwaka huu Wiki ya Usalama Barabarani itafanyika hapa Zanzibar ili kuweka msisitizo kwenye hili la kupunguza ikiwezekana kuondosha ajali” alisema Masauni

Makosa mengine
Naibu Waziri Masauni aliyataja makosa mengine ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi wa magari, wizi wa mali za serikali kuu, wizi wa mifugo, ajali za moto, rushwa na wizi katika vyama vya ushirika kudhibitiwa huku makosa yake yakiendelea kushuka siku hadi siku kwa jitihada za jeshi la polisi na wadau wengine ikiwemo wananchi wema ambao hutoa taarifa mapema kwa jeshi la polisi.

“makosa kama rushwa ndani ya mwaka 2018 tukio moja tu liliripotiwa huku mwaka 2019 hakukua na tukio likihusisha utoaji na upokeaji rushwa.Wizi wa magari pia mwaka 2018 magari 5 yaliripotiwa kuibiwa huku kuonekana kushuka kwa makosa hayo mwaka 2019 baada ya matukio 2 kuripotiwa, kupatikana na nyara kwa miaka miwili 2018 na 2019 hakuna tukio lililotokea” alisema Masauni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.