Habari za Punde

Katibu Mkuu Mwaluko Azitaka Sekta Zishirikiane Kukabili Maafa.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko akifafanua umuhimu wa ushiriki wa kisekta kwenye Kupunguza madhara ya maafa, wakati akifungua kikao cha SADC cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa katika ukanda wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambapo yeye ni mwenyekiti wa kikao hicho, leo tarehe 18 Februari 2020, Zanzibar.

Na. Ibrahim Hamidu. OWM.
“Tatizo la athari za maafa yanayotokana na majanga ya asili linahitaji ushiriki wa sekta zote ili kukabiliana nalo ipasavyo, katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)” Mwaluko.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Zanzibar na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko wakati alipokuwa anafungua kikao cha SADC cha Makatibu Wakuu wenye dhamana ya maafa katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambaye yeye ni mwenyekiti.

 Mwaluko amesema nchi zote za SADC zina uzoefu wa masuala ya maafa, hivyo ni matarajio yake kuwa kazi waliyopewa ya kuandaa nyaraka kwa ajili ya mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya maafa utakaofanyika siku ya Ijumaa tarehe 21 Februari 2020,  uweze kufikia malengo yake.
Katika kikao hicho, Makatibu Wakuu wataandaa nyaraka itakayo ainisha mikakati na programu za kukabiliana na maafa na mpango unaobainisha namna nchi za SADC zilivyojipanga kukabiliana na maafa yanapotokea katika ukanda huo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji wa SADC wa Masuala ya Ushirikiano wa Kikanda, Dkt. Thembinkosi Mhlongo  alieleza kuwa athari za maafa zikiwemo vifo, uharibifu wa mali na miundombinu zimezikumba takribani nchi zote za SADC. Hivyo amesisitiza umuhimu wa nchi hizo kushirikiana kwa pamoja kuandaa mikakati ya menejimenti ya maafa.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar, Bw. Abdallah Hassan Mitawi amewaeleza  wajumbe wa kikao hicho kuwa nchi za SADC zimelipa umuhimu mkubwa suala la kukabiliana na athari za maafa na hilo linadhihirishwa na ushiriki wa nchi 15 kati ya 16 wanachama wa SADC katika mkutano huo.

Mkutano huo unaofanyika kwenye Hoteli ya Madinat AL Bahir iliyopo Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar unatarajiwa kuhitimishwa kwa kikao cha ngazi ya Mawaziri tarehe 21 Februari 2020 ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.

Kaulimbiu ya Mkutano huo : “Ushiriki wa kisekta kwenye Kupunguza madhara  ya maafa ni njia  bora ya kujenga Uhimili  katika ukanda wa nchi wanachama wa  Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)”

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.