Habari za Punde

RAIS MAGUFULI: VIONGOZI WALIOCHUKUA FEDHA ZA TASAF KINYUME NA MALENGO WAZIREJESHE HARAKANa Mwandishi Wetu,MAELEZO DAR ES SALAAM 17.2.2020
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli amewataka Viongozi wote wa Serikali waliochukua fedha za mpango wa kunusuru kaya maskini nchini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuzitumia isivyo sahihi kuzirejesha mara moja kwani serikali haipo tayari kuona fedha hizo zikitumika kinyume na malengo yaliyowekwa.

Akizngumza katika hafla ya uzinduzi wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) leo Jumatatu (Februari 17, 2020) Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema katika zoezi la Serikali ilibaini changamoto mbalimbali katika mfuko huo ikiwemo malipo kwa kaya hewa nchini.

Rais Magufuli alisema kupitia zoezi la uhakiki wa kaya masikini lililofanyika kuanzia Novemba 2015 hadi Juni 2017, Serikali iliweza kubaini uwepo wa kaya hewa 73,651 ambapo kaya 22034 zilithibitika kuwa wanakaya wake si masikini, kaya 18,700 ambazo hazikujitokeza mara mbili kupokea ruzuku na kaya 9903 zilizohamia vijiji/ mtaa/shehia ambapo mpango haujaanza.

‘’Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda naye pia anasema aliwahi kunufaika na TASAF na alisema alizitumia katika safari yake ya kwenda Dodoma katika masuala yake, sasa naomba fedha hizo uzirudishe mara moja kama ulizitumia katika matumizi hayo uliyoyasema’’ alisema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli alizitaja Halmashauri 10 zilizoathirika zaidi na kaya hewa ni Songea Manispaa (2,991), Chamwino (1,840), Kinondoni (1,538), Ilala (1,476), Moshi Manispaa (1,071), Arusha Mjini (851), Temeke (2,012), Dodoma Mjini (1,334), Buhigwe (862) na Morogoro (954), na kuongeza kuwa hiyo ni aibu sana kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri hizo.

Aliongeza kuwa zipo baadhi ya halmashauri 10 zilizojitahidi kudhibiti vitendo vya kaya hewa na kuwa na iidadi ndogo ya kaya hewa na kuzitaja halmashauri hizo ni pamoja na Pangani (149), Kilolo (211), Unguja (242), Igunga (76), Mtwara Mikindani (25), Rorya (207), Mkinga (140), Babati Mji (45), Geita Mjini (56) na Chunya 140.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema mara baada ya Serikali kubaini kasoro na changamoto zilizojitokeza awali, katika kipindi cha pili cha Awamu ya tatu ya TASAF (2020-2023) Serikali imekusudia kupunguza kiasi cha ruzuku kutoka asilimia 67 hadi 38, ambapo ruzuyku hiyo itatolewa kwa wazee wasiojiweza, watoto wadogo na kwa watu wenye kiwango kikubwa cha ulemavu.

‘’Awamu hii mpya tumepanga kuitekeleza katika halmashauri zote 185 na Wilaya 11 za Zanzibar na asilimia 60 ya fedha, sawa na shilingi trilioni 1.22 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo takribani 30,000 kwenye vijiji na mitaa 16,596 Tanzania Bara na shehia 388 kule Zanzibar’’ alisema Rais Magufuli.

Aliitaja miradi hiyo ni pamoja na sekta ya afya (Tsh Bilioni 121.736), elimu (Tsh. Bilioni 365.209), maji Tsh (Bilioni 585.937), barabara (Tsh Bilioni 49.668) na mazingira (Tsh Bilioni 96.416), ambapo katika kutekeleza miradi hiyo kipaumbele kitatolewa kutoka kwa watu wenye nguvu wanaotoka kwenye kaya maskini, ambapo Serikali inatarajia kuzalisha ajira na kuwapatia ujuzi pamoja na stadi za kazi watu wapatao milioni 1.2.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika alisema katika kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa changamoto zote zilizojitokeza katika awamu ya kwanza zinapatiwa ufumbuzi ikiwemo kufikia asilimia 30 ya kaya zilizobaki katika maeneo yote nchini.

Anaongeza kuwa kipindi cha kwanza cha Awamu ya tatu ya TASAF iliyoanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2013 imekamilika Desemba mwaka 2019, ambapo asilima 70 ya walengwa wote wamenufaika na mfuko huo kwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kuweza kubuni miradi iliyowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Abood Mohamed alisema utekelezaji wa miradi ya TASAF umekuwa ni wenye mafanikio makubwa kwa upande wa Zanzibar ambapo katika awamu ya kwanza iliyoanza mwaka 200-2005 jumla ya miradi 75 iliyogharimu kiasi cha Tsh Bilioni 3 ilitekelezwa na Serikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein katika hotuba yake iliyosomwa Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi alisema wananchi wa Zanzibar wamenufaika kwa kiasi kikubwa na miradi ya TASAF ambapo kwa sasa wananchi kutoka ndani na nje ya nchi, wamefika Zanzibar kwa ajili ya kujifunza mafanikio hayo yaliyopatikana.

Dkt. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano na wadau wote wa maenndeleo ili kuhakikisha kuwa awamu ya tatu ya TASAF itafanikiwa na kuleta tija iliyokuwa kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya TASAF, kiasi cha Tsh trilioni 1.46 kimetumika ambapo utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umefanyika katika Mamlaka za Serikali 159 kwa Tanzania Bara pamoja na Wilaya zote 11 kwa upande wa Zanzibar.

‘’Utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha Awamu ya tatu ya TASAF katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini ulijikita katika kutoa ruzuku kwa masharti, kutoa ajira ya muda, kuongeza kipato, kujenga na kuboresha miundombinu na kujenga uwezo katika ngazi zote za utekelezaji’’ alisema Mwamanga.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha Awamu ya Tatu ya TASAF katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umekuwa na mafanikio makubwa ambapo jumla ya miradi 8,809 yenye thamani ya Tsh Bilioni 130 kutoka vijiji/shehia 2,578 ilibuliwa na kutekelezwa na jamii ambapo jumla ya Tsh. Bilioni 97.5 zimetumika kulipa ujira kwa walengwa kwa walioshiriki kufanya kazi kwenye miradi.

Naye Mwakilishi wa Benki ya Dunia Ofisi ya Dar es Salaam Ms Preet Arora, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na mradi bora zaidi duniani ambao umewawezesha wananchi wa kipato cha chini kuweza kujiongeza kipato pamoja na kumudu gharama mbalimbali za huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya n.k.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.