Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Wakiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa mwezi wa Julai hadi Disemba 2029 /2020, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameitaka Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa ma Idara maalum za SMZ kushirikiana na
Wizara Afya na kuwa na mipango ya pamoja
itakayowezesha uendelezaji wa kituo cha Afya Mbuzini na kuwa Hospitali ya
Wilaya Magharibi ‘A’.
Dk. Shein amesema
hayo Ikulu Jijini Zanzibar, wakati akipokea taarifa ya Utekelezaji ya mpango
kazi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ,
kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2019/2020.
Alisema jengo hilo
linaweza kuendelezwa kupitia bajeti za Wizara hizo na ujenzi wake kufanyika
awamu kwa awamu, ili liweze kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo na vitongoji
jirani.
Alisema jengo
hilo la zamani lililogharimu fedha nyingi katika ujenzi wake lipo mahala pazuri
na linafaa kuendelezwa kwa dhamira ya kuwasaidia wananchi katika upatikanaji wa
huduma za Afya.
“Jengo lile lipo
mahala pazuri, lipo barabarani litaweza kuwasaidia wananchi wa Wilaya Magharibi
‘A’ likiendelezwa na kuwa hospitali ya Wilaya “, alisema.
Aidha, Dk. Shein
aliwakumbusha Wakuu wa Mikoa juu ya dhima waliyonayo katika ulinzi na usalama wa
Mikoa yao kwa kuhakikisha hakuna mgeni au mwekezaji anaefanya shughuli
zinazoashiria uvunjifu amani na kuingilia usalama wa nchi.
Kauli ya Rais Dk.
Shein ilikuja kufuatia taarifa ya kuwepo raia wa kigeni kutoka nchini Uingereza
alietengeneza makaazi juu ya mibuyu katika eneo la Pete, huku kukiwa na
viashiria kadhaa katika makaazi hayo vinavyohatarisha
usalama wa nchi.
Kwa kushirikiana
na vyombo vya Ulinzi na Usalama , aliagiza kufanyika uchunguzi ili kubaini uhalali
wa mgeni huyo kuwepo nchini na kumiiliki eneo hilo pamoja na vifaa anavyomiliki,
vinginevyo hatua za kiusalama zichukuliwe dhidi yake.
Aidha, aliwataka
viongozi wa Wizara hiyo pamoja na Viongozi wa Mkoa Kusini na Wilaya Kusini
kukutana na akinamama wa shehiya Kizimkazi wanaojishughulisha na kazi za
kutanda dagaa na kuwasikiliza , ili kuona vipi wataweza kuwasaidia kuendeleza
shughuli zao , huku kukiwa na katazo la kuepukana na uharibifu wa mazingira
katika ghuba ya Menai.
Vile vile, aliushauri
uongozi wa Wizara hiyo kuandaa utaratibu maalum utakaowezesha kupatikana maeneo
mbadala, ili vijana wanaoondoshwa katika maeneo waliyojikusanya muda mrefu na
ambayo hayako rasmi waweze kuondoka na kwenda kuendeleza maisha yao katika
maeneo mapya.
Rais Dk. Shein
aliukumbusha uongozi wa Wilaya ndogo Tumbatu umuhimu wa kutoa taaluma kwa
manahodha na wananchi kuepuka kujaza abiria na mizigo katika vyombo vya
baharini kupita kiasi, ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
Akigusia
changamoto zinaoikabili Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, Dk. Shein aliutaka
uongozi wa Wilaya hiyo kuwafahamisha wananchi juu ya maharibiko ya baadhi ya
vifaa muhimu vya uchunguzi, wakati ambapo Serikali imekuwa ikifanya juhudi za
kuvifanyia matengenezo, na kubainisha kuwa matatizo yaliopo ni ya muda.
Aidha, alitaka
kuangalia upya taratibu za ajira, vyeo na uhamisho kati ya Unguja na Pemba kwa
wafanyakazi wa sekta za Afya na Elimu walioko katika Ugatuzi ili kudhihirisha
dhana na malengo ya Ugatuzi, wakati ambapo hivi sasa Wizara zinazohusika na
sekta hizo zinaonekana kuendelea kushughulikia mambo hayo badala ya Halmashauri
za Wilaya.
Vile vile,
aliwataka watendaji wa Halmashauri kote nchni kusimamia matumizi bora ya masoko
kwa kuhakikisha wafanyabaishara wanapanga bidhaa zao katika maeneo yaliowekwa
an Serikali badala ya kupanga barabarani.
Mapema, akiwasilisha
taarifa ya Utekelezaji ya mpango kazi kwa kipindi cha Julai hadi Disemba
2019/2020, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa
na Idara maalum za SMZ Haji Omar Kheir alisema katika kipindi hicho Ofisi hiyo
imepata mafanikio makubwa, baada ya kuidhinishiwa jumla ya shilingi
107,297,564,386/ ikiwa ni asilimia 95 ya makadirio.
Alisema miongoni
mwa mafanikio hayo ni utekelezaji wa maamuzi ya Serikali ya kuanzisha mfumo wa
Ugatuzi na kupeleka madaraka kwa wananchi.
Alisema Serikali
kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imeendelea kutoa fedha za ruzuku lwa
Serikali za Mitaa ili kuziwezesha kutekeleza maukumu yao, ambapo kwa kipindi
cha Julai – Disemba,2019 ilifanikiwa kupata ruzuku ya shilingi 39,009,250,003/,
ikiwa sawa na asilimia mia moja.
Alisema katika
kipindi hicho pia kulifanyika uzinduzi wa Vitambulisho vipya vya Mzanzibari
mkaazi vyenye kutumia mfumo wa kisasa,
ambapo zoezi la ugawaji wake kwa wananchi lilianza rasmi Novemba 27, 2019 katika
Wilaya ya Micheweni Pemba.
Aidha, alisema mfumo
wa Usajili wa Vizazi umefanikiwa kufikishwa na kufungwa katika baadhi ya
Hospitali ili kurahisisha upatikanaji wa
vyeti vya kuzaliwa kwa wakati.
Alieleza kuwa
utoaji wa vyeti vya kuzaliwa ulianza kufanyika katika Wilaya kumi (10), huku
taratibu za kurejesha Mkonga wa Taifa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ zikianza.
Katika hatua
nyengine, Waziri Kheir aliipongeza Serikali kwa kusimamia kwa vitendo tamko la
Elimu bila malipo na kubainisha kuwa katika kipindi hicho imefanikiwa kununua
mabuku kwa ajili ya wanafunzi wote wa skuli za msingi na maandalizi.
Alisema katika
mwezi wa Disemba 2019, jumla ya makontena 32 yenye mabuku ya kuandikia, mabuku ya
mahudhurio ya wanafunzi na kadi za maendeleo za wanafunzi ziliwasili nchini
kutoka China na hatimae zoezi la ugawaji kufanyika katika Wilaya zote 11 za
Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa
shughuli za uhamasishaji wa uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya msingi na
maandalizi ulifanyika ambapo wanafunzi wapya 79,371 waliandikishwa.
Hata hivyo alisema
pamoja na changamoto ya kutoingiziwa fedha, Baraza la Jiji la Zanzibar
lilifanya uchaguzi wa Mheshimiwa Meya na Naibu Meya , sambamba na kubuni na
kuandaa mapendekezo ya miradi minane kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu
na kupanga utekelezaji wake.
Aidha, Mkuu wa
Mkoa Kusini Unguja Ayoub Mohamoud alisema Uongozi wa Mkoa huo umo katika
maandalizi ya kuanzisha mahakama ya Halmashauri ya Wilaya Kusini kama ilivyo
kwa Wilaya Kati, ili kuharakisha uchukuwaji wa hatua dhidi ya makosa mbali
mbali, ikiwemo ya wizi wa rasilimali za misitu ya Serikali.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment