Habari za Punde

USAID yavutiwa na jitihada za THBUB

Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Kimarekani, USAID, Andy Karas akiongea katika kikao kifupi kilichofanyika baina yake na viongozi wa tume alipotembelea ofisi hizo za  THBUB zilizopo jijini Dodoma  

Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu  Mathew Mwaimu akimkabidhi Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Kimarekani, USAID, Andy Karas Mpango mkakati wa THBUB wa miaka mitano (2018/ 2023) alipotembelea ofisi za THBUB zilizopo jijini Dodoma na kukutana na viongozi wa juu wa taasisi hiyo 

Na  Mbaraka Kambona,
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Kimarekani nchini Tanzania, USAID, Andy Karas ameipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa jitihada zake kuhamasisha ulinzi na utetezi wa haki za binadamu na usimamizi wa  misingi ya utawala bora, na kusema kuwa jitihada hizo ni muhimu katika kusaidia nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikiapo 2025.

Karas alisema hayo alipotembelea ofisi za THBUB zilizopo jijini Dodoma na kukutana na viongozi wa juu wa taasisi hiyo leo (Februari 20, 2020).

Alisema kuwa jukumu la THBUB la kuhamasisha ulinzi na utetezi wa haki za binadamu na uzingatiwaji wa misingi ya utawala bora ni muhimu sana kwani mahali ambapo haki haipatikani ni vigumu watu kupata maendeleo yao.

“Jukumu la tume ni muhimu mno, jitihada zenu ni nzuri, ni wazi kuwa mahala popote ambapo hakuna haki maendeleo ni ngumu kuyafikia, milango yetu ipo wazi tuendelee kushirikiana”, alisema Karas

Karas alisema kuwa USAID ipo mstari wa mbele katika  uwekezaji kwenye sekta mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo sekta ya Afya, Elimu, Kilimo na Utawala Bora na kusema kuwa wamekuwa wanawekeza Dola za Kimarekani milioni mia tatu hamsini (350) kwa mwaka kutekeleza miradi katika maeneo hayo.

Aliendelea kusema kuwa uwekezaji unaofanywa na USAID unaenda sambamba na mipango mikakati ya Tanzania ili kusaidia nchi kutimiza ndoto yake ya kufikia uchumi wa kati ifikapo    2025.

“Hivyo tupo hapa leo, kubadilishana uzoefu na kujadiliana maeneo tunayofikiri tunaweza kuunganisha nguvu zetu kwa lengo la kuboresha uhamasishaji wa haki za binadamu na uzingatiwaji wa misingi ya utawala bora nchini”, aliongeza Kalas

Aidha, alisistiza kuwa USAID ni mwenyekiti wa wadau wa maendeleo katika eneo la utawala bora hivyo tume isisite kuwasiliana nao pindi wanapokuwa na jambo lolote linalohitaji msaada au ushauri.

Akiongea mapema, Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu  Mathew Mwaimu alimueleza kwa ufupi Mkurugenzi huyo wa USAID kuwa tume imepewa majukumu mawili kwa pamoja nayo ni kusimamia haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.

Jaji Mwaimu alitaja vipaumbele vya THBUB mwaka huu kuwa ni kupokea malalamiko ya uvunjifu wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora, kukuza uelewa wa wananchi kuhusu haki za binadamu, kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, kujenga uwezo wa watumishi na kufanya ufuatiliaji wa uchaguzi mkuu.

“Tunajipanga kutoa elimu ya kuhamasisha haki ya kupiga kura wakati, huohuo tunapanga kuwa na mikutano na wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwemo Tume ya Uchaguzi ili kujadiliana na kukumbushana umuhimu wa kuwa na uchaguzi mzuri na wa amani”, alisema Mwaimu

“Hivi karibuni maafisa wetu walikuwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kufanya ufuatiliaji wa zoezi la uandikishaji wananchi katika Daftari la Mpiga kura japo lengo letu ni kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi nchi nzima”, alisisitiza Mwaimu

Katika kikao hicho, Karas aliahidi kuwatuma maafisa wa kitengo cha utawala bora kutoka USAID kwenda kukaa na maafisa wa THBUB kwa lengo la kujadiliana na kuangalia maeneo ambayo wanaweza kushirikiana.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.