Habari za Punde

Watanzania Walioko Nchi China Wanaendelea Kuwa Salama

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi wa Pili kutoka Kulia akiipongeza Serikali ya China kupitia Balozi wake Mdogo kwa jitihada inazochukuwa za kuendelea kuvidhitibi virusi vya Corona vinavyosababisha Homa ya Mafua Makali.
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaowu Kushoto akimpatia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi taarifa ya Watanzania walioko Nchini China ambao wanaendelea kuishi kwa amani ndani yamkipindi hichi cha mpito cha kuibuka kwa Virusi vya Corona Nchini humo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaowu wakiwa katika Picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Picha na – OMPR – ZN
Na.Othman Khamis.OMPR. 
Watanzania walioko Nchini Jamuhuri ya Watu wa China wanaendelea kuwa salama ndani ya kipindi hichi cha mpito cha Taifa hilo kukumbwa na Virusi vya Corona vinavyosababisha Homa ya Mafua makali ambayo kwa sasa janga hilo limeanza kupungua.
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaowu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar alipofika kumpa Taarifa halisi ya Wananchi wa Zanzibar walioko Nchini humo kwa shughuli tofauti ikiwemo Mafunzo.
Bwana Xie Xiaowu alisema licha ya kupungua kasi ya kuenea kwa Virusi hivyo vya Corona lakini idadi ya Watu waliofariki imeongezeka na kufikia Elfu 1,368 kutokana na Wagonjwa wengi kati yao kusumbuliwa na maradhi mengine makubwa kabla ya matatizo hayo.
Alisema idadi ya Watu Walioathirika wa Virusi hivyo kwa sasa imepindukia 40,000 ambapo juhudi zimeendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kukabiliana na jango hilo ambapo hadi hivi karibu Wagonjwa 5,992 wamehudumiwa  na kupoa kabisa.
Balozi Mdogo huyo wa China aliyepo Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba utafiti wa Kitaalamu uliofanywa katika maabara mbali mbali umebainisha kwamba Virusi hivyo vinavyoenea kwa njia ya hewa vinatokana na Wanyama pamoja na Popo.
Bwana Xie Xiaowu alielezea matumaini yake kutokana na Mataifa na Mashirika mbali mbali Duniani kuendelea kuchukuwa hatua na tahadhari za kukabiliana na wimbi hilo la kuenea kwa Virusi vya Corona.
Alisema Homa ya Mafua Makali inayosababishwa na Virusi vya Corona imeripotiwa kuibuka katika Mji wa Wuhan Nchini Jamuhuri ya Watu wa China yenye Watu Bilioni 1.4 mwishoni mwa Mwaka jana.
Akitoa shukrani zake kwa jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya China katika kukabiliana kudhibiti kuenea kwa Virusi vya Corona Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Janga lililowakumba Wananchi wa China pia limewagusa Watanzania kutokana na uhusiano wa Kihistoria uliopo wa Mataifa hayo rafiki.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa niaba ya Wananchi wake inatoa salamu za mkono wa pole kwa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China ili zifikishwe kwa Familia za Wananchi wake zilizopoteza Jamaa zao kutokana na janga hilo zito.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema janga hilo la kuenea kwa Virusi vya Corona kwa njia moja au nyengine limeathiri kundi kubwa la Watanzania waliojiwekeza katika shughuli za ujasiriamali uliojikita katika Sekta ya biashara wakitumia zaidi soko la China katika kuendesha miradi yao.
Alisema yeye binafsi na Wananchi walio wengi wamepata faraja kubwa kutokana na taarifa hiyo muhimu hasa ikizingatiwa kwamba wapo Watanzania zaidi ya 4,000 Nchini Jamuhuri ya Watu wa China wengine wakiwa Wanafunzi wa Fani mbali mbali za Kitaaluma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.