Habari za Punde

Rostam Awataka Watanzania Kuchukua Tahadhari Ya Maambukizi Ya Corona (COVID-19).

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi leo wakati akikabidhiwa msaada wa vifaa mbalimbali vya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona vyenye thamani ya Sh milioni 500 kutoka kwa Mfanyabiashara Rostam Aziz.
Mfanyabiashara Rostam Aziz akizungumza mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi leo wakati akikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona vyenye thamani ya Sh milioni 500 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Mfanyabiashara Rostam Aziz amewataka Watanzania kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi vya corona kutokana na ugonjwa huo kuwa tishio nchini na duniani kwa ujumla.


Rostam amesema hayo leo wakati akikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona vyenye thamani ya Sh milioni 500 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Vifaa hivyo ambavyo amevikabidhi leo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ni pamoja na vitakasa mikono 3,000, barakoa 20,000, kifaa cha kumpatia mgonjwa oxygen, vifaa vya kupima mwenendo wa moyo na mashine za kupumulia.


Pamoja na vifaa hivyo, pia ametoa mashine kubwa ya kusafisha mwili mbili ambayo moja ni kwa Hospitali ya Mnazi Mmoja na nyingine katika Soko Kuu la Darajani.


“Ujumbe wangu kwenu leo ni kutumia barakoa huku tukiendelea kuchukua tahadhari na kauli mbiu yangu ni Tahadhari kabla ya Athari,” amesema Rostam.


Akipokea msaada huo Balozi Iddi amesema: “Vita hii si ya mtu mmoja, ni vita yetu sote maana tunapigana na mtu ambaye hatumuoni. Nawasihi wananchi kuvaa barakoa na kuacha tabia ya ukaidi wa maelekezo wa serikali na wataalamu wa afya. 


“Sisi tunasemwa semwa sana kwa ukaidi, tuache ukaidi tuvae barakoa na tujitahidi sana kuzingatia maelekezo.”

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.