Habari za Punde

Virusi vya Corona: Vifo vyazidi 2,000 kwa siku moja Marekani

Rais Donald Trump pia amesema kuwa anatarajia Marekani kushuhudia kiwango cha chini cha vifo kuliko makadirio ya awali ya vifo 100,000
Marekani imekua nchi ya kwanza duniani kurekodi zaidi ya vifo 2000 vya virusi vya corona kwa siku moja.
Takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins zinaonyesha kuwa watu 2,108 wamekufa katika kipindi cha saa 24, huku kukiwa sasa na zaidi ya watu nusu milioni walioambukia virusi hivyo nchini Marekani.
Marekani hivi karibuni inaweza kuipita Italia kwa idadi zaidi ya vifo vinavyotokana na virusi hivyo kote duniani.
Lakini Mtaalamu wa Ikilu ya White House kuhusu Covid-19 anasema mlipuko unaanza kuwa wa kiwango cha chini kote nchini Marekani.
Dokta Deborah Birx anasema kuwa kuna ishara nzuri za kupungua kwa mlipuko, lakini akaonya kuwa : "Licha ya kwamba matokeo yanaweza kutia moyo, hatujafikia kilele cha maambukizi."
Rais Donald Trump pia amesema kuwa anatarajia Marekani kushuhudia kiwango cha chini cha vifo kuliko makadirio ya awali ya vifo 100,000, akiongeza kuwa: " Tunaona ishara za wazi kwamba mikakati yetu mizuri inanusuru maisha ya watu wasiohesabika".
Marekani sasa ina takribani vifo 18,693 na idadi ya visa vilivyothibitishwa ni 500,399, kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, ambacho ndicho kinachofuatilia takwimu za ugonjwa huo kote duniani.
Takriban nusu ya vifo vilirekodiwa katika eneo la New York.
Italia imeripoti vifo 18,849 huku vifo zaidi ya 102,000 vikiripotiwa kote duniani kutokana na virusi vya corona.
Watafiti walikua wamekadiria idadi ya vifo nchini Marekani ingefikia kilele chake Ijumaa na hatimae kuanza kushuka, vilishuka hadi kufikia vifo vipatavyo 970 kwa siku ilipofika Mei Mosi-siku ambayo utawala wa Trump ulikua umeitaja kama siku ya kuanza shughuli zake za kiuchumi.
"Ninataka shughuli za uchumi zifunguliwe mapema iwezekanavyo," Bwana Trump alisema katika hotuba yake ya siku ya Ijumaa Kuu aliyoitoa katika Ikulu ya White House. "Ninaweza kusema bila shaka ni uamuzi mkumbwa ambao imewahi kuufanya"
Hatahivyo, hakuna hatua ambayo itachukuliwa hadi serikali itakapofahamu kuwa" nchi itakua katika hali nzuri ya afya", alisema. "Hatutaki kurudi nyuma na kuanza tena kupambana na virusi ."
Wakazi wa New York wameshitushwa na kushuhudia: magari ya kubebea wagonjwa (ambulansi) karibu wakati wote yakiwasha vimulimuli katika mitaa iliyotorokwa na watu, miili iliyowekwa kwenye mifuko ya plasitiki inayoingizwa kwenye malori ya friji nje ya hospitali na sasa makaburi mapya yanachimbwa katika kisiwa Hart kwa ajili ya uwezekano wa kufanya mazishi ya jumla.
Makaburi yaliyoko mbali yanayoweza kufikiwa kwa njia ya maboti, ni sehemu inayofahamika kihistoria kama eneo la huzuni kasababu ni mahala pa makaburi ya jumla yasiyojengwa na mawe kutokana na kwamba ni eneo inapozikwa miili isiyo na wenyewe.
Hifadhi ya maiti ya jiji la New York ilikuwa na uwezo wa kupokea miili mingi kabla ya dharura ya mazishi ya wahanga wa mlipuko wa Covid-19. Lakini sasa lazima wahanga wa virusi wazikwe haraka ili kuepusha maambukizi.
Wakurugenzi wa mazishi wanazungumzia jinsi ongozeko la juu la vifo inavyotisha na kufadhaisha. Hata kabla ya rekodi ya wiki hii ya idadi ya vifo, baadhi ya familia zililazimika kusubiri kwa wiki moja au zaidi kuizika au kuiteketeza miili ya wapendwa wao.

Chanzo cha Habari BBC News.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.