Habari za Punde

Taasisi ya PAMOJA pamoja na RED CROSS watoa misaada wa vifaa vya kupambana na Virusi vya Corona

Mwakilishi wa Taasisi ya Pamoja inayojishughulisha na utoaji wa mafunzo ya Ufundi wa Gari na Ushoni Mbweni Bwana Christhart Scholz akimkabidhi Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Maski 10,000 kwa ajili ya kusambazwa kwa Wananchi mbali mbali Nchini.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Kulia akipokea Ndoo 65 pamoja na Mifereji 65 iliyotolewa na Taasisi ya Pamoja kwa kushirikiana na Red Cross Zoni ya Unguja.
 Nd. Shaaban Seif Mohamed akiyashukuru Makampuni, Taasisi na Jumuiya za Kiraia zinazoendelea kuiunga mkono Serikali Kuu katika mapambano yake dhidi ya kuzuia kuenea kwa Virusi vya Corona Nchini.
 Mwakilishi wa Taasisi ya Pamoja inayojishughulisha na utoaji wa mafunzo ya Ufundi wa Gari na Ushoni Mbweni Bwana Christhart Scholz akielezea Taasisi yake ilivyoamua kujitolea katika mapambano dhidi ya Corona
  Katibu Mkuu OMPR Nd. Shaaban Seif kati kati akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Taasisi ya pamoja na ile ta Red Cross Zone ya Unguja mara baada ya hafla ya makabidhiano ya Vifaa vya kupambana na Corona
Baadhi ya Vifaa vya mapambano dhidi ya Corona ambavyo ni Mifereji, Ndoo na vitakasa Mikono ambavyo Mtu anaweza kutumia bila ya kugusa kwa mkono.
                                       Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Taasisi ya pamoja iliyopo Mbweni inayojishughulisha na masuala ya Ufundi wa Vyombo vya Moto na Ushoni Zanzibar kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu Kanda ya Unguja vimetoa msaada wa Vifaa mbali mbali vya kupambana na Virusi vya Corona hapa Nchini.
Vifaa hivyo ni pamoja na Mifereji Hamsini iliyotengenezwa Kitaalamu kulingana na mazingira halisi ya kujiepusha na Virusi vya Corona, ndoo 65, Sabuni pamoja na Vitakasa Mikono.
Akikabidhi Vifaa hivyo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed, Mwakilishi wa Taasisi ya Pamoja Bwana Christhart Scholz alisema Taasisi yake imekuwa ikitoa taaluma kwa Vijana katika masuala ya Ufundi wa Gari pamoja na Ushoni.
Bwana Chriss alisema Wataalamu wake kwa vile wamebobea katika masuala ya Ufundi walilazimika na kuamua kutengeneza Mifereji iliyo salama bila ya kuguswa kwa mikono na mtumiaji mara tuu baada ya kuibuka kwa janga la kuendea kwa Virusi vya Corona hapa Nchini.
Naye kwa upande wake Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu {Red Cross} Zoni ya Unguja Nd. Soud Kudra Mponzemenya alisema Taasisi yake kwa kushirikiana na ile ya pamoja tayari wameshajipanga kusambaza Maski hizo Elfu 10,000  katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Nd. Soud alifafanua kwamba usambazaji huo utakwenda sambamba na Watendaji wa Taasisi hizo kutoa elimu kwa Wananchi hasa Vijijini juu ya namna Jamii itakavyoweza kuendelea kujiepusha na maambukizi ya Virusi thakili vya COVIC – 19 ambavyo kwa sasa vimeleta mtafaruk Dunia nzima.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed alisema msaada huo wa vifaa unaoleta faraja kwa Serikali Kuu na Jamii kwa ujumla utasambazwa maeneo mbali mbali Nchini kadri mahitaji yatakavyoruhusu.
Nd. Shaaban aliwakumbusha Watendaji wa Taasisi zinazojitolea kusaidia zana na Vifaa vya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona ni vyema wakazingatia ushauri wa Wataalamu wa Afya ili kile wanacho kitengeneza kiwe katika ubora unaohitajika Kitaalamu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.