Mwenyekiti wa Kamati ya Mwaka Kogwa Mwita Masemo Makungu wa kwanza (Kushoto) akielezea kuhusu maandalizi ya Skukuu ya Mwaka kogwa huko Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja, wa kwanza (kulia) ni Mkuu wa Kamati hiyo Ali Hatibu na (wakati kati ) ni Mjumbe wa Kamati ya Mwaka Kogwa Haji Ramadhan Haji.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
Na Bahati Habibu – Maelezo. 29/06/2020.
Wazanzibari wametakiwa kulinda kuzienzi na kuzitangaza mila na desturi zinazowatambulisha kwa mataifa mengine ili kuwa endelevu kwao na vizazi vijavyo .
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa kamati ya skukuu ya mwaka kogwa Bwana Mwita Masemo Makungu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Makunduchi katika kijiji cha Koba Wilaya ya Kusini Unguja.
Amesema miongoni mwa mila za kizanzibari ni sikukuu ya mwaka kogwa ambazo hufanyika Makunduchi kila mwaka ambazo kwa sasa zinatambulika kuwa ni sherehe za kitaifa ambapo wageni wa ndani na nje ya nchi huhudhuria skukuu hiyo .
Aidha ameeleza kuwa skukuu hiyo ni miongoni mwa mila na tamaduni zilizoletwa na watu waliotoka bara la Asia na kufikia katika kijiji hicho cha Makunduchi ambapo mwanzo walikipa jina la Kae kuu lenye maana ya sehemu inayoishi watu .
Nae katibu wa kamati hiyo Ali Khatibu Ali amesema Skukuu ya Mwaka Kogwa ni kitu wanachojivunia kutokana na kusheherekewa na watu wa matifa mbali mbali hivyo kuwa ni chanzo cha mapato kwa Taifa na nembo ya Taifa.
Sambamba na hayo amewataka watu wanaoishi Makunduchi kuwa wakarimu kwa wageni watakaohudhuria katika Skukuu hiyo kwa kuwapikia chakula cha asili na kuwatembeza sehemu za kihistoria katika kijiji chao.
Nae mjumbe wa kamati ya mwaka kogwa Haji Ramadhan amewataka vijana kuhudhuria kwa wingi katika kuadhimisha skukuu hiyo ambayo ni ya asili hasa kwa wale wenye asili ya Makunduchi.
Aidha amewataka wale wote watakaohudhuria Skukuu ya Mwaka Kogwa kuwa na tahadhari ya kujikinga na maradhi ya korona ambapo skukuu hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe 17 ya mwezi wa saba kwa mwaka huu.
No comments:
Post a Comment