Habari za Punde

ONGEZEKO LA WATU HALINA ATHARI KIUCHUMI


Naibu Waziri waFedhanaMipango, Mhe. Dkt. AshatuKijaji (Mb)

Na. SaidinaMsangina Peter Haule,WFM, Dodoma
SERIKALI imesema kuwa ongezeko la watu nchi halina athari za kiuchumi na kijamii kwa kuwa Tanzania inarasilimali za kutosha kuhudumia idadi hiyo kutokana na sera yake ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Susan Lyimo, aliyetaka ushauri wa Serikali kuhusu ongezeko la idadi ya watu lisiloendana na rasilimali zilizopo.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, Serikali katika kuhakikisha ongezeko la watu linakuwa na faida kwa nchi, pamoja na mambo mengine imeanzisha miradi kama ufuaji wa umeme wa maji Julius Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR lakini pia kuboresha huduma za afya, uimarishaji wa mtandao wa usafirishaji na elimu bure ya msingi, mambo yanayochochea uanzishwaji wa viwanda vikubwa, vidogo na vya kati vitakavyo ajiri watanzania wengi.

“Mara zote idadi ya watu imekuwa na faida zaidi kwa nchi zinazoendelea ambazo teknolojia yake haijakua kwa kiasi kinachohitajika katika kuendeleza shughuli za kiuchumi ukilinganisha na nchi zilizoendelea Duniani”,  alieleza Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa rasilimali watu inaendelea kuongezeka kwa asilimia 2.7, idadi ambayo ni fursa ikizingatiwa kuwa ardhi ipo ya kutosha na Serikali inauwezo wa kuwahudumia wananchi kwa kuwa Tanzania imezungukwa na mito, mabwawa, bandari na rasilimali nyingine.

Akinukuu kauli ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema kuwa ili nchi iendelee inahitaji vitu vitatua mbavyo ni siasa safi, uongozi bora na watu.

Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na idadi ya watu milioni 44.9 ili hali inamiliki rasilimali ardhi yenye eneo la kilomita za mraba 947,303 ambapo ardhi kavu ni 885,803 na eneo la majini 61,500 sawa na watu 65 kwa kila kilometa moja ya mraba kwa mwaka 2020, jambo linaloashiria idadi ya watu sitatizo nchini.

Aidha Dkt. Kijaji imeanza maandalizi ya awali kwa ajili ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwaka 2022.

Ametoa rai ya kuhakikisha wananchi wanamuunga mkono Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchapa kazi katika kuujenga uchumi wa viwanda ambao utasaidia kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.