Habari za Punde

Majambazi Yamjeruhi Mfanyabiashara na Kumpora Fedha na Simu.Majeruhi Aongea..


Na.Hamida Kamchalla, HANDENI.
MFANYABIASHARA Wilayani Handeni Tanga amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi na kukatwa usoni na kichwani huku akiporwa kiasi cha pesa taslimu shilingi milioni 7 pamoja na simu za mkononi zaidi ya 25.

Akiongea na Nipashe kwenye kituo cha Afya Mkata, majeruhi alijitambulisha kwa majina ya Mkombozi Mjaila (32) mkazi wa mtaa wa Kulimba A katika kata ya Mkata, wilayani Handeni, alisema kuwa alipatwa na mkasa huo usiku wa saa nane kuamkia siku ya ijumaa.

Mjaila ambaye alieleza kwamba ni mfanyabiashara katika Kata hiyo na ana duka la spea, duka la simu za mkononi na vifaa vyake pamoja na duka la uwakala wa miamala ya pesa mitandao yote ya simu

Alieleza kwamba usiku wa tukio alisikia geti likifunguliwa kwa kupigwa na vitu vizito kabla watu hao hawajaufikia mlango wa kuingilia ndani aliamka kuuendea mlango lakini kabla hajaufikia alishtuka mlango huo umefunguliwa kwa kupigwa na kitu kizito.

"Niliuendea mlango nikausukuma kwa nje lakini ukarudishwa tena ndani na watu watatu wakaingia huku wakitaka niwape pesa, kabla sijajibu mmoja akanipiga na kitu kama jembe limewekwa mpini mfupi, kwanza alinipiga usoni halafu akanipiga tena kichwani nikahisi majimaji yakidondoka kujishika usoni ni damu" alisema.

"Basi nikajua pale siwezi tena kupambana huku wale wawili wakimpiga mke wangu, basi walichukua simu zetu mbili, wakachukua na simu tano za ofisini za kurushia miamala pamoja na pesa taslimu shilingi milioni saba ambazo zilikuwa mauzo ya simu hiyo" aliongeza Mjaila.

Katika tukio hilo pia watu wengine wawili walijeruhiwa ambao walikuwa majirani wa Mjaila ambao wakati tukio likiendelea walifanikiwa kupiga simu kituo cha polisi lakini hawakuweza kupata msaada zaidi askari polisi aliyekuwa zamu aliyetajwa kwa jina la Boaz alijibu kuwa hakuwepo kituoni hapo.

Majeruhi hao ni waliojitambulisha kwa majina walisema wahalifu hao walijigawa kwenye makundi tofauti na kila kundi la watu watatu lilivamia kwa wakati tofauti ambapo baada ya kutoka kwa Mjaila waliendelea kufanya matukio ya kuwaingilia ndani kwa kuvunja milango na kuwapiga huku wakidai pesa.

Kufuatia tukio hilo mkuu wa Wilaya ya Handeni Toba Nguvila amemtaka mkuu wa polisi wilayani humo Willium Nyelu kuwahamisha kituo cha kazi polisi waliokuwa zamu siku ya tukio na kumuondoa kabisa mkuu wa kituo hicho Mnubi (KONKI)  ndani ya siku saba.

"Ocd nakuagiza kumuondoa mkuu wa kituo hiki ndani ya siku saba na ikiwezekana hata kesho asionekane hapa, mwambie Mkubwa wako huyu mtu sitaki kumuona kwenye Wilaya yangu, na hao waliokuwa zamu siku hiyo uwaondoe hapa uwapeleke wilayani na utoe wengine kwenye nidhamu kule wilayani uwalete hapa" alisema.

Aidha alimuelezea Konki kuwa ni askari asiyekuwa na nidhamu ya kazi kwa kuwadhulumu na kuchukua rushwa kwa wafanyabiashara kwenye mji huo ambapo wananchi wamekuwa wakitoa malalamiko yao kituoni hapo lakini hakuwa akiwatetea wala kuwajali akiwa kama kiongozi.

Aidha aliwapa pole kwa majeruhi wote ikiwa ni pamoja na kufika katika eneo la tukio ambako wafanyabiashara hao walivamiwa na kutoa pole kwa ndugu na majirani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.