Habari za Punde

Misa ya kumuombea Rais Mstaafu Uwanja wa Michezo wa Uhuru Jijini Dar e salaam

 Mke wa Marehemu Mzee Benjamin William Mkapa Rais Mstaafu wa Tanzania Mama Anna  Mkapa akiingizwa ndani ya eneo maalum kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya Ibada ya Misa Maalum
 Makanali na Mabrigedia wa Jeshi la Ulionzi wa Tanzania {JWTZ} wakiubeba na kuuingiza Mwili wa Marehemu Mzee Mkapa katika eneo Maalum lililotengwa kwa ajili ya Ibada ya Misa ya Kumuombea.
 Viongozi wa Kitaifa wakiongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli  wa Pili kutoka Kulia wakisimama kuashiria kuungana na Watanzania katika dua maalum ya kumuombea Mzee Bendjamin William Mkapa.Kulia ya Dr. Magufuli ni Makamu wake Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, Makamu Wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mgombea Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya CCM Dr. Hussein Mwinyi.
Mke wa Marehemu Mzee Bendjamin William Mkapa Rais Mstaafu wa Tanzania Mama Anna  Mkapa pamoja na Familia akiwa katika majonzi kwenye Misa Maalum ya kumuombea Dua Mumewe.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Watanzania kadhaa wameshiriki Misa Takatifu ya kumuombea dua Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Mzee Bendjamin William Mkapa ambayo imeandaliwa Maalum na Baraza la Maaskofu Tanzania kutokana na mchango Mkubwa uliotolewa na Kiongozi huyo wakati wa uhai wake. 
Misa hiyo iliyofanyika Katika  ilihudhuriwa pia na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli, Makamu wake Mama Samia Suuhu Hassan pamoja na Wananchi iliratibiwa na Kamati ya Kitaifa vya Mazishi chini ya Mwenyekiti wake Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa na Mwenyekiti Mwenza Balozi Seif Ali Iddi.
Ibada hiyo ya Misa Maalum ya Kitaifa iliyoongozwa na Jopo la Maaskofu, Mapadri na Watumishi wa Makanisa ilipambwa na Kwaya ya Upwakata ya Jijini Dar es salaam pamoja na nyimbo za Maombolezo za Kikundi cha Tanzania One Theatre {TOT}.
Akitoa salamu kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania MhashammAskofu Ndorobo alisema Marehemu Mzee Bendjamin William Mkapa aliwa Baba mwema sio kwa familia yake tu bali hata kwa Jamii nzima iliyomzunguuka ya Watanzania.
Askofu Ndorobo alisema Mzee Mkapa aliyependa Watu wa rika zote alijikita katika kuheshimu kila Mwanaadam sifa zilizompelekea kujenga imani na huruma za kujitolea kwake kugharamia matengenezo makubwa ya Jengo la Mapadri wa Lupaso.
Alibainisha na kuwaeleza Watanzania walioshiriki Ibada Misa hiyo kwamba Kiongozi huyo wa Awamu ya Tatu ya Utawala wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alipenda kutumia msemo mashuhuri unaoeleza kwamba kila mtu ni zawadi kwa mwenzake akimaanisha kwamba hakuna uadui kwa mwenzake.
Naye akitoa shukrani kwa Watanzania Mmoja wa wanafamilia ya Marehemu Mzee Bendjamin William Mkapa Nd. William Erio alisema Mchango Mkubwa  uliotolea na Serikali Kuu tokea kifo, maandalizi hadi mazishi Kijiji kwake utaendelea kubakia ndani ya mioyo yao wanafamilia hao.
Nd. William Erio alisema kitendo hicho cha ushiriki wa Serikali pamoja na Watanzania iwe vikundi, Taasisi, Mashirika  na hata Mtu Mmoja Mmoja katika Msiba huo kimeonyesha jinsi gani Watanzania walivyobobea kushirikiana na kushikamana katika maisha yao ya kila siku.
Hata hivyo Mwakilishi huyo wa Familia ya Marehemu Mzee Mkapa alibainisha na kutanabahisha kwamba ule uvumi uliotolewa na baadhi ya Mitandao ya Kijamii dhidi ya Mzee wao wa kutangaza mazingira ya kifo chake kinyume na uhalisia ni vyema ukaepukwa kwani unakwenda kinyume na Utamaduni wa Watanzania.
Alisema Mzee Bendjamin William Mkapa alijisikia vibaya usiku wa jumatano na kupelekwa Hospitalini kwa uangalizi wa kiafya uliobainisha kwamba alikuwa akisumbuliwa na Malaria.
Nd. William alifafanua kwamba usiku wa Alhamis  majira ya saa mbili alikwenda kumkagua na kumkuta akifuatilia matangazo ya Mubashara ya Chaguzi za Umoja wa Wanawake Tanzania { UWT} Mkoa wa Dar es salaam zilizokuwa zikiendelea Nchini kote.
Alisema baada ya muda mfupi  ghafla, Mzee Bendjamin William Mkapa alipata mshtuko wa moyo uliosababisha kukatika kwa muda wake wa kuendelea kuishi hapa Duniani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.