Habari za Punde

Bila ya Maendeleo Endelevu Yenye Tija Katika Sekta ya Kilimo Amani na Utulivu Uliopo Utatetereka Kwa Sababu ya Kudhoofika Kwa Sekta Hiyo na Kuathiri Hali ya Uhakika wa Chakula.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati akifungua Maonesho yua Maadhimisho ya Siku ya Wakulima Nanenane Zanzibar,uliofanyiuka katika viwanja vya Kizimbani Wilaya ya Magharibi "B"Unguja leo 4/8/2020.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa bila ya maendeleo endelevu yenye tija katika sekta ya kilimo amani na utulivu uliopo utatetereka kwa sababu ya kudhoofika kwa sekta hiyo na kuathiri hali ya uhakika wa chakula.

Dk. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa Maonyesho ya Nane Nane yaliyofanyika huko Langoni, Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na wananchi wengine.

Rais Dk. Shein alisema kuwa uhakika wa chakula unapoathirika mifumko ya bei huzuka kwa kile chakula kidogo kilichopo hivyo, watakuwepo watakaomudu na watakaoshindwa kukabiliana na mifumko hiyo.

Hivyo, alisema kuwa malalamiko, bughudha, hasira na chuki zitakuwa haziishi kwani njaa inazaa athari nyingi mbali ya hizo za kisaikolojia lakini hata za kiafya sambamba na kuondoa subira na uvumilivu, mambo ambayo yanaweza kupelekea utendaji wa maovu mbali mbali na kusababisha kuvunjika kwa amani na utulivu.

Rais Dk. Shein alisema kuwa ukosefu wa amani na utulivu si kama tu unazuia jitihada za maendeleo zisifanikiwe bali unateketeza mpaka yale maendeleo ambayo yalikwishafikiwa kama ambavyo nzige wanavyoteketeza mazao shambani.

“Mwenyezi Mungu atuepushie mbali nchini mwetu na awaondoshee wenzetu waliofikwa na balaa hilo la kukosa amani na utulivu”,alisisitiza Rais Dk. Shein.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuzingatia umuhimu wa uhakika wa chakula na lishe na uimarishaji wa kilimo endelevu, imekuwa ikitekeleza kwa vitendo Sheria Namba 5 ya mwaka 2011 ya Uhakika wa Chakula na Lishe Zanzibar.

Alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imeongeza bajeti ya Kilimo kutoka TZS Bilioni 88.17 ya mwaka 2019/2020 hadi kufikia TZS Bilioni 129.86 kwa mwaka 2020/2021.

Alieleza kuwa mambo mengi  katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kusisitiza kuwa miongoni mwa mambo ambayo Serikali imeyafanya ni kujenga miundombinu ya umwagiliaji maji katika hekta 1,524 Unguja na Pemba kutokana na mkopo wa dola za Kimarekani milioni 59 kutoka Benki ya Exim ya Jamhuri ya Korea.

Vile vile, alisema kuwa Serikali imekiunganisha Chuo cha Kilimo cha Kizimbani kuwa ni Skuli ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ili kukijengea uwezo zaidi ambapo jumla ya vijana 26 wanaendelea na masomo ya Shahada ya Kwanza ya Kilimo ya Chuo Kikuu hicho ili kuongeza idadi ya wataalamu wa kilimo.

Alisema kuwa Serikali imelipa kipaumbele suala la Uchumi wa Bahari (Blue Economy) ambapo kwa sasa umekuwa ni miongoni mwa vyanzo vikubwa ya kukuza uchumi hasa kwa nchi za bahari kuu zikiwemo za visiwa.

Aidha, alisema kuwa Serikali imelifufua Shirika la Uvuvi la Zanzibar (ZAFICO), ili liweze kuimarisha shughuli za uvuvi na kuleta mageuzi ya uvuvi nchini ikiwemo mkazo katika uvuvi wa bahari kuu ambao una tija zaidi.

Aliongeza kuwa kutokana na jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba, hivi sasa kilimo cha mwani kimeimarika na bei ya mwani imepanda kutoka TZS 800 hadi kufikia TZS 1,800 kwa kilo moja kwa aina ya mwani wa Cotonii na mwani wa aina ya Spinosum umetoka bei ya TZS 400 hadi TZS 700 kwa kilo moja.

Kwa upande wa sekta ya mifugo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali inaendeleza sekta hio kwa hatua kadhaa ikiwemo kutoa elimu kwa wafugaji, kutoa huduma za chanjo na tiba kwa wanyama, Serikali imenunua mtambo wa kutengenezea chakula cha kuku na samaki pamoja na kuwasomesha vijana 45 udaktari wa wanyama.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa kwa upande wa sekta ya uvuvi, mipango ya baadae ni kuanza ujenzi wa diko na soko la kisasa la samaki katika eneo la Malindi litakalotoa huduma kwa wananchi wapatao 6,500 ambapo ujenzi wa soko hilo tayari umeshaanza kutokana na msaada wa TZS Bilioni 18 kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shen alisema kuwa mipango ya baadae pia, itahusika katika kufanya tafiti mbali mbali kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mazao bora ya kilimo, mifugo na ya baharini.

Akimalizia hotuba yake  Rais Dk. Shein aliwanasihi wananchi kwamba waendeleze ustaarabu walionao wakati watakapokuwa wanashiriki katika shughuli za Kampeni za uchaguzi zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Aliwataka wananchi kuelewa kuwa uchaguzi ni tukio la kidemokrasia linalofanyika  mara moja lakini wananchi watakuwa wanaendelea kuhitajiana katika shughuli zao mbali mbali za kijamii kila wakati, hivyo ni lazima wawe makini.

Aliongeza kuwa hilo ni jambo la kheri ambalo ni la kubadilishana uongozi na badala yake isiwe chanzo cha kutukanana na kubezana kwani demokrasia ni kutafuta nafasi ya kuongoza kwa ridhaa ya wananchi walio wengi bila ya kutumia nguvu.

“Napenda kuyazungumza hayo kwani mimi ndie Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi niliopo hivi sasa  lazima nikutanabaisheni wananchi wa Zanzibar kwani tunapendana”,alisema Rais Dk. Shein.

Nae Kaimu Waziri wa Wizara ya Kilimo, maliasili, Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri alimpongeza Rais Dk. Shein kwa wazo lake la kuanzisha maonyesho hayo.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mariam Abdalla Sadalla alisema kuwa kauli mbiu ya maonyesho hayo mwaka huu ni “Tudumishe amani na utulivu kwa maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini”.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa kilele cha maonyesho hayo ni tarehe 8 mwezi huu ambapo Taasisi 219 zimeshiriki na kuzipita zile za mwaka jana ambazo zilikuwa 172 huku akizisisitiza zile Taasisi zilizopewa maeneo ya kudumu kuyajenga ili kuepusha gharama za ujenzi zinazofanywa na Wizara yake kila yananapofika maonyesho.

Alisema kuwa maonyesho hayo yamefanyika sambamba Unguja na Pemba  na yamegharimu TZS milioni 71.1 ambapo washiriki wengine wakiwemo wajasiriamali wamechangia TZS milioni 12.5.

Katika ufunguzi huo, Pia Rais Dk. Shein alipata fursa ya kutembelea mabanda ya maonyesho pamoja na kujionea vifaa mbali mbali vya uvuvi, kilimo na ufugaji na kupata maelezo ikiwa ni pamoja na kuyazindua matreka mapya 20.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.