Habari za Punde

Tanzania Yaendelea Kufanya Vizuri Mfumuko wa Bei Ikilinganishwa na Kenya na Uganda


Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi Ruth Minja akizungumza na waandishi wa habari  wa vyombo mbalimbali leo Jijini Dodoma kuhusu mfumuko wa bei kwa mwezi wa Agosti, 2020 ambapo Tanzania  ni asilimia 3.3 na inaendelea kufanya vizuri ikilinganishwa na nchi za Kenya kwa asilimia 4.36 na Uganda asilimia4.7



Na Mwandishi wetu- Dodoma                                                                                                                  
Tanzania yaendelea kufanya vizuri Mfumuko wa  Bei wa Taifa kwa mwaka ulioshia mwezi Julai, 2020 ambao ni asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2020 ikilinganishwa na Kenya asilimia 4.36 na Uganda asilimia 4.7

Akizungumza leo, Jijini Dodoma Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Bi Ruth Minja amesema kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2020 umeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2020.

Akifafanua amesema kuwa baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka kwa mwezi Julai ni pamoja na; unga wa mahindi kwa asilimia 7.9, mtama asilimia 4.8, unga wa muhogo kwa asilimia 3.0, dagaa asilimia 3.8, matunda asilimia 4.0, mbogamboga asilimia 9.6.

Aliongeza kuwa, Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi Julai, 2020 zikilinganishwa na zile za Julai, 2019 ni pamoja na; mavazi kwa asilimia 2.8, gesi ya kupikia kwa asilimia 5.9, samani kwa asilimia 2.7, gharama za utengenezaji na ukarabati wa nyumba kwa asilimia 6.2 na mkaa kwa asilimia 11.6.

“Nchini Kenya Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2020 ni asilimia 4.36 kutoka asilimia 4.59 kwa mwaka unaoishia mwezi Juni 2020, kwa upande wa Uganda, Mfumuko wa Bei kwa mwaka ulioishia Julai, 2020 umeongezeka hadi asilimia 4.7 kutoka 4.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2020”, Alisisitiza Bi Minja

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imepewa mamlaka ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji na usambazaji wa Takwimu Rasmi nchini ikiwa ni pamoja na takwimu za Mfumuko wa Bei kwa ajili ya matumizi ya Serikali na wadau wa takwimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.