Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo
Dkt.Harrison Mwakyembe (mwenye kofia) akisalimiana na viongozi wa Kituo cha
Redio cha Hopeje kilichopo Mkoani Mtwara
mara baada ya kukizindua
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo
Dkt.Harrison Mwakyembe (mwenye kofia) akisikiliza maelezo kuhusu Kituo cha
kurusha Matangazo cha Shirika la Utangazaji la Taifa TBC kilichopo Lilungu
mkoani Mtwara kutoka kwa Mhandisi wa Shirika hilo Bibi Upendo Mbele wakati alipotembelea kituo hicho
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo
Dkt.Harrison Mwakyembe (mwenye kofia) akisikiliza maelezo kuhusu Kituo cha
kurusha Matangazo cha Shirika la Utangazaji la Taifa TBC kilichopo Lilungu
mkoani Mtwara kutoka kwa Fundi Mitambo wa Shirika hilo Bw.Hamis Kalanje wakati alipotembelea kituo hicho Agosti
07,2020.Kulia ni Mhandisi wa Shirika hilo Bibi.Upendo Mbele.
Na Shamimu Nyaki
–WHUSM-Mtwara
Serikali imeendelea
kuimarisha usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa TBC kwa idhaa za TBC Taifa na TBC Fm katika Mikoa ya Lindi
na Mtwara baada ya kufunga Mtambo wenye nguvu
ya kilo wati moja (1KW) kwa kila idhaa hizo.
Akizungumza wakati
alipotembelea kituo cha kurusha matangazo ya redio hizo cha Lilungu Mkoani
Mtwara Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe
amesema, kuimarika kwa usikivu wa TBC katika mikoa ya kusini ni jitihada za Serikali
kuhakiksha wananchi wake wanapata taarifa ambazo zinaelezea utekelezaji
unaofanywa na Serikali kwa ajili ya wananchi wake.
“Wananchi wana haki
kikatiba ya kujua Serikali imewafanyia nini,na ili wajue ni kupitia vyombo vya
habari vya kuaminika kama TBC,hivyo upanuzi wa usikivu wa shirikia hili
umesaidia wananchi kupata habari zinazohusu nchi yao” alisema Dkt.Mwakyembe.
Aidha Dkt.Mwakyembe
amesema kuwa kuna changamoto ya miundombinu
ya kufikia maeneo mbalimbali ya mitambo ya TBC hasa barabara kutokana na
Mitambo hiyo kusimikwa maeneo ya miinuko,ambapo ameahidi kuwasiliana na Mamlaka
husika ziweze kushughulikia changamoto hiyo.
Kwa upande wake
Mhandisi wa Shirika hilo Bibi.Upendo Mbele amesema kuwa fedha za maendeleo
zilizotengwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya usikivu zimesaidia
kuboresha mradi wa Kilwa na Ruagwa ambao utasaidia katika kuongeza nguvu ya
usikivu.
“Kituo hiki cha
Mtwara kimepatikana kutokana na juhudi na mipango ya shirika kutumia mafundi wa
ndani na vipuri vya vituo vya Namanga,Rombo,Tarime,Kibondo na Mbamba
Bay ambavyo vilitumika kuunda mtambo huu”alisema Bibi Upendo.
Naye Fundi Mitambo wa
Shirika hilo Bw.Hamis Kalanje amesema kuwa kituo hicho kimeanza kurusha
matangazo kwa mitambo ya FM kwa idhaa za TBC TAIFA kwa masafa ya 87.7Mhz na TBC
FM kwa masafa ya 89.7Mhz kwa uwiano wa nguvu ya kilo wati moja kwa kila mtambo.
“Baada ya kufunga
mtambo huu usikivu umeongezeka katika maeneo ya Msimbati,
Mtendachi,Kilambo,Mayanga,Mikindani,Nanguruwe,Mpapura na
Ndumbwe”alisema Bw.Kalanje.
Katika hatua nyingine
Waziri huyo amezindua kituo cha redio cha Hopaje FM (Nyakati za Kusisimua)
kilichopo Mtwara ambapo amewahimiza wanahabari wa kituo hicho kufanya kazi kwa
weledi na kufuata miiko ya taaluma ya habari,ambapo pia amesisitiza kutoa
habari zinazoelezea utekelezaji wa serikali kwa wananchi wake na kusisitiza
amani katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment