Habari za Punde

Viwanda Vyatakiwa Kuzalisha Maziwa Kwa Wingi Nchini Kupunguza Uingizwaji wa Maziwa Kutoka Nje ya Nchi.-Waziri Mpina

Mwenyekiti wa chama cha ushirika wa wafugaji wa ng'ombe wa maziwa mkoa wa Tanga (TDCU) Hamid Mzee akieleza jambo wakati wa ziara hiyo

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
VIWANDA vya kuzalisha maziwa kwa njia ya mchakato nchini vimetakiwa kuzalisha maziwa kwa wingi na kukuza soko ili kukwepa uagizwaji wa maziwa kutoka nje ya nchi.

Waziri wa kilimo, ufugaji na uvuvi Luhaga Mpina aliyasema hayo juzi alipotembelea kiwanda cha maziwa cha maziwa cha Tanga fresh jijini Tanga alipokuwa kwenye ziara fupi ya kikazi.

Mpina alisema kuwa hakuna sababu ya kuagizwa maziwa nchini kutoka nje kutokana na kuwepo kwa mifugo ya kutosha ambayo ikiwekeka utaratibu mzuri itajitosheleza kuzalisha bidhaa hiyo kwa kiasi cha kutosha.

"Tumeweza kuona changamoto na fursa mlizonazo kuanzia kwenye mifugo mpaka uzalishaji na masoko, nawapongeza sana Tanga fresh kwasasa kwa kazi nzuri mnayofanya, hakuna sababu ya watu kuingiza maziwa kutoka nje ya nchi wakati tuna mifugo ya kutosha kutupatia maziwa" alisema Mpina.

Aidha Mpina aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kununua maziwa kwa wafugaji kwa bei itakayomfanya mfugaji kunufaika na uzalishaji wa mifugo yake jambo ambalo litaleta alieleza kwamba limetokana na kutoweka bei elekezi ya kununulia maziwa kwa mfugaji.

"Changamoto nyingine ni hii ya bei, tulipotangaza ununuzi wa maziwa hatukuweka bei elekezi lakini ningependa bei ya maziwa kwa mfugaji iwe ni shilingi mia nane kwa lita, nitafurahi na nitapenda kwa kila kiwanda kinunue maziwa kwa mfugaji kwa bei hiyo" alibainisha.

Mpina alifafanua kuhusu changamoto ya magonjwa kwa mifugo ambapo alisema kuwa ili kupata maziwa kwa wingi na yenye ubora ipo haja ya kuangalia ukuaji wa mifugo hususani katika magonjwa, lishe na chanjo pamoja na mazingira wanayoishi.

"Mkurugenzi wa nyanja za malisho muende muwatembelee wafugaji kule kwenye maeneo yao muone maeneo wanayofugia, vyakula wanavyoipatia mifugo na hata chanjo ili kuwakinga na magonjwa" alisema Mpina.

Naye Mwenyekiti wa chama cha ushirika wa wafugaji wa ng'ombe wa maziwa mkoa wa Tanga (TDCU) Hamid Mzee changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakumba wafugaji ni migogoro ya ardhi na kueleza kwamba wanatakiwa kuweka mpango mkakati ili kutengeneza maligafi kwa wingi na kukwepa ukosefu wa bidhaa hiyo.

Mzee aliiomba serikali kuangalia kwa ukaribu wafugaji na kuwawezesha kuzalisha kwa tija huku wakinufaika na mifugo yao kwani tatizo la uzalishaji lililokuwepo awali kwa sasa limepungua na kufanya soko kuongezeka.

"Migogoro ya kunyang" anyana ardhi ndani ya kipindi cha miaka kumi iliyopita hatukuweza kuzalisha mitamba ya kutosha na kusababisha tatizo la kuoungua kwa uzalishaji lakini sasa soko limerudi tena,  niiombe serikali ijitahidi kuliangalia hili suala ili wafugaji wetu wanufaike na mazao yao ya mifugo" alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.