Habari za Punde

WAAJIRI WENGI WAFURAHIA MFUMO WA KUJISAJILI NA KUTOA TAARIFA ZA AJALI AU MAGONJWA WCF KUPITIA MTANDAO


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kushoto), akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Masha Mshomba kwenye maonesho ya Nanenane kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu Agosti 8, 2020. Katikati ni Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Profesa Tadeo Satta.

Na mwandishi wetu, Simiyu Agosti 8, 2020
KUMEKUWA na mwitikio mkubwa kwa waajiri waliofika kwenye banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kutaka kujua jinsi ya kujisajili na kuwasilisha madai ya fidia kupitia mtandao yaani Online Registration System-WCF Portal (ORS), Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Masha Mshomba amesema.

Bw. Mshomba ameyasema hayo Agosti 8, 2020 kwenye banda la Mfuko huo katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

“Imekuwa ni nafasi nzuri sana ya mfuko kuelezea huduma zake hususan huduma mpya ambazo zinapatikana kupitia mtandao zinaanzia katika hatua ya mwanzo kabisa ambayo mwajiri anataka kujisajili katika mfuko, kuleta michango kupitia mtandao lakini kubwa zaidi ni jinsi ya kutoa taarifa (kuwasilisha madai) endapo mfanyakazi amepata ajali au ugonjwa utokanao na kazi.” Alisema Bw. Msomba.

Alisema katika maonesho hayo waajiri wengi walifika katika banda la WCF wakiwa na shauku kubwa ya kuelewa jinsi ya kujisajili na kuwasilisha madai kupitia mtandao.

“Tumepata mwitikio mzuri sana karibu waajiri 200 wamefika kujisajili kupitia mtandao na hii inaonyesha ni jinsi gani suala la matumizi ya mtandao limerahisisha sana utoaji wa huduma za mfuko na hii inakwenda sambamba na azma nzima ya serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye anatamani sana kuona taasisi hizi za serikali zikitumia huduma hizi za mtandao kwasababu anajua wazi kwamba zinapunguza gharama na zinaleta ufanisi katika utendaji wa taasisi na taifa zima kwa ujumla.” Alisisitiza.

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni taasisi ya serikali yenye jukumu kubwa la kulipa fidia kwa mfanyakazi aliyeumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi na walengwa hasa ni watumishi wote kutoka sekta ya Umma na Binafsi Tanzania bara.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Masha Mshomba (kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga kwenye banda la WCF katika maonesho ya Nanenane yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Bw.Abdulmajid Nsekela (kushoto) akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la WCF kwenye maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabidni mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Masha Mshomba (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Hosea Kashimba wakiwa mbele ya banda la WCF katika maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.Gaana wa Benki Kuu wa Tanzania Profesa Florens Lupoga akitembelea banda la WCF katika viwanja vya Nanenane viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.
Afisa Uhusiano Mwandamizi Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Sebera Fulgence (kulia) akiwapa elimu wanafunzi waliofika kwenye banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi wakiongozwa na mwalimu wao ili kujifunza kuhusu masuala ya fidia kwa Wafanyakazi kwenye maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.