Habari za Punde

Balozi Seif afika Ubalozi mdogo wa India kuomboleza kifo cha Rais wa Zamani wa Nchi hiyo Shri Pranab Mukherjee

Balozi Mdogo wa India Shri Bhagwant Singh akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisi ya Ubalozi wa Nchi hiyo Migombani kusaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia Kifo cha Rais wa zamani wa India Shri Pranab Mukherjee.
Balozi Seif Ali Iddi akimpa pole Balozi Mdogo wa India Shri Bhagwant Singh pamoja na Watendaji wake kabla ya kutia saini Kitabu cha Maombolezo ya Kifo cha Rais wa 13 wa India.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitia saini Kitabu cha Maombolezo kufuatia Kifo cha Rais wa zamani wa India Shri Pranab Mukherjee kwenye Ubalozi Mdogo wa India uliopo eneo la Migombani. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kushoto akimuaga rasmi Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar Shri Bhagwant Singh  baada ya kusaini Kitabu cha aombolezo.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na othman Khamis, OMPR

Maombolezo ya siku Saba Nchini India kufuatia kifo cha Rais wa Zamani wa Nchi hiyo Shri Pranab Mukherjee kilichotokea Jumatatu ya Tarehe 31 Agosti 2020 yanaendelea Nchini humo huku Ubalozi wa Nchi hiyo Nchini Tanzania umeweka kitabu cha Maombolezi kwa ajili ya msiba huo.

Visiwani Zanzibar Ubalozi Mdogo wa India wenye Ofisi yake Mtaa wa Migombani umeanza kupokea Viongozi mbali mbali wa Kiserikali, wanadiplomasia na hata Wananchi wa kawaida wakiwemo wale wenye asili ya India kutia saini kitabu hicho cha maombolezi cha Kifo cha Shri Pranab akiwa Rais wa 13 wa India.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mapema asubuhi alifika kwenye Ofisi hiyo ya Balozi Mdogo wa India kutia saini kitabu hicho akiungana na Viongozi mbali mbali Duniani kuonyesha kuguswa kwake na Kifo cha Kiongozi huyo aliyebobea katika masuala ya Siasa, Historia na mahusiano ya Kimataifa.

Shri Pranab Mukherjee aliyefariki kutokana na ugonjwa na Moyo alianza harakati za masuala ya Kisiasa akitokea fani ya Habari licha ya kuwa na Shahada ya Pili ya Historia na Sayansi ya Siasa alizaliwa Tarehe 11 Disemba Mwaka 1935 katika kijiji kidogo cha Mirati Maghaibi mwa Wilaya ya Bengal akiwa miongoni mwa Watoto wa Wapiganaji wa Ukombozi wa India.

Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wananchi wake aliwaomba Wananchi wa India kupitia Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar Shri Bagwant Singh kuwa na moyo wa subra ndani ya kipindi hichi cha msiba mzito wa kuondokewa na Kiongozi wao huyo.

Alisema kifo ambacho humgusa moja kwa moja kiumbe awe Mwanaadamu au mnyama ni wajibu usiopingika. Hivyo wale wanaopatwa na mitihani hiyo wanapaswa kuikubali hali hiyo nzito ili kupata utulivu wa nafsi.

Shri Pranab Mukherjee ni miongoni mwa viongozi wa zamani wa India waliowahi kufanya kazi katika Serikali ya Waziri Mkuu wa Zamani Indira Gandhi aliyewahi kukabidhiwa nyadhifa mbali mbali ikiwemo Waziri katika Sekta tofauti iliyoanzia katika Miaka ya Sabini.

Katika Nyanja za Kimataifa Shri Pranab Mukherjee aliwahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Fedha wa Dunia {IMF}, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Bara la Asia ikiwemo pia Benki ya Maendeleo ya Bara la Afrika.

Uzoefu huo umemuwezesha kujenga nguvu zilizompatia fursa ya kuwa miongoni mwa Viongozi Waandamizi wa India waliopewa jukumu la kushiriki kwenye Vikao na Mikutano mbali mbali ya Kimataifa kwenye Taasisi za Umoja wa Mataifa.

Uwajibikaji mkubwa wa Shri Mukherjee Kitaifa na Kimataifa ulimjengea sifa zilizopelekea kuzawadiwa tuzo na nishani mbali mbali za Kimataifa kutoka Vyuo Vikuu tofauti Ulimwenguni katika Nyanja za Fedha, Uchumi, Biashara na hata kusuluhisha migogoro ya Kisiasa kwenye Mataifa yaliyokumbwa na Mogogoro.

Shri Pranab Mukherjee aliyependa kusoma, kufuatilia Muziki, fani ya Sanaa na masuala ya Utamaduni ameacha Kizuka Mmoja na alibahatika kupata Watoto Wawili na Mjukuu Mmoja.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.