Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibare Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Balozi Mdogo wa China Zanzibar Mhe. Xie Xiaowu.

Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaowu akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika kuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake wa Miaka Minne wa Utumishi wa Kidiplomasia Nchini Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaowu ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiaowu wa Pili kutoka Kushoto akisisitiza umuhimu wa Nchi yake kuendelea kushirikiana na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika uhusiano wao wa Kihistoria wa muda mrefu.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.                                                                                                 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inajivunia kasi kubwa iliyopiga ya Miradi ya Kiuchumi na Maendeleo ndani ya kipindi kifupi kutokana na usaidizi Uandamizi mkubwa unaoendelea kufanywa na Taifa Rafiki la Jamuhuri ya Watu wa China.

Alisema ipo miradi ya wazi inayoshuhudiwa na Wananchi pamoja na Jumuiya za Kimataifa ambayo tayari inaendelea kuwafaidisha Watu wakati mengine ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika kwake ikilenga kustawisha maisha ya Jamii sambamba na kuongeza pato la Taifa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiuow aliyefika Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kuaga Rasmi baada ya kumaliza muda wake wa Miaka Minne ya Utumishi wa Kidiplomasia Visiwani Zanzibar.

Alisema Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa Mshirika wa karibu na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla mara tuu bada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ambapo imekuwa ikiunga mkono Miradi ya Maendeleo katika Taasisi mbali mbali ya Umma na hata zile Binafsi.

Balozi Seif alibainisha kwamba ipo Miradi iliyoanzishwa kwa Ushirikiano kati ya pande hizo mbili kama Ujenzi wa Kiwanda cha Sukari, Mahonda, Viwanda vya Sigara na Viatu Maruhubi, Mashamba ya Kilimo Upenja na Bambi sekta zilizotoa mchango mkubwa wa Kitaalamu na ajira kwa Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alimpongeza na kumshukuru Balozi huyo Mdogo wa China aliyepo Zanzibar kwa usimamizi wake mkubwa wa ushirikiano wa Kidiplomasia uliopelekea kuibuka kwa miradi mingi ya Kiuchumi na Maendeleo ndani ya kipindi chake cha Miaka Minne hapa Zanzibar.

Balozi Seif aliitaja baadhi ya Miradi hiyo kuwa ni pamoja na uimarishaji wa Miundombinu ya Sekta ya Maji, Ujenzi wa Skuli za Sekondari, huduma za Afya hasa kipindi cha mpito wakati wa mripuko wa Homa Kali ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona.

Alisema China licha ya kuwa na Idadi kubwa ya Watu wake wanaokadiriwa kufikia Zaidi ya Bilioni 1.4 wanaohitaji huduma za msingi katika Ustawi wao lakini bado imezingatia kuendelea kuiunga Mkono Zanzibar katika kuona Wananchi wa Zanzibar pia wanaendelea kudumisha Ustawi wao.

Mapema Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Xiuow alisema anajisikia faraja kuona kwamba Miradi Mikubwa iliyoanzishwa  ndani ya kipindi chake cha Miaka Minne iliyopata Msukumo kutoka Jamuhuri ya Watu wa China imekamilika na mengine ikiwa katika hatua za mwisho.

Balozi  Xie alitolea mfano Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Abdullah Mzee iliyopo Mkoani Pemba, Utanuzi wa Uwanja Wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar Viwanja vya Michezo vya Mao Tse Tung, Jengo la Skuli iliyopo Mtaa wa Mombasa, uwekaji wa Taa za Bara barani katika maeneo ya Miji pamoja na usimamizi wa mafunzo ya juu kwa Wanafunzi wa Zanzibar Nchini China. 

Alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba licha ya kumaliza muda wake wa Utumishi Zanzibar lakini Uongozi Mpya utakaoshika nnafasi yake utaendelea kudumisha uhusiano wa Kidugu wa Kihistoria unaoendelea kushamiri kila siku kati ya pande hizo mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.