Habari za Punde

Mbunge Mteule Viti Maalum Nitakuwa Kiungo Kati ya Ngo's, Bunge, Serikali na Wafadhili Kuleta Maendeleo Endelevu -Neema Lugangira.

 

Mbunge Mteule Viti Maalum Kundi la Asasi za kiraia Tanzania bara Neema Lugangira (kulia) akizungumza jambo na baadhi ya viongozi wa Mtandao wa Vikundi vya wakulima wadogo Tanzania (MVIWATA) alipotembelea ofisi hiyo.

Na.Assenga Oscar

MBUNGE Mteule Viti Maalum kundi la Asasi za kiraia Tanzania bara kwa tiketi ya CCM Neema Lugangira, amesema kuwa atakuwa kiunganishi kati ya Asasi za kiraia(NGO'S), bunge, serikali, wafadhili na chama ili kubadilishana mawazo katika kuleta maendeleo endelevu.

Neema ameyasema hayo wakati alipotembelea Mtandao wa Vikundi vya wakulima wadogo Tanzania (MVIWATA) mkoani Morogoro ili kujua changamoto zinazo wakabili na namna ya kuzitatua. 

Ameeleza kuwa kwa kuongea na wadau hao anapata fursa ya kupata mambo ya kujadili yaliyomo kwenye ilani ya CCM yanayohusiana na Asasi hizo na kuweza kubadilishana mawazo yatakayosaidia kwenye utekelezaji.

Akizungumzia maeneo yaliyoguswa na ilani ya CCM amesema lengo kubwa ni kuongeza tija katika kilimo ili kusaidia viwanda, kuimarisha miundo mbinu na uzalishaji, kumsaidia mkulima kuzalisha na kupata masoko, usimamizi wa mazao ya kimkakati, lishe na kuzijengea uwezo Asasi za ndani.

Naye Mkurugenzi wa MVIWATA Stephen Ruvuga akitoa shukrani zake kwa chama na serikali amesema kwa kitendo hicho cha kiongozi kuwatembelea na kujua changamoto zao wanatarajia kuwepo kwa maelewano mazuri kati ya serikali na Asasi hizo, hali itakayochochea maendeleo kwa haraka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.