Habari za Punde

Waandishi Watakiwa Kuweka Mbele Mtazamo wa Kijinsia Kumuinua Mwanamke.

Na.Mohammed Khamis -TAMWA Zanzibar.
Waandishi wa Habari Zanzibar wametakiwa kuweka mbele zaidi mtazamo wa kijinisia katika kazi zao za kila siku kwa lengo la kumuinua mwanamke katika harakati mbali mbali za uongozi,kiuchumi na nyenginezo.
Akifungua mafunzo ya siku moja Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Zanzibar Dkt,Mzuri Issa Ally katika ofisi za Chama hicho huko Tunguu Wilaya ya kati Unguja alisema waandishi wa habari wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika jamii.
Alieleza kuwa  waandishi wa habari wanawajibu mkubwa wa kuibadili jamii kutokana na kazi zao za kila siku hivyo wasikubali kuona jamii inamkandamiza mwanamke katika shughuli zao za kila siku.
Pia alisema waandishi wa habari hawana budi kuwa na jicho la tatu ambalo litaangazia zaidi maswala ya kijinsia kwa kuwa bado Zanzibar  baadhi ya wanawake wamekua wakikosa fursa muhimu kwa mitazamo isiokua na mashiko.
Alisema hadi sasa kwenye jamii ya Zanzibar wapo miongoni mwa watu wanaendelea kuwatafsiri wanawake kwa jicho baya na kuwaona kama watu wasiopaswa kufanya au kupewa nafasi yoyote hile kubwa.
Kwa mazingira hayo aliwataka waandishi wa habari kubadili mtazamo huo potofu na kisha  kumlinda mwanamke ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki kwa nafasi yake.
‘’Wanawake wana uwezo mkubwa zaidi kinyume na inavoelezwa na watu kwenye maeneo yetu lakini kwa sababu ya dhana potofu wanawake wanawekwa nyuma msikubali waandishi kabadilisheni hili’’aliongezea.
Akiendelea kufafanua zaidi  Dkt,Mzuri alizungumzaia kuhusu ushiriki wa wanawake na uongozi na kueleza kuwa licha ya mwamko mkubwa wa wanawake waliouonesha katika ushiriki wao kuwania  nafasi mbali mbali za uongozi lakini inaonekana bado jamii haimkubali mwanamke.
Alieleza kuwa wakati wanawake wengi walishindwa katika mchakato wa kura za maoni ambazo wajumbe walio wengi hawakuwapa nafasi wanawake hatimae wanawake wengi walijikuta wakiangushwa.
Akifafanua zaidi alisema inasikitisha sana kuona hadi leo iwapo kuna mwanamke atajitokeza kugombea nafasi ya uongozi kupitia vyama vya siasa huchunguzwa sana kuliko mwanaume jambo ambalo alisema halileti usawa.
Alisema  ifike wakati kila mtu anapaswa kufahamu haki ya kuwa kiongozi ni ya kila mmoja na haipaswi kubaguliwa kama wanavyofanya baadhi ya watu kwenye jamii.
Awali akiwasilisha mada kwa wanahabari hao Zanzibar Hawra Shamte alisema waandishi wa habari Zanzibar bado wana kazi kubwa ya kuwasaidia wanawake.
Alisema wanawake wengi bado Zanzibar wamekua wakikosa fursa muhimu ambapo anaamini iwapo vyombo vya habari vingekua makini na kufanya vyema katika Nyanja ya jinsia kusingeibuka baadhi ya changamoto.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo Salum Vuai alisema yamewajengea uwezo mkuwa kwa kuwa baadhi ya waandishi wamekua wakishindwa kutambua umuhimu wa jisnia katika vyombo vyao vya habari.
Alisema kutokana na mafunzo hayo ya Tamwa-Zanzibar anaamini walio wengi watafaidika na hatimae kuibadilisha jamii ili iweze kutoa fursa na kumuamini mwanamke.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.