Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano Maalum la Wanawake "Umoja Wetu Wanawake Ndio Nguvu Yetu" lililofanyika katika ukumbi wa Afisi ya CCM Mkoa wa Mjini Kichama Amani Jijini Zanzibar.
Mapema Mgeni Maalum wa Kongamano hilo Mama
Mwanamwema Shein katika hotuba yake alieleza kuwa Kongamano hilo maalum
limeandaliwa na Umoja wa Wake wa Viongozi kwa kushirikiana na Umoja wa Wanawake
wa Tanzania (UWT).
Mama Shein alitumia fursa hiyo kuwasihi wanawake
pamoja na wananchi wote kuzingatia umuhimu
wa kutunza amani iliyopo hivi sasa na baada ya uchaguzi.
Alieleza kuwa bila ya amani hakuna lolote
linaloweza kufanikiwa kwani bahati mbaya ni kuwa wanawake na watoto ndio
wanaoathirika sana wakati amani na usalama vinapotoweka.
“Tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie tuweze
kushiriki katika uchaguzi Mkuu kwa amni, salama na utulivu”,alisema Mama Shein.
Mama Shein alitoa pongezi zake kwa wanawake kwa
kuchagua kauli mbiu ya Kongamano hilo isemayo “Umoja wetu ndio nguvu yetu”, na
kueleza kuwa anakubaliana na kauli mbiu hiyo kutokana na ukweli na umuhimu
wake.
Alisema kuwa wanawake wakiwa pamoja ndio watakuwa
na nguvu zaidi ya kufanya uwamuzi unaofaa kwa faida yao na kusisitiza kuwa
uwamuzi unaofaa hivi sasa ni kuipigania CCM ili ishinde katika nafasi zote za
uongozi katika uchaguzi Mkuu ujao.
“Tusisahau maneno ya wazee wetu yasemayo “Umoja ni
nguvu na utengano ni udhaifu”.
Aidha, Mama Shein alisema kuwa umoja na mshikamano
ni mambo ya msingi katika kukipatia ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi na
kuwataka wagombea wa nafasi mbali mbali katika chama hicho ni vyema wavunje
makundi yao na waunge mkono wagombea wote waliopitishwa na CCM na kuendelea
kuwa kitu kimoja.
Pamoja na hayo, alisema kuwa Mgombea wa Urais wa
Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Mwinyi ni mtu makini, mwenye uzoefu
mkubwa katika uongozi na anaependa maendeleo.
Nae Mgeni rasmi katika Kongamano hilo Mwenyekiti
wa (UWT) Gaudentia Kabaka aliwataka wagombea wote wanawake waliogombea nafasi
mbali mbali za uongozi kuwa kitu kimoja na kufahamu kuwa huo walioupata ni
uteuzi si ushindi kwani wapo walioshinda kwa kura nyingi lakini hawakuteuliwa
na badala yake wameteuliwa wale wenye kura kidogo.
Alieleza kuwa CCM ni chama kikubwa na kueleza kuwa
wanawake wanajukumu kubwa la kutafuta kura za Ubunge, Uwakilishi, Udiwani
pamoja na Urais wa Jamhuri ya Muungano na Urais wa Zanzibar.
Alitumia fursa hiyo kuupongeza mchakato wa
kuwapata viongozi ndani ya CCM ulivyofanyika na kuwataka wagombea ndani ya CCM kufahamu
kuwa katika mchakato huo wa kuwapata wagombea hakukuwa na chuki wala uadui
kwani CCM ina katiba nzuri inayokwenda kwa kanuni na taratibu nzuri.
Kwa upande wake kiongozi wa Umoja wa Wake wa
Viongozi MamaAsha Balozi alitoa pongezi kwa Mama Shein kwa ushirikiano wake
mkubwa katika kufanikisha Kongamano hilo pamoja na kueleza hatua zilizofikiwa
na Umoja huo.
Katika Kongamano hilo Mada mbali mbali zilitolewa
ikiwemo “Wanawake Kutokata Tamaa”, aliyotolewa Balozi Amina Salum Ali, Waziri
wa Biashara na Viwanda, Mada ya “Amani na Utulivu”,iliyotolewa na Sharifa Abeid
Salum kutoka Ofisi ya Makamo wa Pili wa rais wa Zanzibar na Mada ya Tatu
ilikuwa ni “Uzalendo na Mshikamano” iliyotolewa na Catherine Peter Nao Katibu
wa Idara ya Uenezi Zanzibar.
Sambamba na hayo Kongamano hilo liling’arishwa na
burudani mbali mbali kikiwemo kikundi cha Taarab cha “Big Star” cha Chama Cha
Mapinduzi (CCM) huku Dj Maarufu wa Zanzibar Kul Para akionesha mbwembwe zake
katika tasnia ya muziki.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment