Na Mwashungi Tahir Maelezo 18-11-2020.
Kuwepo kwa mashirikiano ya utoaji wa taarifa za uhakika katika taasisi za Serikali kutasaidia kupata takwimu zilizo sahihi ambazo zitasaidia katika kupanga mipango bora ya maendeleo ya Nchi.
Ameyasema hayo Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Zanzibar Dr Juma Malik Akili kwa niaba ya ya Katibu Mtendaji wa Timu hiyo leo huko katika Ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar ilioko Mazizini wakati wa Maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika.
Amesema kwamba maendeleo yoyote ya kweli katika Nchi zote duniani yanatokana na Takwimu zinazozalishwa kwa mifumo mizuri ambazo zitakuwa za kweli na za uhakika.
Amesema Serikali ya awamu ya nane imeanza kuleta mabadiliko ya haraka katika Serikali ikiwa na lengo ya kuweka mipango ilio bora katika kupatikana uhakika wa Takwimu zilizo sahihi.
“Wito wangu kuwa na mashirikiano na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar katika utoaji wa takwimu zilizo sahihi”, alisema Naibu huyo.
Nae Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar Mayasa Mahfoudh Mwinyi amesema ikiwa Afrika inaadhimisha siku ya Takwimu Ofisi ya Mtakwimu Mkuu inajivunia hatua kubwa iliyopiga ya uboreshaji wa takwimu kutoka katika matumizi ya karatasi na pia kutumia ukusanyaji wa takwimu kwa njia ya teknolojia.
Aidha amesema maadhimisho ya Siku ya Takwimu duniani yanaandaliwa kwa lengo la kuielimisha jamii juu ya umuhimu na jukumu la kila mmoja wetu katika ukusanyaji uchambuzi na uwasilishaji wa Takwimu sahihi kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya nchi za Afrika.
Pia amesema Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali inawaomba wadau mbali mbali na jamii kwa ujumla kutoa mashirikiano ya dhati katika suala zima la utoaji wa taarifa sahihi ili kuwa na takwimu bora kwa mipango ya maendeleo ya nchi yetu.
Kwa upande wa washiriki wa sekta mbali mbali katika maadhimisho hayo wamesema licha ya maendeleo yaliyopatikana wanahitaji kupatiwa elimu ili kuondosha changamoto ndogo ndogo za utumiaji wa mitandao.
Siku ya Takwimu ya Afrika huadhimisha kila ifikapo tarehe 18 Novemba ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni uimarishaji wa mifumo ya Takwimu Kitaifa kwa uzalishaji wa taarifa na utoaji wa Takwimu ili kuwepo kwa amani na maendeleo endelevu Barani Afrika.
No comments:
Post a Comment