Habari za Punde

Tumbaku huathiri afya na ni kichochezi cha maradhi yasiyoambukiza

Na Khadija Khamis –Maelezo.13/11/2020

 

MATUMIZI  ya Tumbaku yanaathari katika afya ya binaadamu na husababisha vichocheo vya maradhi yasioambukiza ikiwemo magonjwa ya Saratani.

 

Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari huko katika ukumbi wa Jumuiya ya Maradhi Yasioambukiza Mpendae wilaya ya Mjini, Meneja wa maradhi yasioambukiza kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Bw. Omar Abdalla Ali amesema utumiaji wa tumbaku  unaathiri zaidi ubongo wa binaadamu na kupelekea Maradhi ya kiharusi.

 

Amesema pia Tumbaku inasababisha maradhi ya Shindikizo la damu, Saratani ya ngozi,maradhi ya mapafu kinywa kuganda uchafu kuharibu meno na fizi kuoza, pamoja na kuzaa watoto wafu,

 

Aidha amesema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean road ya Dar-es-saalam 2011 imeaonyesha kuwa asilimia 7.3 ya Wakaazi wa Zanzibar  wanatumia Tumbaku.

 

Amefahamisha kuwa baadhi ya vijana wanatumia Tumbaku kwa kuvuta,kunusa na kutafuna pamoja na kuvuta Sigara, Kuber na Pombe iliokithiri hali ambayo inapelekea kupata athari za shindikizo la damu,Presha na Saratani. 

 

Meneja Omar amesema baadhi ya Vijana huvuta Sigara zaidi ya sita kwa siku na  kutumia Pombe kali jambo ambalo linaleta athari kubwa ikiwemo ya maradhi yasioambukiza kwa Vijana

 

Aidha amesema tafiti zimeonyesha wanafunzi nao wamo katika uvutaji wa sigara, kati ya wanafunzi 100 wanafunzi 10 ni wavutaji sigara .

 

“wavutaji sigara wajitenge maeneo ya mbali na jamii sio kuvuta ovyo  katika maeneo ya  masoko vituoni huathiri jamii iliokuwepo karibu nae kwa huvuta moshi wa sigara “alisema Meneja huyo.

 

Alieleza kuwa tafiti zimeonyesha  waathirika zaidi ni wale wanaotoka majumbani na sehemu za kazi hasa wanawake ambao waume zao kuwa wavutaji sigara .

 

Akitoa wito kwa jamii Meneja huyo amewataka watumiaji wa sigara kufuata sheria zilizowekwa za afya ya mazingira 2012 kuvuta maeneo sahihi ambayo hayatasababisha athari kwa wengine.

 

Nae Meneja wa Jumuiya ya Maradhi yasioambukiza Zanzibar Bw Haji Khamis Fundi amefahamisha kuwa wanatarajia kutoa elimu kwa  wanaowahudumia waathirika wa maradhi yasioambukiza kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar.

 

Amesema utoaji wa elimu hiyo itawasaidia waathirika hao kuwapa huduma nzuri na kufanyiwa uchunguzi wa vipimo mara kwa mara ili kujuwa maendeleo ya afya zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.