Habari za Punde

Mhe Hemed apongeza kasi ya uwajibikaji ya viongozi wa majimbo kuondoa kero za wananchi

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Chumbuni hapo Uwanja wa Michezo wa Masumbani katika Mkutano wa hadhara wa shukrani baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Nd. Talib Ali Talib akitoa salamu katika Mkutano huo kama mwenyeji wa shughuli za Chama ndani ya Mkoa.

Mwakilishi wa Jimbo la Chumbuni Mheshimiwa Miraji Khamis Mussa {Kwaza akielezea Mikakati ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Jimbo hilo kwa Mwaka 2020 – 2025.

 Mbunge wa Jimbo la Chumbuni  Mh. Ussi Salum Pondeza {Amjadi}akiwapongeza Wana CCM na Wananchi wa Jimbo hilo kwa Imani yao ya kuwakabidhi Tena jukumu la kuwahudumia ndani ya Miaka Mitano ijayo.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mh. Hemed Suleiman Abdulla akisisitiza jambo wakati akiwapongeza Wananchi kwa kuendelea kuiunga Mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibay ya Awamu ya Nane

Mheshimiwa Hemed akimkabidhi Mmoja miongoni mwa Mabalozi wa Jimbo la Chumbuni waliokabidhiwa Vyarahani 120 kati ya 160 vilivyotolewa na Uongozi wa Jimbo la Chumbuni kutekeleza Ahadi uliyotoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mh. Hemed Suleiman Abdulla  amepongeza kasi kubwa ya ajabu ya Viongozi wa Majimbo katika muelekeo wao wa kuondoa kero zinazowakabili Wananchi katika maeneo yao.

Mheshimiwa Hemed Suleiman ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Chumbuni hapo Uwanja wa Michezo wa Masumbani katika Mkutano wa hadhara wa shukrani baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba Mwaka huu.

Mkutano huo umekwenda sambamba na mwanzo wa Utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ndani ya Jimbo la Chumbuni pamoja na utekelezaji wa Ahadi zilizotolewa na Viongozi wa Jimbo hilo wakati wa Kampeni za Uchguzi.

Alisema hilo ni jukumu kubwa lililobebwa na Viongozi hao likilenga kwenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020-2025.

Mheshimiwa Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Viongozi wa Majimbo mengine kuiga mfano wa Viongozi wa Jimbo la Chumbuni lililoanza safari ya Utekelezaji huo uliyoonyesha mwanzo mwema wa mafanikio katika ustawi wa Kijamii.

Aliwatahadharisha Wananchi watakaobahatika kupata nyenzo za kuendeleza miradi ya Ujasiri Amali kuhakikisha kwamba Vyarahani walivyokabidhiwa vinaendelea kuwahudumia na kuonya kwamba haitapendeza kutokea siku zana hizo zikakutwa sokoni.

Mheshimiwa Hemed aliwahakikishia Viongozi na Wananchi wa Jimbo la Chumbuni kwamba Serikali iko tayari kuzipokea changamoto za Wananchi hao ambazo haziko kwenye uwezo wao wa kuzitatua.

Akizungumzia suala ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane, Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwataka Wananchi kumvumilia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi akiendelea kupanga safu ya Uongozi.

Akimkariri Dr. Hussein kutokana na kauli zake za kupanga safu Mheshimiwa Hemed alisema zipo changamoto zilizokuwa zikikwaza utendaji wa Serikali ikiwemo kero ya rushwa, uzembe na ubadhirifu aliokusudia Rais wa Zanzibar kuuondosha.

Akielezea Mikakati ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Jimbo la Chumbuni Mwakilishi wa Jimbo hilo Mheshimiwa Miraji Khamis Mussa {Kwaza} alisema zipo changamoto kadhaa zitakazoshughulikiwa NA Uongozi Wa Jimbo hilo katika Kipindi cha Miaka Mitano ijayo.

Hata hivyo alisema zile changamoto kubwa ya nzito zinazohitaji nguvu za Serikali waliomba waongezewe nguvu akitolea mfano mtaro wa Maji machafu ambao msimu wa mvua kubwa za masika huleta athari zinazosababisha baadhi ya Wananchi wa eneo husika kuhama.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo  Mh. Ussi Salum Pondeza {Amjadi} alisema Mabalozi wa Chama cha Mapinduzi ndani ya Jimbo hilo wamefanya kazi kubwa ya kukipigania Chama hicho na matokeo yake Wananchi waliowengi wameamua kuipa ridhaa CCM kuendelea kuongoza Dola.

Alieleza katika mwanzo wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 hadi 2025 kasi yao inaanzia katika kuwapa nguvu Mabalozi katika ile dhana nzima ya kuthamini uzalendo wao na hatimae CCM inazidi kunawiri.

Mh. Pondeza kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo lake wamempongeza Dr. John Pombe Magufuli kwa Kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar pamoja na Wasaidizi wao wa karibu kitendo kilichoonyeshwa na Wananchi kuwaunga mkono katika safari yao ya kuwatumikia Watanzania.

Akitoa salamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Nd. Talib Ali Talib alisema kitendo cha Viongozi wa Jimbo la Chumbuni kuwapatia vifaa vya Ujasiri amali vya Charahani ni mwanzo mwema wa kuwajengea nguvu za kuweza kujitegemea.

Nd. Talib alisema Charahani ni moja ya nyenzo inayomuongoza Mwananchi mjasiri amali kuweza kujiendesha kimaisha bila ya kusubiri ajira za Serikali ambazo kadri maisha yanavyosonga mbele zimekuwa finyu katika Taasisi za Umma.

Katika Mkutano huo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM Mh. Hemed Suleiman Abdulla alikabidhi Vyarahani 162 vilivyotolewa na Viongozi wa Jimbo la Chumbuzi wakati wa Kampeni za Uchguzi walipoahidi kuwajengea mazingira bora Wananchi katika masuala ya Ujasiri amali.

Vyarahani hivyo vilikabidhiwa kwa Mabalozi 120, Umoja wa Akina Mama wakuhifadhisha Quran, Jumuiya ya Vyuo vya Quran, Wananchi wanaoishi katika Mazingira magumu pamoja na Umoja wa Vijana vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 59.7.

 


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.