Habari za Punde

Serikali kuanzisha Maonesho ya Sanaa za Ufundi Kitaifa

 

Mwakilishi wa Kikundi cha Wanawake wanaofanya Sanaa ya Uchoraji Safina Kipokota (kushoto) akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi,leo Desemba 04,2020, Jijini Dar es Salaam, katika kikao na wadau wa Sanaa za Ufundi  kujadili namna ya kuendeleza tasnia ya hiyo kufuatia tamko la Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kuendeleza Sanaa alipokuwa akifungua bunge.


Na.Anitha Jonas – WHUSM, Dar es Salaam. 05/12/2020

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi amesema kuanzia mwaka 2021 kutakuwa Maonesho ya Kitaifa ya Sanaa za Ufundi nchini.

Dkt. Abbasi ametoa kauli hiyo leo Desemba 03,  Jijini Dar es Salaam, katika mkutano na Wasanii wa Sanaa za Ufundi ikiwa ni mwendelezo wa vikao vyake vya kukutana na makundi mbalimbali ya wadau wa Sanaa kwa lengo la kujadili namna ya kukuza na kuendeleza sekta ya Sanaa kwa kuzingatia ahadi ya Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli katika hotuba yake wakati akifungua Bunge.

Akizungumza katika kikao hicho Dkt.Abbasi alisisitiza kuwa serikali imedhamiria kusaidia sekta  ya sanaa, kwa kukuza masoko na kujenga mazingira rafiki ya kuendeleza sanaa nchini.

"Viongozi wa Mashirikisho na vyama nendeni mkafanye utafiti wa Maonesho ya kazi za Sanaa za Ufundi Kimataifa na mnilete kalenda inayoonyesha matukio hayo,  na nchi inayoandaa maonesho hayo ili tuwasiliane na balozi zetu kuona namna tunaweza kuwasaidia, sisi pia kama wizara kila patakapo kuwa na matukio makubwa au mechi kubwa pale Uwanja wa Benjamin Mkapa  nitatoa eneo kwa wasanii wa Sanaa za Ufundi kuonyesha na kuuza kazi zao,"alisema Dkt.Abbasi.

Akizungumza katika kikao hicho Dkt.Abbasi alisisitiza  wasanii kutumia vyama vyao na Mashirikisho kutoa maoni ya mambo wanayokwamisha uendeshaji wa kazi zao ikiwemo utitiri wa kodi na tozo ambazo nikubwa zinazokwamisha shughuli hizo.

Naye Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa Taifa Godfrey Mngereza ahidi kupokea maoni yote ya wadau hao na kusema atayafanyia kazi ikiwemo kuandaa mpango wa kutoa mafunzo kwa wasanii wa Sanaa za Ufundi ya namna ya kufanya biashara katika mfumo wa kisasa kwa kuweka kipao mbele thamani ya kazi zao.

Halikadhalika nae Msanii wa Sanaa ya Uchoraji Hasmain Raza alitoa ombi kwa Serikali la kuangalia muundo wa majukumu kwa taasisi ya BASATA katika uendeshaji, kwa kuomba ianzishe Idara au Vitengo cha Muziki kwa kila sanaa wanayoisimamia, badala ya sasa hali ilivyo sasa vitu vyote kuendeshwa kwa pamoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.