Habari za Punde

Serikali Kusimamia Michezo Kikamilifu Ili Taifa Liweze Kushiriki Michuano ya Kimataifa - Dk. Mwinyi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wanamichezo na Wadau wa michezo Zanzibar wakati wa hafla ya Mchezo wa Fainali Kombe la Yamle yamle Cup Kati ya Mboriborini na Mbirimbirini mchezo uliofanyika Uwanja wa Amaan Timu ya Mboriborini imeshinda mchezo huo kwa bao 2-1. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itahakikisha inasimamia michezo kikamilifu ili Taifa liweze kushiriki katika michuano mbali mbali ya Kimataifa.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo katika fainali ya michuano ya soka ya ‘Yamle yamle Cup’ iliyofanyika katika Uwanja wa Amani Jijini hapa, ambapo klabu ya Mboriborini FC ilimenyana na timu ya Mbirimbini na hatimae timu ya Mboriborini FC kunyakuwa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kuigaragaza Mbirimbini kwa mabao 2- 1.

Aliwataka wadau kukaa pamoja na kuondoa vikwazo vyote vinavyokwaza maendeleo ya michezo nchini ikiwemo soka, hatua itakayoleta ufanisi katika michezo.

Akigusia kuhusiana na mchezo huo, Dk. Mwinyi alisema ameridhishwa na viwango vizuri vilivyoonyeshwa na wachezaji wa fainali hiyo, sambamba na kuwapongeza waandaaji wa michuano hiyo Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) akibainisha hatua hiyo  itakuza vipaji.

Alisema kuwa kutokana na kuridhishwa na viwango vya juu vilivyoonyeshwa na wachezaji hao katika kutandaza soka, Dk. Mwinyi alichagia shilingi Milioni kumi kwa ajili ya washiriki wa michuano hiyo.

Aidha, aliwashukuru mashabiki waliojitokeza kwa wingi uwanjani kushangilia mchezo huo na kubainisha hatua hiyo inatoa taswira ya mapenzi makubwa waliyonayo katika soka.

Katika mtanange huo ulioshuhudiwa na mamia ya wapenda soka kutoka Mikoa mitatu ya Unguja, hadi timu hizo zinakwenda mapumziko timu ya Mboriborini FC ilikuwa ikiongoza kwa goli moja lililofungwa na Ibrahim Abdalla katika dakika ya 37.

Aidha, kipindi cha pili kilianza kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu na hatimae timu ya Mbirimbini ikafanikiwa kupata goli la kusawazisha, kabla ya Ibrahim Abdalla wa Mboriborini FC kuzisalimia nyavu za wapinzani wao kwa mara ya pili mnamo dakika ya 89.

Kwa matokeo hayo , Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa mgeni rasmi wa michuano hiyo alikabidhi zawadi kwa washindi, ambapo Bingwa wa Michuano hiyo klabu ya Mboriborini iliondoka na Shilingi Milioni saba, Kikombe pamoja na Jezi, huku mshindi wa Pili timu ya Mbirimbini FC wakiondoka na shilingi Milioni nne, Jezi na Kikombe.

Aidha, mfungaji bora wa Michuano hiyo Ali Othman Mmanga kutoka timu ya New Juve aliondoka uwanjani na zawadi ya Pikipiki.

Mashirika na taasisi mbali zilijitokeza kudhamini michuano hiyo, ikiwemo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF), Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Yassin Professional, ZAT, Shirika la Bima, Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) pamoja na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.