Habari za Punde

Mahafali ya Kumi na Tatu ya Chuo Cha Utawala wa Umma Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akiyaongoza Maandamano ya Wahitimu wa Chuo cha Utawala wa Umma kwenye Mahafali ya 13 ya Chuo hicho akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi.
Uongozi wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar umetakiwa kusimamia ipasavyo Mitaala ya kufundishia katika muelekeo wa kuzalisha Wanafunzi mahiri watakaokijengea sifa Chuo hicho kiwe miongozi mwa Vyuo vyenye hadhi ya Kitaifa na Kimataifa katika kuwafinyanga Watumishi wa Umma.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dr. Husseina Ali Mwinyi alitoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla katika Mahafali ya 13 ya Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Dr. Ali Mohamed Shein wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} uliopo Tunguu Mkoa Kuainsi Unguja.

Jumla ya Wahitimu Mia 664 wa Chuo hicho cha Utawala wa Umma katika fani mbali mbali za Taaluma wamefanikiwa kutunukiwa Astashahada, Stashahada pamoja na Shahada katika zinazofundishwa kwenye Chuo hicho.

Dr. Hussein Ali Mwinyi alisema Chuo cha Utawala wa Umma ni Taasisi inayotegemewa na Serikali na hata Jumuiya za Kiraia katika kuwaandaa Wafanyakazi watakaoweza kuivusha Zanzibar  kutoka kwenye Uchumi wa Daraja la Tatu chini hadi Daraja la Tatu juu.

Alisema Taifa linashauku ya kuona Chuo hicho kinatoa Watumishi wa Umma walioshiba Nidhamu, Heshima, Uadilifu na Uaminifu utakaozaa sifa zitakazowashawishi Wananchi moja kwa moja kuiamini Serikali yao kutokana na Utumishi uliotukuka wa Watumishi hao.

“ Wananchi wenye kuiamini Serikali yao ndio wanaokuwa tayari kushirikiana kwa karibu na Serikali yao katika kushiriki mipango ya Maendeleo inayokwenda sambamba na ushiriki wa Wawekezaji wanaohitajika katika kuijenga Zanzibar Mpya”. Alisema Dr. Hussein.

Rais wa Zanzibar wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alielezea faraja yake kusikia kuwa Chuo hicho kupitia Wizara dhamana kiko katika hatua ya Kusaini Hati ya makubaliano na Chuo Kikuu cha Dodoma { UDOM} kwa nia ya kuwaendeleza Wakufunzi na Watumishi wengine katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu.

Alisema kwa vile makubaliano hayo yanatarajiwa kufikiwa katika hatua ya utekelezaji muda wowote maandalizi yatakapokamilika ni jambo jema na linastahiki kuungwa mkono  kutakokifanya chuo hicho kuwa bora zaidi Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  aliupongeza Uongozi wa Baraza la Chuo kwa usimamizi mzuri wa sera, sheria na utekelezaji wa miongozo tofauti inayotolewa  katika uendeshaji wa Chuo  unaotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kwa Taasisi hiyo iayojitegemea.

Halkadhalika aliwapongeza wahitimu hao kwa mafanikio waliyoyapata ya kufaulu vyema kwenye masomo yao akiwakumbusha kwamba bado Taifa linahitaji  Watumishi wenye  Utaalamu na ujuzi ili kwenda sambamba  na mabadiliko ya teknolojia na changamoto za maendeleo zinazotokea Duniani kiujumla.

Aliwatahadharisha Wahitimu hao kutobweteka na  Elimu waliyoipata na badala yake waongeze jitihada za kuitafuta zaidi Elimu itakayoleta manufaa kwa Jamii ambayo hatimae ndiyo watakayokwenda kuihudumia.

Katika kuendelea kuimarisha mazingira Bora ya chuo hicho Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Chuo hicho kuwa na muono wa kuwa na Majengo ya Kudumu ya Chuo hicho Kisiwani Pemba ili kuondokana na tabia ya kuazima Majengo.

Aliuhakikishia Uongozi wa Chuo hicho pamoja zile Taasisi jirani na sehemu hiyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itajipanga katika kuona Bara bara fupi inayoingia eneo hilo inajengwa kwa kiwango cha Lami ili kuwaondoshea Usumbufu Wanafunzi, Walimu na hata Wananchi wa eneo hilo.

Akisoma Risala ya Wanachuo cha Utawala wa Umma Mkurugenzi wa Chuo hicho Dr. Shaaban Mwinchumu Suleiman alisema Chuo cha Utawala wa Umma ni Taasisi inayojitegemea ikiwa na dhamira ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma Nchini.

Dr. Mwinchumu alisema IPA ikiendelea kuwafinya Wanafunzi zaidi ya elfu 1,235 kwa mwaka wa masomo wa 2020/2021 pamoja na mambo mengine imebeba dhima ya kufanya Utafiti unaosaidia kupata ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinazoibuka ndani ya Taasisi za Umma Nchini.

Alisema wakati Uongozi wa Chuo ukiendelea kujenga uwezo katika kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu imepanga kupeleka muongozo Serikali Kuu ili iongeze nguvu katika upatikanaji wa Fedha kwa ajili ya Usomeshaji wa Wakufunzi wa Chuo hicho katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na ile ya Uzamivu.

Akitoa salamu katika Mahafali hayo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma Bibi Fatma Said Ali alisema Wakufunzi Watano wa chuo hicho tayari wameshapelekwa kupata elimu Zaidi kwenye Vyuo mbali mbali ndani na Nje ya Nchi.

Bibi Fatma alisema hatua hiyo imezingatiwa katika azma ya kuwajengea uwezo wa kitaalum Wakufunzi hao ili kwenda sasmbamba na Malengo ya Chuo ya kukifanya kufikia hadi ya Kitaifa na Kimataifa.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kwenye Mahafali hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mh. Haroun Ali Suleiman alisema zile ndoto za Chuo cha Utawala wa Umma zilizotarajiwa wakati wa kuanzishwa kwake zimeanza kutoa matunda kwa kuwa na Wahitima wa Ngazi ya Shahada.

Waziri Haroun  alisema ndoto hizo zilizotokana na jitihada kubwa iliyochukuliwa na Uongozi wa Chuo hicho chini ya Mkurugenzi Mstaafu Bibi Amina Masheko na Mkurugenzi wa Sasa Dr. Shaaban Mwinchum Suleiman kwa jitihada zao za kuwafinyanga Wanafunzi na hatimae kufikia hadhi ya ngazi hiyo muhimu.

Katika kukijengea uwezo wa Taaluma chuo hicho pamoja na mazingira bora ya wanataaluma wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuandaa Programu Maalum ya kujenga Majengo yake ili kukabiliana na changamoto zinazokikabili chuo hicho hivi sasa.

Mheshimiwa  Haroun Ali Suleiman amempongeza na Kumshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla  kwa usimamizi wake wa kuona Chuo cha Utawala wa Umma kinatekeleza malengo yake ya kutoa Elimu Kisiwani Pemba wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba.

Katika hafla hiyo ya Mahafali ya 13 ya Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi alikabidhi zawadi mbali mbali kwa Wahitimu Bora waliofanya vizuri kwenye mafunzo yao.

Chuo cha Utawala wa Umma kimekuwa kikifundisha  fani mbali mbali tokea kilipoasisiwa kwake  karibu Miaka 13 sasa zikiwemo Biashara na Teknolojia ya Mawasiliano, Ununuzi na Ugavi, Mipango na Maendeleo pamoja na Usimamizi wa Rasilmali Watu.

Nyengine ni Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia,Utawala wa Serikali za Mitaa, Mahusiano ya Umma, Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka, Uhazili pamoja na Uongozi wa Elimu ya Utawala katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, na Shahada.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.