Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Akilhutubia na Kulifungua Kongamano la Pili la Amani Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati wa hafla ya Mkutano wa Kangombani la Pili la Amani Zanzibar lililoandaliwa na Friends of Zanzibar  katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibae Beach Resort Mazizini Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeundwakwa lengo la kuendeleza na kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.

Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Amani uliofanyika huko katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Mazizini nje kidogo mwa Jiji la Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa  Mkutano huo umefanyika wakati muafaka ambapo nchi imefanikiwa kufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 katika hali ya amani na ulivu mkubwa.

Alifahamisha kwamba suala la kuendeleza na kudumisha amani hapa Zanzibar limepewa kipaumbele katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na mipango ya maendeleo ya Kitaifa.

Akinukuu Katiba hiyo katika kifungu cha 9(2-b) kimeeleza kwamba “Usalama na hali nzuri kwa wananchi itakuwa ndiyo lengo kubwa la Serikali”.

Rais Dk. Mwinyi aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane itaendelea kufanya kila linalowezekana kwa ajili ya kuendeleza fikra za waasisi wa nchi hii na viongozi waliotangulia katika kudumisha umoja na mshikamano wa wananchi wa Zanzibar.

Aliongeza kuwa ni ukweli usio na shaka kwamba maendeleo hayawezi kupatikana katika nchi yoyote bila ya kuwepo amani na mshikamano.

Kwa msingi huo, Dk. Mwinyi aliwahimiza viongozi wa vyama na Serikali, viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali, vyombo vya habari, wazee na vijana katika jamii kushirikiana katika kudumisha misingi muhimu ya amani ili hali ya amani iliyopo hapa Zanzibar izidi na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania izidi kuimarika.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kushirikiana na nchi za jirani katika Bara la Afrika katika kulinda hali ya amani na utulivu.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kushikamana katika kuhubiri amani na utulivu katika nyumba za ibada, taasisi za Serikali na ndani ya jamii na familia huku akieleza haja kwa vyombo vya habari kuendelea kuwa makini ili kujiepusha kusambaza habari zinazoweza kuhatarisha amani.

“Sote tuwe tayari kushirikiana katika kurejesha amani pale ilipotoweka.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kutodharau mambo madogo madogo yanayoweza kuhatarisha amani, kwani amani inapotoweka ni tabu kuirejesha  na kujifunza kwa wale waliopata mitihani ya kuondolewa amani na utulivu.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi zake kwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti pamoja na Taasisi ya Marafiki wa Zanzibar (Friends of Zanzibar) kwa kuandaa mkutano huo.

Dk. Mwinyi aliwakaribisha wageni wote waliokuja katika mkutano huo na kuwahimiza kutembelea vivutio vya utalii ili wajifunze historia na utamaduni wa watu wa Zanzibar kwani yamo mambo mengi ya kujifunza kuhusu amani katika historia na utamaduni wa Kizanzibari.

Aliwataka washiriki wa mkutano huo kutoa michango yao na uzoefu walionao katika kulinda amani kwa kutegemea uzoefu na taaluma zao na kueleza imani yake kwamba maazimio yatayopitishwa katika mkutano huo yatakuwa na mchango mkubwa katika juhudi za kulinda na kudumisha hali ya amani.

Nae Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitoa salamu zake katika mkutano huo alisema kuwa suala la amani si suala la hiari kwani bila ya amani hakuna maendeleo na pia, amani ni msingi wakila kitu.

Maalim Seif alieleza kwamba maridhiano yanahitaji kulelewa ili vizazi vijavyo viweze kuja kurithi.

Makamo wa Pili na yeye kwa upande wake alitoa pongezi kwa waandaaji wote wa Mkutano huo na kusisitiza kwamba amani ni msingi wa maendeleo huku akieleza haja ya kuengezwa washiriki katika mkutano ujao kutokana na umuhimu wa mkutano huo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alizipongeza juhudi za Dk. Mwinyi katika kuitunza amani iliyopo huku akiwataka wananchi waendelee kuunga mkono juhudi hizo ili amani izidi kudumu.

Mapema Mabalozi wa nchi za Jumuiya ya Ulaya zikiwemo Ujerumani, Norway na Switzerland kwa nyakati tofauti walipongeza hatua za makusudi zilizochukuliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi pamoja na Maalim Seif Sharif Hamad za kuwa na mashirikiano ya pamoja katika kuidumisha amani na hatimae kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mabalozi hao walieleza matarajio yao makubwa kwa Zanzibar na kusisitiza kwamba wataendelea kuinga mkono katika kuhakikisha amani iliyopo inadumishwa sambamba na kuendeleza kushirikiana na Zanzibar katika masuala mbali mbali ya maendeleo.

Mapema wawakilishi wa Taasisi ya Marafiki wa Zanzibar (Friends of Zanzibar) kutoka Msumbiji, Malawi, Congo DRC, Rwanda, Burundi, Kenya na Tanzania Bara kwa nyakati tofauti walitoa salamu zao ambazo ziliwapongeza viongozi na wananchi wa Zanzibar kwa kuimarisha amani, umoja na mshikamano.

Viongozi hao walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuonesha uongozi bora na uliotukuka hatua ambayo imeweza kudumisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa huku wakimpongeza Maalim Seif Sharif Hamad kwa kukubali kuwa miongoni wa viongozi wa Serikali hiyo.

Walieleza matumaini yao makubwa kwa Zanzibar ambapo waliitabiri kuwa ni sehemu itakayopata maendeleo makubwa na ya haraka kutokana na kuwepo  kwa amani, umoja na mshikamano huku na wao wakiahidi kuendelea kuiunga mkono.

Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih aliwakaribisha wageno wote kutoka nji ya Zanzibar katika mkutano huo huku akieleza umuhimu wa amani.

Mkutano huo wa Amani umeshawahi kufanyika hapa Zanzibar na huo wa leo utakuwa ni wa pili ambapo ule wa mwanzo ulifanyika hapa Zanzibar mnamo mwaka 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Viongozi mbali mbali walihudhuria kutoka ndani na nje ya Zanzibar katika mkutano huo wa siku mbili  ambapo moja kati ya mada zitakazowasilishwa ni “Mambo tunayopaswa kujifunza baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauaji yaliyotokea nchini Rwanda”.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.