Habari za Punde

Taasisi za kiraia lashiriki zoezi la kupanda Mikoko Kinazini

 Na Ali Issa Maelezo 23/1/2021

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Mifugo na Maliasili zisizo rejesheka Dkt.Soud Nahoda Hassan amesema Taasisi za kiraia nchini zinawajibu mkubwa wa kuweka usafi na kuhifadhi mazingira.

Hayo ameyasema leo huko Kinazini katika bahari ya Mpiga duri -Kizingo wakati wa zoezi la upandaji mikoko lililoandaliwa na Taasisi za kiraia hapa Zanzibar.

Amesema mazingira ya Zanzibar yatalindwa na wazanzibari wenyewe hivyo jamii iwe na mwamko wa kuhifadhi na kulinda mazingira ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi

Amefahamisha kuwa mazingira ya bahari ya Kinazni Mpigaduri na Kizingo yameharibiwa kwa kuchimbwa mchanga kukata mikoko na kutupa taka ovyo bila kuzingatia mustakabali mwema wa baadae.

 “Hali hii ni mbaya kwani inapelekea kutokea mabadiliko ya tabianchi wananchi waache mara moja kufanya vitendo hivyo vibaya vikomeshwe mazingira yalindwe watu wasifanye wanavyotaka na iwapo atatokea mtu kuharibu kwa makusudi sheria zimuandame”, alieleza Waziri huyo.

Ameeleza kuwa taasisi hizo kupanda mikoko katika eneo hilo ni jambo jema sana na mfano mkubwa wa kuigwa na wananchi wengine ili kuepuka uharibifu wa mazingira nchini.

Dkt. Soud amezishukuru taasisi hizo kwa mchango mkubwa wa kazi wanazozifanya  kwani Serikali inathamini juhudi hizo na kuwataka kuendelea kufanya bidii ya kupanda miti ya mikoko katika maeneo yaliyoharika kwa lengo la kulinda mazingira ya bahari.

Nae Mwenyekiti wa Tasisi ya kupambana na Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar ZACCA Mahafudh Shaban Haji amesema wanakusudia kupanda mikoko elfu 50 na miti mengine elfu 20 kwa lengo la kupunguza mabadiliko ya tabia nchi hapa visiwani.

Zoezi hilo la upandaji mikoko limeshirikisha  Taasisi mbalimbali za Kiraia ikiwemo Taasisi ya Usafi ya Mwanakwerekwe (USAFI HUB), Taasisi ya Kupambana na Madiliko ya Tabianchi(ZACCA), Taasisi ya Habari na Vijana (MYCN) na Taasisi ya Kuhifadhi Mazingira Jozani ( JECA) ambapo jumla ya mbegu 2000 za mikoko zilipandwa eneo la Bahari ya Kinazini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.