Habari za Punde

Dk. Mwinyi Ameyataja Maeneo Kumi Kwa Waandishi wa Habari Pamoja na Kuwepo kwa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa Mafanikio Makubwa Yamepatikana

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Wahariri na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali, yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 9-2-2021. 
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  amesema kuwa mafanikio yake makubwa aliyoyapata katika Serikali yake ya Awamu ya Nane tokea aingie madarakani ni  kuleta umoja wa wananchi na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Waandishi na Wahariri wa Habari wa vyombo mbali mbali vya habari vya nje na ndani ya Zanzibar ikiwa ni siku mia moja katika uongozi wake wa Serikali ya Awamu ya Nane, hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.

Akieleza kwa wananchi kupitia vyombo vya habari wakati akizungumza na waandishi hao, Rais Dk. Mwinyi aliyataja maeneo kumi ambayo ameyaeleza kwa ufupi ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa maridhiano na umoja wa Kitaifa ambapo mafanikio makubwa yamepatikana katika maeneo hayo.

Alisema kuwa wakati anaingia madarakani alitambua fika kwamba hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila ya kuwepo amani na umoja mambo ambayo aliwashukuru wananchi wa Zanzibar kuendelea na hilo pamoja na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuilinda na kuiendeleza .

Alisisitiza kwamba  pia, aliona umuhimu wa kuwaunganisha wananchi kwa azma ya kutafuta maridhiano na kuwa na umoja wa kitaifa na hatimae kukubaliana na chama cha ACT Wazalendo kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa aliona umuhimu wa kuwaunganisha wananchi na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na ndipo walipoanza mazungumzo hayo yaliyozaa maridhiano huku akisema kuwa bila ya kuwepo Serikali ya Umoja wa Kitaifa maendeleo yangekawia kwani mazingira yasingekuwa rafiki.

Alisema kuwa hatua hiyo imepelekea kukidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar, kuwepo kwa umoja wa wananchi na hivi sasa wananchi wamekuwa wakizungumzia maendeleo na wameacha kulumbana kisiasa pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kisiasa ili kuleta mazingira mazuri ya kiuchumi

Alisema kuwa tayari ameshaunda Serikali na amepunguza ukubwa wa serikali ili kupunguza gharama za utawala na badala yake fedha nyingi zielekezwe kwenye miundombinu na huduma za jamii sambamba na kuzingatia mambo yote katika uteuzi.  

Kwa upande wa uchumi, alisema kuwa uchumi wa buluu ndio aliounadi wakati wa kampeni na tokea alipoingia madarakani ameshafanya mazungumzo na wawekezaji mbali mbali ambao tayari mikataba ya awali imeshatiwa saini ikiwemo ujenzi wa bandari ya Mangapwani/Bumbwini ambayo itaifanya Mangapwani iwe mji wa Bandari.

Katika hilo alisema kuwa tayari Oman imeonesha nia ya mashirikiano huku akieleza jinsi ya saini iliyotiwa hivi karibuni ya ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri ambayo itaekezwa kwa Dola za Kimarekani  Bilioni 6.3 ambao ni mradi mkubwa sana huku bandari ya Malindi kugeuzwa kuwa bandari ya utalii.

Aidha, alisema hatua ya kuongeza uzalishaji wa umeme ambapo tayari Serikali imeshatiliana saini na Kampuni kutoka Marekani yenye kutaka kuzalisha umeme wa megawati  350 kwa awamu ili kuchochea uchumi wa Zanzibar na limepewa kipaumbele.

Alisema kuwa hivi karibuni Serikali itakopa fedha kutoka Benki ya dunia kwa ajili ya kujenga miundombinu ya umeme wa jua pamoja na kuimarisha miundombinu itakayowezesha kupatikana kwa kv 135 ambayo itaweza kubeba umeme mkubwa.

Katika suala zima la miundombinu, alieleza kuwa kwa kiwango kikubwa bandari ya Malindi imeimarika na kwenye mapato imeweza kuingiza fedha nyingi ambapo kwa muda wa mwaka mmoja uliopita ilikuwa ikiingiza faida ya TZS Bilioni 4.3 lakini kwa mwezi Disemba peke yake imeingiza TZS Bilioni  2.1 hatua ambayo imeonesha ufanisi mkubwa.

Aidha, alieleza hatua za kuimarisha huduma za uwanja wa ndege wa Zanzibar sambamba na juhudi zinazochukuliwa katika kuhakikisha huduma za kiwanja hicho zinaimarika.

Alieleza hatua zilizochukulwia za awali kwamba hata wawekezaji kutoka nje wamevutika na wanataka kuja kuekeza Zanzibar sambamba na wale wawekezaji wa wazalendo wa Zanzibar.

Kwa upande wa wafanyabiashra wadogo wadogo alieleza hatua alizozichukua za kujengwa kwa maeneo maalum ambapo hivi karibu soko lao la Kibandamaiti litafunguliwa.

Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua zinazotaka kuchukuliwa na serikali katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuanzisha kwa Bima ya Afya huku sekta ya elimu nayo ikiimarishwa.

Alisema kuwa suala la uwajibikaji limekuwa likipewa kipaumbe na hivi sasa na kazi zimeanza kufanyika na kutoa mfano kwa Mashirika ya ZECO, Mamlaka ya ZAWA, Wakala wa Barabara nao wamekuwa wakitekeleza vyema kazi zao huku juhudi za makusudi zikiendelea kuchukuliwa katika kutatua migogoro ya ardhi.

Alisema suala zima la utawala bora na kusema kwamba Serikali haitaki masihara katika masuala ya rushwa na kusema kwamba amechukua hatua kila kasoro na ataendelea kufanya hivyo na hiyo sio nguvu za soda na hatua zitaendele kuchukuliwa.

Akieleza kuhusu ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa katika kipindi hichi cha siku 100, mapato ya kodi yameongezeka sana na kusema kuwa bado hajaridhika na ukusanyaji huo huku akieleza kwamba Serikali inajipanga kufunga mifumo ya kielektoniki katika maeneo yote hatua ambayo itaongeza pato la serikali

Kwa upandewa suala la udhalilishaji alisema kuwa vituo vya uchunguzi vifanye kaziya ziada na kwa upande wa Mkurugenzi wa Mashtaka kesi ziende kwa haraka ambapo pia tayari Mahakama maalum ya udhalilishaji imeshaanzishwa na kusisitiza kwamba hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Wawakilishi ameagiza Serikali ipeleke maelekezo ili kesi za udhalilishaji zisiwe na dhamana.

Akieleza juu ya ushirikiano na sekta binafsi, hatua kubwa zimechukuliwa na sekta nyingi ziko tayari kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nane kutokana na mwitikio mkubwa sana zikiwemo Benki na kuahidi kuimarisha mazingira ya biashara hapa Zanzibar.

Alisema kuwa siku 100 za kwanza za Serikali  ya Awamu ya Nane zimethibitishwa kwamba serikali iko makini na imekusudi kutekeleza ahadi ilizozitoa kwa wananchi     imezingatia misingi iliyowekwa na Serikali zilizopita, na kutoa shukurani kwa wasaidizi wake wakuu kwa kumsaidi majukumu yake na kuwashukuru viongozi wa umma kwa kutekeleza vyema majukumu yao.

Akijibu masuala mbali mbali ya waandishi wa Habari Rais, Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali imejipanga kujenga mifumo ya kielektroniki hatua za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha suala la ajira linaondokana na changamoto iliyopo.

Katika suala zima la kuwajibikaji, suala zima la ugawaji wa viwanja na kusema kwamba ni vyema kuwepo kwa utaratibu mzuri wa kupewa wananchi viwanja bila ya upendeleo.

Aidha,a lisema haja kwa viongozi aliowateua wakiwemo Mawaziri kuhakikisha wanakutaka na waandishi wa habari na kusisitiza kwamba hilo atalisimamia.

Nao Waandishi na Wahariri walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake kubwa alizozifanya na kazi kubwa aliyoifanya ndani ya siku 100 huku wakimpongeza kwa hatua yake hiyo ya kuzungumza na nao jambo ambalo waliomba kuendelezwa kwa kila pale atakapopata wasaa.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.