Habari za Punde

Ripoti ya Uchunguzi yaibua mazito chanzo cha kuporomoka sehemu ya jengo la Beit el Ajaib

Waziri wa Utalii na mambo ya Kale Mhe,Lalila Mohamed Mussa akionesha Ripoti ya Kamati Maalum ya kuchunguza Chanzo cha kuporomoka sehemu ya Jengo la Baitil Ajaibu kwa Waandishi wa Habari hawapo pichani wakati akiwasilisha Ripoti hio katika ukumbi wa Wizara hio Kikwajuni Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria katika Mkutano wa  Waziri wa Utalii na mambo ya Kale Mhe,Lalila Mohamed Mussa kuhusiana na kuwasilisha  Ripoti ya Kamati Maalum ya kuchunguza Chanzo cha kuporomoka sehemu ya Jengo la Baitil Ajaibu kwa Waandishi hao  katika ukumbi wa Wizara hio Kikwajuni Zanzibar.

Waziri wa Utalii na mambo ya Kale Mhe,Lalila Mohamed Mussa akiwasilisha mbele ya Vyombo vya Habari  Ripoti ya Kamati Maalum ya kuchunguza Chanzo cha kuporomoka sehemu ya Jengo la Baitil katika ukumbi wa Wizara hio Kikwajuni Zanzibar.

                   Picha na Yussuf Simai - Maelezo Zanzibar.

Na Rahma Khamis/Maelezo Zanzibar   4/2/2021

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Muhamed Mussa amesema Wizara itamchukulia hatua za kisheria mkandarasi aliyejenga jumba la Bet al Ajab na kusababisha kuporomoka kwa jengo hilo,  ikiwemo kulipia fidia ya uharibifu wa mali.

 

Alisema mbali ya fidia hiyo, lakini pia kupitia Sheria ya Madai Wizara itahakikisha Mkandarasi huyo analipia fidia ya afya na uhai wa watu walioathirika katika tukio hilo.

 

Lela alitoa kauli hiyo ukumbi mdogo uliopo Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni Mjini Unguja, wakati alipokuwa akitoa ripoti ya kamati ya uchunguzi ya kuporomoka kwa jengo la Bet al Ajab ambalo liliporomoka Desember 25, 2020.

 

Alisema mbali ya hatua hiyo lakini Pia Wizara itawawajibisha watendaji wakuu waliokuwa Wizara ya Habari,Utalii na Mambo ya kale pamoja na Mamlaka ya Hifadhi na undelezaji wa Mji Mkongwe kwa mujibu wa Sheria za Utumishi wa Umma, kuwawajibisha Wizara ya Ardhi ,Nyumba Maji na Nishati kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma No 2 ya mwaka 2011 pamoja na sheria.

 

Alisema Wizara pia inashauri Mamlaka ya uteuzi kuivunja Bodi na kuunda Bodi mpya, kufanyiwa marekebisho ya sheria ya Mamlaka ya uhifadhi ya uendelezaji wa mji Mkongwe hasa katika maeneo ya sifa ya wajumbe wa Bodi.

 

“Lakini pia tutachukua hatua za kuvunja timu ya usimamizi ya mradi na kuajiri mshauri elekezi mwenye sifa na weledi wa kusimamia mradi kama huo”alisema Lela.

 

Alisema mbali ya hatua hizo lakini pia Mshauri elekezi wa mradi huo naye atachukuliwa hatua za kimkataba mshauri huyo, pamoja kuwachukulia hatua za kisheria wahusika kupitia sheria ya uhujumu wa Uchumi (ZAECA) pamoja na kuwataka wahusika warejeshe fedha zote kwa umoja wao.

 

Hatua hiyo imekujaa baada ya kubainika kasoro mbali mbali katika mradi huo wa ujenzi wa wa jengo la Bet al Ajab ambalo limeporoka mwishoni mwa mwaka uliopita.

 

Waziri Lela alitaja baadhi ya kasoro hizo ni pamoja na Mshauri elekezi kujipatia fedha kiasi cha sh 58,700,000 pamoja na mkandarasi kushindwa kufanya kazi zao kwa mujibu wa mkataba waliopewa, kulipwa kiasi cha sh 86,800,250 kinyume na taratibu za kisheria.

 

Alisema kasoro nyengine Wizara kushindwa kusimamia timu ya usimamizi wa Mradi katika utekelezaji wa mkataba, Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi na uendelezaji wa Mji Mkongwe kushindwa kusimamia katika utekelezaji wa ujenzi huo.

 

Alisema kasoro nyengine ni kubainika kwamba kuwasilisha na kuthibitisha Bima yenye utata juu ya kulipia fidia za hasara iliojitokeza, pamoja na kushindwa kutekeleza majukumu ya mkataba kwa mujibu wa masharti ya mkataba.

 

Hata hivyo Waziri Lela alisema mradi wa jengo hilo ilianza November 26, 2019 na kutarajiwa kukamilika Februar 26, 2021, ambapo ujenzi huo ulikisiwa kutumia Dola 5,931,770.70 zilizofadhiliwa na Serikali ya Oman, ambapo mkandarasi alihusika na mradi huo ni Construzioni General Gilardi – GGG kutoka Itali chini ya usimamizi Mamlaka ya Hifadhi na uendelezaji wa Mji Mkongwe.

 

Alisema hadi wakati huu Mkandarasi ameshalipwa Dola 621,389.07 kutoka fedha za mradi huo ambazo ni Dola 5,931,770.70, ambapo malipo yote hayo yamelipwa na Serikali ya Oman kwenda kwa Mkandarasi moja kwa moja, baada ya Serikali ya Zanzibar kupitia iliokuwa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya kale kuthibitisha uhalali wa malipo hayo.

 

Alisema baaada ya kuanguka kwa jengo hilo Serikali iliunda kamati ya kufanya uchunguzi ili kujua sababu za msingi zilizopelekea jengo hilo kuanguka, ambapo kamati hiyo iligundua kasoro hizo.

 

“Hadi mradi wa jengo hilo linaanguka umeshatumia zaidi ya asilimia 80 ya muda uliopangwa katika mkataba lakini kazi iliofanywa haikufikia hata asilimia 10”alisema Lela.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.