Na Mwandishi wetu- Unguja
Wananchi Visiwani Zanzibar wameaswa ktumia hati miliki
za kumiliki ardhi kujiletea maendeleo
ili kuendana na falsafa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)
inayolenga kujenga uchumi wa buluu
unaowanufaisha wananchi wote.
Hayo yamesemwa na
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na
Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Bi Immaculata Senje wakati wa hafla
ya kukabidhi hati miliki za kumiliki ardhi zipatazo 50 kwa wananchi wa Welezo wilaya ya Magharibi A,
Unguja leo Februari 9, 2021 baada ya urasimishaji ardhi.
“ Hati miliki za
ardhi mlizopata ni mtaji hivyo zitumieni katika kujiendeleza kwa kuanzisha
shughuli za uzalishaji kupitia mikopo kutoka katika taasisi za fedha kama
mabenki ambayo yemeonesha dhahiri kuwa yako tayari kuwakopesha kwa kutumia hati
hizi”, alisisitiza Bi. Senje
Akifafanua amesema
kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibari (SMZ) ni kuona wananchi
wananufaika na rasilimali zilizopo ikiwemo ardhi hivyo kila mwananchi ana
wajibu wa kuhakikisha anatumia fursa hiyo ya urasimishaji ardhi katika
kujiletea maendeleo.
Mratibu wa MKURABITA
Dkt. Seraphia Mgembe amesema kuwa
wananchi waliopata hati hizo wanapaswa kuwa chachu kwa wale ambao bado hawajarasimisha maeneo
yao kwa kutumia hati hizo kupata mitaji katika taasisi za fedha.
Aliongeza kuwa katika
maeneo mengi wananchi waliofikiwa na
mpango huo wametumia hati zao kukopa na kukuza mitaji yao hali iliyowawezesha
kuchangia katika kujenga uchumi na kuzalisha ajira.
“ Kila Mwananchi hapa
Zanzibar ana jukumu la kuunga mkono juhudi za Rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ) Dkt. Hussein Ali Mwinyi kupitia hati hizi na kushiriki
kikamilifu katika kujiletea ukombozi wa kiuchumi kama inavyosisitiza Serikali”,
alieleza Dkt. Mghembe.
Naye Afisa kutoka
Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Bw. Ali Alhaj Masoud amesema kuwa Benki hiyo
iko tayari kuwakopesha wananchi kwa kutumia hati za kumiliki ardhi zilizotolewa
na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
MKURABITA kwa kushirikiana na wizara za kisekta za
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikiwemo Wizara ya ardhi na Maendeleo ya
Makaazi imewezesha kutolewa kwa hati za kumiliki ardhi kwa wakaazi wa Pemba na Unguja tangu kuanza
kwa urasimishaji hadi sasa.
No comments:
Post a Comment