Habari za Punde

Uongozi wa Manispaa Mjini Watakiwa Kuhakikisha Wanapatiwa Nafasi Walengwa wa Soko Hilo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wafanyabiashara wa Soko la Kijanwani wakati wa ziara yake kutembelea eneo la ujenzi wa Soko la Muda Kibandamaiti, akiwa katika ziara yake.
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka Uongozi wa Manispaa Mjini kuhakikisha watu wanaopatiwa nafasi ya kufanya biashara katika soko la Kibandamaiti ni wale waliolengwa pekee, ili kuepusha vurugu hapo baadae.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika hafla ya kupokea soko la muda liliopo Kibandamaiti Jijini  hapa,lilojengwa na Vikosi vya Ulinzi na  Usalama kwa gharama ya shilingi Milioni Miasita.

Amesema wafanyabiashara wanaopaswa kupewa nafasi katika soko hilo ni wale waliokuwa wakifanya biashara katika eneo la Kijangwani pamoja na maeneo mengine yasio rasmi, hivyo akasisitiza haja ya kuwepo utaratibu mzuri katika ugavi wa nafasi za biashara.

Aliwataka wasimamizi wa soko hilo kusimamia vyema mchakato wa wafanyabaishara hao ili kuepusha vurugu.

Aidha, aliagiza soko hilo kuanza shughuli za kibiashara ndani ya kipindi cha wiki mbili, badala ya kusubiri mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Rais Dk. Mwinyi, ameviagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuweka ulinzi wa kutosha sokoni hapo, sambamba na Wizara ya Maji na Nishati kufikisha umeme eneo hilo ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao hadi nyakati za usiku pamoja na Manispaa kuweka vitofali katika maeneo ya wazi ili kuepuka uchafu katika kipindi cha mvua.

Alisema amefurahishwa kupatikana soko hilo la muda litakalotoa fursa kwa wafanyabiashara hususan wale waliokuwa Kijangwani kufanya shughuli zao na hivyo akautaka uongozi wa Manispaa hiyo kuhakikisha maeneo hayo hayadhibitiwi na watu.

Aidha, alisema Serikali iko tayari kufanyaka kazi na sekta binafsi , hivyo akabainisha umuhimu wa kushirikiana na Benki ya NMB yenye  dhamira ya kufanikisha ujenzi wa  soko kubwa la kisasa.

Rais Dk. Mwinyi aliwataka wafanyabiashara kuhamishia shughuli zao katika soko hilo, akibainisha kuwa ni eneo zuri kibiashara na lisilo na tatizo la wateja, kwa kuzingatia kuwa liko karibu na baarabara kuu.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alisema vitambulisho maalum vinaandaliwa kwa ajili ya wafanyabiashara wa soko hilo ili waweze kulipa kodi iliyopangwa na kueleza kuwa  hakutakuwa na tozo nyengine yoyote kwa ajili yao.

Alisema mipango ya Serikali ni kujenga masoko ya kisasa pamoja na vituo vya mabasi ili kwenda na wakati.

Nae, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana Mustafa alisema pamoja na mambo mengine, ujenzi wa soko hilo utaleta manufaa makubwa kwa Taifa na wnanachi kutokana na ukusanyaji wa Kodi  pamoja na upatikanaji wa ajira.

Alisema katika kuliimarisha eneo la soko hilo, miongoni mwa malengo yaliopo ni kujenga ukuta ili kuwawezesha wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao bila usumbufu na kuingiliwa na shughuli za michezo katika viwanja vya mpira, sambamba na uvamizi wa wafanyabiashara pembeni mwa soko hilo.

Nao, baadhi ya Wananachi waliopata fursa ya kuchangia , walimuomba Rais Dk. Mwinyi kuwapatia nafasi tano vijana waliokuwa wamejiajiri kwa kazi ya ulinzi wa magari katika eneo hilo kabla ya ujenzi kufanyika.

Aidha, waliomba kuharakishwa matengenezo yaliobaki katika soko hilo ili waweze kulitumia mapema zaidi, kwa kigezo kuwa wamekuwa wakifanya shughuli zao katika mazingira magumu katika maeneo yaliokosa wateja.

Ujenzi wa Soko la Muda Kibandamaiti ni utekelezaji wa agizo la Rais alilolitoa Novemba 18, 2020 wakati alipofanya ziara ya kuwatembelea wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao eneo la Kijangwani waliotakiwa kuhama eneo hilo kupisha shughuli nyengine za maendeleo.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.