Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Aendelea na Ziara Yake Kisiwani Pemba.

 

Makamu Wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman na ujumbe wake akiukaguwa Mradi Mkubwa wa Umwagiliaji iliopo Dodo Jimbo la Chambani ambao uko katika hatua ya ujenzi kwa asilimia 20%.
Makamu wa Pili wa Raiswa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akisikiliza Taarifa za kiufundi za baadhi ya Vifaa vya huduma za Hospitali ya Abdulla Mzee visivyofanya kazi na kuagiza hitilafu hiyo irekebishwe ndani ya wiki moja na kurejea kama kawaida.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwatembelea Wajasiriamali wanaojishughulisha na Kilimo cha Mwani katika Bahari ya Chokocho Wilaya ya Mkoani  kuona maendeleo na changamoto zinazowakabilio kwenye Miradi yao.

                                          Picha na – OMPR – ZNZ.    

Na.Othman Khamis OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amewahakikishia Wananchi na Wakulima waliomo kwenye miradi mikubwa inayoanzishwa kwamba Serikali Kuu iko makini kulipa fidia ya mali zao ili kuona miradi hiyo inaleta faida kwao na Serikali yenyewe.

Akizungumza na Wananchi na Wakulima wa Kijiji cha Dodo Jimbo la Chambani waliyoonyesha hofu ya malipo ya fidia ya mali zao baada ya kuutembelea mradi mkubwa wa Kilimo cha Umwagiliaji Mh. Hemed alisema Mtathmini Mkuu wa Serikali ameanza uchambuzi wa Kazi hiyo ili kila Mwananchi mwenye haki aweze kulipwa fidia yake.

Hata hivyo wakati akiwaomba Wananchi wa Dodo wasisite kutoa Taarifa pale wanapobaini changamoto zinazojichomoza kwenye Mradi huo aliwatahadharisha wazi kwamba Serikali kamwe haitakuwa tayari kumlipa fidia Mtu asiyehusika kwa kutumia ujanja utakaobainika.

Mheshimikwa Hemed aliwaeleza Wananchi hao kwamba Serikali imekuwa na nia safi ya kustawisha maisha ya Wananchi wake ndipo inapofikia maamuzi ya kuanzisha Miradi mikubwa kama hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi wa Wizara ya Kilimo kupitia Wahandisi wake kuharakisha utekelezaji wa mradi huo wa Umwagiliaji uliokusudiwa kuanza mapema mwaka 2019.

Halkadhalika Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwashauri wahandisi wa mradi huo kuwapatia fursa za ajira Vijana wa Vijiji vinavyouzunguuka Mradi huo kwa zile kasi zisizohitaji Taaluma kubwa.

Akizungumzia ubovu wa madarasa uliopo Skuli ya Mtambile baada ya kukagua Kituo cha ubunifu wa Sayansi. Mheshimiwa Hemed alisema kila Kiongozi anapaswa kuwa mbunifu katika kutanzua kero zinazowasumbua Wananchi anaowaongoza badala ya kuisubiri Serikali.

Hata hivyo katika kukabiliana na tatizo hilo linalosababishwa na athari za Kimazingira Wazawa wa eneo hilo wana dhima ya kuchangia utatuzi wa changamoto za skuli hiyo hata kama watakuwa wakiishi nje ya Tanzania.

Alisema Wanafunzi na Watoto wa maeneo hayo kwa vile tayari wameshaonyesha muelekeo bora wa Kitaaluma hasa katika Fani ya Sayansi inayobeba mambo mengi Kitaalamu lazima wajengewe mazingira mazuri ya kupata Elimu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza  Wanafunzi wa Kituo hicho cha Ubunifu wa Sayansi wa Skuli ya Mtambile kwa umahiri wao wa kujifunza, pongezi zilizokwenda sambamba na Halmashauri ya Wilaya ya Mkoani iliyojitolea kuwajengea Kivuko Wananchi wa Bodoa Jundamiti ambao Watoto wao walikuwa wakisumbuka kuvuka kwenye eneo lenye maji mengi yanayopita kwa kasi katika bonde la eneo hilo.

Akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Chokocho wanaojishughulisha na Kilimo cha Mwani baada ya kupokea changamoto zao Mh. Hemed alisema Wakulima wa Mwani lazima waendelee kupata kipato sahihi kulingana na nguvu wanayotumia wakati wa kuendeleza kilimo hicho.

Alitoa rai kwamba Kampuni isiyochangia vifaa pamoja na mafunzo kwa ajili ya utayarishaji wa ukulimwa wa Mwani inastahiki kupigwa marufuku ya kutonunua Mwani kutoka moja kwa moja kwa Wakulima.

Mheshimiwa Hemed alieleza kwamba Biashara yoyote inahitaji ushindani jambo ambalo Serikali Kuu kupitia Wizara  husika itaendelea kujitahidi kulinda maslahi ya Wananchi wake hasa Wakulima kwa kuelewa fika ugumu wa mazingira ya masoko kutokana na kile wanachokizalisha.

Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Buluu Zanzibar Mheshimiwa Masoud alisema Serikali kupitia Wizara anayoiongoza wanaendelea kutafuta Wawekezaji ili kuongeza ushindani wa soko la Mwani juhudi iliyoanza kuleta matumaini kwa kujitokeza Muwekezji kutoka Nchini Jamuhuri ya Watu wa China.

Mheshimiwa Masoud alieleza kwamba jitihada za Wakulima ni vyema zikaongezwa kwa kuimarisha zao la Mwani wa kabila la Cotonee lenye soko kubwa Kimataifa.

Mapema akitoa Taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za Serikali za Wilaya ya Mkoani ndani ya Mwezi Julai 2020 hadi Machi 2021, Mkuu wa Wilaya hiyo Ndu. Issa Juma Issa alisema huduma za Kiuchumi na ustawi tayari zimewafikia Wananchi kwa zaidi ya asilimia 80%.

Nd. Issa alizitaja huduma hizo zilizoleta mafanikio ni pamoja na huduma za Umeme, utatuzi wa mogogoro ya Ardhi pamoja na uokoaji wa zao la Karafuu uliopelekea kununuliwa kwa Tani 97.87 za Karafuu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.3.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya ya Mkoani alisema zipo changamoto kubwa zinazoleta kero ndani ya Wilaya hiyo akitolea mfano kesi za udhalilishaji pamoja na kupungua kwa ufaulu wa Skuli za Sekondari licha ya kupanda kwa ufaulu kwa zile skuli za Msingi.

Alifahamisha kwamba upungufu wa Walimu Mia Nne na Nne umeongeza kuchangia ufaulu mdogo wa Wanafunzi wa Skuli zilizomo ndani ya Wilaya ya Mkoani.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman alitembelea Hospitali ya Wilaya ya Mkoani ya Abdullah Mzee kuangalia mazingira halisi ya utoaji huduma za Afya ambazo hakuridhika nazo.

Mheshimiwa Hemed alilazimika kuuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya kupitia Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo Pemba kufanya marekebisho ya haraka ya upatikanaji wa huduma za usafishaji wa Figo pamoja na kufungwa Kifaa kinachosaidia Sehemu ya kuchomea Taka.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa muda usiozidi Wiki Moja kuona huduma zilizosimama katika Hospitali hiyo kwa sababu ya vifaa vilivyoharibika zinarejea kama kawaida.

Akimalizia ziara yake ya Wilaya ya Mkoani katika Mkutano wa majumuisho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzikbar Mh. Hemed aliwaonya watendaji wa Jeshi la Polisi Pemba kubadilika katika ushughulikiaji wa kesi za Udhalilishaji ili kuwarejeshea imani Wananchi.

Alisema wapo watendaji wasiokuwa waaminifu wa  Jeshi hilo katika baadhi ya Vituo Kisiwani Pemba ambao wamekuwa wakihusika na Rushwa zinazopelekea kuwalinda watuhumiwa wa keshi za Udhalilishaji ikiwemo ubakaji mambo ambayo Serikali zote mbili zinayakemea.

Alionya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayofanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Muungano wa Tanzania haitasita kumtolea Taarifa mara moja Askari atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo kwa kufukuzwa kazi au kuhamishwa kwenye Kituo chake alichokizoea kufanya vitendo viovu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Jumatatu anamalizia ziara yake ya Siku Tano Kisiwani Pemba kwa kuitembelea Wilaya ya Chake chake kukagua shughuli za Maendeleo na kujua changamoto zinazowakwaza Wananchi wa Wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.