Habari za Punde

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt.Nchemba Awaagiza TRA Kukadiria Kodi kwa Kufuata Sheria.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha inafuata Sheria wakati wa kukadiria kodi kwa wafanyabiashara ili kukuza biashara, wakati wa Kikao Kazi na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara hiyo, jijini Dodoma.

Na. Saidina Msangi na Peter Haule, WFM, Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwingulu Nchemba, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutumia weledi na kuzingatia sheria katika kukadiria kodi kwa wafanyabiashara ili kulinda walipa kodi na kutanua wigo wa walipa kodi.

Dkt. Nchemba alitoa maagizo hayo Jijini Dodoma alipokutana na wakuu wa Idara na Taasisi za wizara hiyo, katika kikao kazi kilicholenga kutekeleza maelekezo yaliyotolewa hivi karibuni na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo aliiagiza Wizara hiyo kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini kuhusu masuala ya kodi.

“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni muhimu yatekelezwe ipasavyo ili kulinda na kukuza uchumi wa nchi kwa kutoza kodi kwa staha, weledi na kwa mujibu wa Sheria na turekebishe mahali tulipoharibu”alisisitiza Dkt. Nchemba.

Aliitaka TRA kuacha kudai taarifa za miaka mingi ya nyuma ambayo iko nje ya sheria kwa wafanyabiashara ambazo zilikwishafanyiwa kazi,  kwani utunzaji wa kumbukumbu ni changamoto kwa wengi hivyo ni vema kuzingatia sheria na taratibu za namna ya kufanya ukadiriaji wa kodi.

“TRA nawataka mpeleke ujumbe makini kwa wafanyakazi wa TRA nchini nzima kwamba Serikali haijasema msikusanye kodi au mpunguze jitihada za kukusanya kodi hizo bali kinachoongelewa na kusisitizwa ni kukadiria na kukusanya kodi kwa kuzingatia sheria na taratibu, bila kuonea watu”alisisitiza Dkt. Nchemba

Aliongeza kuwa ili kuendelea kupata mapato ya kutosha nchini ni lazima kuwalea wafanyabiashara ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi akitolea mfano wa ngoómbe wa maziwa anayetakiwa kupewa huduma muhimu kabla ya kumkamua maziwa.

“Mheshimiwa Rais alielezea changamoto ya Kushika akaunti, fedha za wafanyabashara, tuache vitendo hivyo, hapa hakuna mjadala ni lazima yafuatwe na sisi Wizara tutaendelea kufuatilia maelekezo hayo” alisema Dkt. Nchemba.

Alisisitiza Mamlaka ya Mapato Tanzania kuzingatia maelekezo aliyotoa na  kurekebisha pale ambapo sheria hazikuzingatiwa ili kulinda uchumi wa nchi na kutodhoofisha biashara za walipakodi pamoja na kuangalia namna ya kuongeza walipa kodi wapya.

Kwa upande mwingine Waziri Dkt. Nchemba ametoa rai kwa Watanzania wakiwemo wafanyabiashara kulipa kodi inavyostahili kwa kufuata Sheria na taratibu zilizopo na kuzingatia matumizi bora ya kutunza kumbukumbu za malipo.

Alieleza kuwa utamaduni wa kulipa kodi uwe jambo la kawaida na la kila siku kwenye maisha yetu, ujanja ujanja wa kukwepa kodi ni kuvunja sheria na Serikali haitavumilia.

Aidha amewataka wafanyabiashara walioziondoa fedha zao kwenye benki wazirejeshe na kuzihifadhi kwenye benki hizo na kuahidi kuwa zitakuwa salama na hazitazuiwa na TRA kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa taasisi hiyo ili kurejesha ari ya ufanyaji biashara nchini.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni, alisema kuwa kikao kazi hicho kitawawezesha kujua hatua gani imefikiwa na Wizara ili kusimamia na kuendeleza uchumi wa nchi na Maisha ya watu.

Alisema kuwa ameona timu nzuri ya wataalam ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo itasaidia kutimiza malengo ya Serikali, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto), akiteta jambo na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Mary Maganga, wakati wa Kikao kazi na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara hiyo, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), akiipongeza Wizara hiyo kwa kuwa na wataalam wabobezi wa masuala ya uchumi ambao amewataka wasimamie vizuri masuala ya uchumi ili kuiwezesha Serikali kutimiza malengo yake ya kuwaletea wananchi maendeleo,  wakati wa Kikao kazi na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara hiyo, jijini Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Mary Maganga, akizungumza jambo wakati wa Kikao Kazi kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Masauni na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara hiyo, jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa Idara wa Wizara ya Fedha na Mipango wakisikiliza kwa makini maelekezo ya Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), na Naibu Waziri wake Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), kuhusu umuhimu wa kuzingatia Sheria na Weledi wakati wa kukadiria na kukusanya kodi kwa wafanyabiashara, wakati wa Kikao kazi na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara hiyo, jijini Dodoma. 
Manaibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Ndunguru (kushoto) na Bi Amina Khamis Shaabani, wakisikiliza maelekezo ya Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), kuhusu kuhakikisha uchumi unakua bila kuwapoteza walipa kodi, wakati wa Kikao Kazi na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara hiyo, jijini Dodoma. 
Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka (katikati) na viongozi wengine wa ofisi hiyo, wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), na Naibu Waziri wake Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), wakati wa Kikao Kazi na Wakuu wa Idara na Taasisi za Wizara hiyo, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- WFM)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.