Habari za Punde

Zimamoto Jijini Dodoma Yazindua Kambi ya Mafunzo ya Vijana wa Skauti

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi Julishaeli Mfinanga akivishwa skafu na kijana wa skauti mara baada ya kuwasili katika Kijiji cha Champumba, Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, ambako uzinduzi wa Mafunzo ya Vitendo kwa vijana wa Skauti ya kuwajengea uwezo wa kuokoa, kuzuia na kukabiliana na majanga mbalimbali katika jamii ikiwemo, moto, mafuriko pamoja na ajali za barabarani umefanyika mapema leo.

Kamishna wa Skauti Mkoa wa Dodoma, Salama Katunda, akifafanua jambo mbele ya mgeni rasmi Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi Julishaeli Mfinanga (Hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Mafunzo ya Vitendo kwa vijana wa Skauti ya kuwajengea uwezo wa kuokoa, kuzuia na kukabiliana na majanga mbalimbali katika jamii ikiwemo, moto, mafuriko pamoja na ajali za barabarani uliyofanyika leo katika Kijiji cha Champumba, Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi Julishaeli Mfinanga, akiimba nyimbo za hamasa pamoja na vijana wa skauti, wakati wa uzinduzi wa Mafunzo ya Vitendo kwa vijana wa Skauti ya kuwajengea uwezo wa kuokoa, kuzuia na kukabiliana na majanga mbalimbali katika jamii ikiwemo, moto, mafuriko pamoja na ajali za barabarani uliyofanyika leo katika Kijiji cha Champumba, Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi Julishaeli Mfinanga, akiwa kwenye picha ya pamoja na Kamishna wa Skauti Mkoa wa Dodoma, Salama Katunda, (Wa pili kushoto), Mratibu wa Maafa toka Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Maafa, Sajini Yona Benjamin (kushoto), na Viongozi wa Kijiji cha Champumba, Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, ambako uzinduzi wa Mafunzo ya Vitendo kwa vijana wa Skauti ya kuwajengea uwezo wa kuokoa, kuzuia na kukabiliana na majanga mbalimbali katika jamii ikiwemo, moto, mafuriko pamoja na ajali za barabarani umefanyika mapema leo. (Picha Zote na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji)

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Dodoma limeanza kutoa Mafunzo ya Vitendo kwa vijana 130 wa Skauti Mkoa wa Dodoma lengo ni kuwajengea uwezo wa kuokoa, kuzuia na kukabiliana na majanga mbalimbali katika jamii ikiwemo, moto, mafuriko pamoja na ajali za barabarani.

Akifungua mafunzo hayo leo Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Julishaeli Mfinanga amesema ni muda muafaka wa kutoa elimu kwa vitendo kwa vijana wa skauti ili kuwawezesha kukabiliana na majanga wawapo shuleni na hata katika jamii inayowazunguka.

Akizungumzia mafunzo hayo Kamishna wa Skauti Mkoa wa Dodoma, Salama Katunda, amemshukuru Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo John Masunga kwa kuwapatia Wakufunzi wanaowezesha mafunzo hayo na kuahidi kusimamia na kuhakikisha mafunzo hayo kwa Vijana wa Chama cha Skauti yanaenda kuwa chachu kwa kuhakikisha majanga mbalimbali yanadhibitiwa ili kulinda maisha ya watu pamoja na mali zao.

Mafunzo hayo yatatolewa kwa muda wa siku 7 na Askari Wakufunzi kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Maafa, Uongozi wa Chama cha Skauti ngazi ya Wilaya na Mkoa pamoja na taasisi nyingine za Kiserikali, ambapo yanafanyika katika Kijiji cha Champumba, Kata ya Chiboli, Tarafa ya Makang’ara, Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma.

Aidha Mafunzo hayo ni mwendelezo wa makubaliano ya Februari 26 mwaka huu ambapo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji liliingia makubaliano ya Ushirikiano wa Programu ya Mafunzo kati ya Jeshi hilo na Chama cha Skauti Tanzania, kwa kutoa elimu kwa vijana wa Skauti nchini ili kuwajengea uwezo katika kukabiliana na majanga mbalimbali.

Kwa upande wake Mratibu wa Maafa toka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sajini Yona Benjamin, amesema mafunzo hayo yametolewa muda muafaka ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Dodoma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya Vijana wa Skauti wameeleza juu ya umuhimu wa mafunzo hayo katika kukabiliana na majanga wawapo shuleni na hata katika jamii zao na kulishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.