Habari za Punde

DKT ABBASI AWATAKA MAAFISA HABARI KUZINGATIA MIONGOZO YA SERIKALI

Dkt. Peter Mataba akiwasilisha mada  kuhusu Mkakati wa Mawasiliano katika taasisi za Umma.

Innocent Mungy akiwasilisha mada kuhusu “uandaaji wa Mkakati wa Mawasiliano na utekelezaji wake” 

Katibu Mkuu wa Habari Dkt. Hassan Abbasi (katikati) na Naibu wake Dkt. Ally Possi (kulia) wakiongoza Kikao cha 16 cha Maafisa Habari Jijini Mbeya. Kushoto ni Aidan Eyakuze Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza.

Na John Mapepele, Mbeya

Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amewataka Maafisa Habari,Mawasiliano na Uhusiano kote nchini kuzingatia maelekezo, mbalimbali ya viongozi wakuu na  miongozo inayotolewa na Serikali wakati wanapoandaa  mikakati ya mawasiliano kwenye maeneo yao

Dkt Abbasi ambaye ni mtaalam mbobezi kwenye taaluma ya Habari ametoa kauli hiyo Mei 25, 2021 wakati akichangia uzoefu wake kwenye mada ya” uandaaji wa Mkakati wa Mawasiliano na utekelezaji wake” iliyowasilishwa na mwanahabari mkongwe, Innocent Mungy kwenye kikao kazi cha Maafisa Habari,Mawasiliano na Uhusiano (TAGCO) kinachoendelea Jijini Mbeya.

Amesema Serikali imekuwa na maelekezo mahususi ya kimkakati ambayo ni muhimu kuyaingiza ili kuleta matokeo bora wakati wa kufanya tathmini ya utendaji wa kazi za taasisi za Serikali.

Akiwasilisha mada hiyo Mungy amesisitiza kuwa wakati wa sasa mkakati wa mawasiliano ni nyenzo muhimu inayosaidia taasisi kufanya kazi kwenye kiwango kinachopimika.

Mwenyekiti wa kikao kazi hicho ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Ally Possi alitaka ufafanuzi wa namna gani Maafisa Habari wanaweza wakawafanya baadhi ya viongozi wasiopenda na kutambua  umuhimu wa kuwa na mikakati ya mawasiliano kwenye maeneo yao ambapo ilielezwa kuwa ni kwa kuwashirikisha.

Naye Dkt Peter Mataba wakati akiwasilisha mada ya “Mkakati wa Mawasiliano” amesisitiza kuwa taasisi zinapaswa kuzingatia ujumbe unaopelekwa kwa hadhira, na malengo ya taasisi husika ambayo yanatekelezeka kulingana na Mpango Mkakati wa taasisi husika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.