Habari za Punde

Serikali kuhakikisha Mahujaji wa Zanzibar watashiriki Ibada ya Hijja kwa mwaka huu

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia Baraza la Eid El Fitry katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.         

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itahakikisha inasimamia kikamilifu  masharti yote yatakayowekwa na Serikali ya Saud Arabia ili kuwawezesha mahujaji wa Zanzibar kushiriki Ibada ya Hijja baadae  mwaka huu (2021).

 Baraza la Eid el Fitri, liliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Jijini Zanzibar ni la Kwanza kwa Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi kuhutubia akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi..

 Alisema Serikali itatowa taarifa za kina kuhusiana na safari ya Hijja, huku akiwataka waislamu wanaofanya kazi kujiandaa na Ibada hiyo mapema, badala ya kusubiri hadi wanapostaafu.

 Aidha, aliitaka Kamisheni ya wakfu na Mali ya Amana kukamilisha mapendekezo yaliotolewa ya kuanzisha Mfuko wa Hijja Zanzibar.

 Rais Alhadj Dk Mwinyi, amewataka waislamu kudumu katika maisha yanayozingatia uadilifu pamoja na kujiepusha na mambo ya batili.

Aidha, Rais Alhadj Dk. Mwinyi alisema wakati huu waislamu wakisherehekea sikukuu ya Eid el Fitri, wana wajibu wa kuwajali na kuwasaidia  waislamu wenzao waliojaaliwa kuwa na  uwezo mdogo wa kipato.

Alisisitiza umuhimu wa kujikurubisha kwa Mola na kufanya ibada za sunna na fardhi , kama ilivyokuwa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambapo waislamu waijitahidi kudumu katika tabia na mwenendo mwema.

Alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa neema waislamu na kuweza kusali sala ya Iddi katika Misikiti na Viwanja mbali mbali Unguja na Pemba, ambapo sala hiyo kitaifa ilisaliwa katika viwanja vya Maisara, hali ya kuwa nchi iko katika hali ya amani na utulivu.

Aidha, alitoa shukran kwa Masheikh na walimu kwa kazi kubwa ya kuendesha darsa misikitini, katika kumbi  pamoja na kutumia vyombo vya habari kuwakumbusha waislamu wajibu wa kusoma Qur-an ili kuimarisha ibada zao.

Alhadj Dk. Mwinyi aliwashukuru wananchi na wageni ambao katika kipindi cha mwezi mtukufu hawakuwa katika funga, lakini walionyesha ushirikiano kwa ndugu zao waliokuwa kwenye swaumu.

Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, wakiwemo Marais wastaafu, wake wa Viongozi wakuu, viongozi wa serikali, vyama vya Siasa, viongozi wa Dini, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama  pamoja na wananchi walihudhuria hafla hiyo.

Mapema, Alhadj Dk. Mwinyi aliungana na mamia ya waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya Idd el Fitri iliyosaliwa katika viwanja vya Maisara, jijini hapa.

Sala hiyo iliongozwa na  Sheikh  Rashid Said Daud, wakati ambapo katika khotuba iliosomwa  na Sheikh Abdurahim Said Abdalla, alisisitiza umuhimu wa waislamu kuendelea kudumu katika kufanya mambo mema na kuepukana na maasi.

Katika hatua nyengine, Rais Alhadj Dk. Mwinyi alipata fursa ya kusalimiana  na Masheikh kutoka maeneo mbali mbali Unguja na Pemba waliofika Ikulu Jijini hapa, ambapo pamoja na kuwapa zawadi ya sikukuu ya Eid el Fitri, aliwatakia kheri ya sikukuu hiyo.

Aidha, Alhajj Dk. Mwinyi aliwatunuku mkono wa eid wananchi na watoto  waliofika katika viwanja vya Ikulu Zanzibar.

Wakati huo huo; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhadj Dk. Hussein Mwinyi alirudia kauli yake na kusisitiza kuwa Serikali itafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha Mahujaji wa Zanzibar wanakamilisha masharti yatakayowekwa, ili waweze kushiriki  ipasavyo Ibada ya Hijja, nchini Saud Arabia baadae mwaka huu.

Akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya ijumaa  Msikiti wa Ijumaa Malindi; Mkoa wa Mjini Magharibi, Alhadj Dk. Mwinyi alisema Serikali itafanya juu chini kuwawezesha Mahujaji kutimiza masharti ya ushiriki wa Ibada hiyo, baada ya Serikali ya Saud Arabia kuondoa zuio lilitokana na Ugonjwa wa Covid-19.

Alisema taarifa za awali zilizopokelewa kutoka nchi hiyo; zimebainisha miongoni mwa masharti yanayohitajika kufanikisha ushiriki huo ni pamoja na waumini kuwa na umri usiozidi miaka 60.

Alisema Mahujaji wote watakaoshiriki Ibada hiyo mwaka huu ni lazima wawe wamepata chanjo ya Ugonjwa wa Covid – 19.

Alhadj Dk. Mwinyi, alitumia fursa hiyo kuwataka waumini wote wenye nia ya kushiriki Ibada hiyo kujiandaa.

Aidha, aliwakumbusha waislamu umuhimu wa siku ya Idd el Fitri ya kuwatembelea ndugu na jamaa na kutakiana kheri, sambamba na kuushukuru Uongozi wa Msikiti huo kwa kumpa fursa ya kuzungumza na waumini.

Alhadj Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuzuru makaburi ya Masheikh mbali mbali maarufu waliozikwa katika eneo la msikiti huo. 

Nae, Khatibu katika sala hiyo  Sheik Ameir Muhidin, amewataka waumini wa  dini hiyo kufuatilia nyendo za watoto wao wakati huu Waislamu wakisherehekea sikukuu ya Eid el Fitri, kw akigezo kuwa  hujitokeza matukio mbali mbali yasio halali.

Aliwataka kuwa wachunga wa watoto wao ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.