Habari za Punde

Uzinduzi wa mbio za mwenge maalum wa Uhuru uwanja wa Mwehe Makunduchi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi akiingia katika Uwanja wa Mwehe Makunduchi kuzindua Mwenge Maalum wa Uhuru utaotembezwa Wilaya 150 Nchini Tanzania
 Mheshimiwa Hemed Suleiman akivishwa Skafu na Vijana wa Skauti mara baada ya kuwasili kwenye sherehe za Uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru Hapo Mwehe Makunduchi Mkoa Kusini Unaguja.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akisimama imara kwenye jukwaa Maalum aliliekewa wakati Nyimbo za Taifa za Zanzibar, Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Ule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zilipokuwa zikiimbwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi na Wananchi waliohudhuria uzinduzi wa Mwenge Maalum wa Uhuru zilizofanyika katika Uwanja wa Mwehe Makunduchi.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizindua Rasmi Mwenge wa Uhuru ambao Mwaka huu umeitwa Mwenge Maalum hapo Uwanja wa Mwehe Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja.
Mh. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi Rasmi Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kepteni Josephine Mumbash mara baada ya kuuasha hapoUwanja wa Mwehe Makunduchi

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiagana na Viongozi Mbali mbali wa Serikali na Vyama vya Kisiasa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uzinduzi wa Mwenge Maalum wa Uhuru hapo Mwehe Makunduchi Mkoa Kusini Unguja.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi alisema Serikali zote Mbili Tanzania Bara na Zanzibar zitaendelea kuienzi na kuidumisha Falsafa ya Mwenge wa Uhuru iliyolenga kuhamasisha kasi ya Maendeleo ya Kiuchumi na kudumisha Umoja Miongoni mwa Watanzania.

Dr. Hussein Ali Mwinyi alitoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla wakati akizindua Mbio za Mwenge Maalum wa Uhuru zilizofanyika katika Uwanja wa Mwehe Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema Umoja ulioshamiri ndani ya Vifua vya Watanzania unazidi kuimarisha Kasi ya Uchumi kitendo kinachoshuhudiwa kuongezeka kwa Mapato ya Serikali zote Mbili ile ya Jamuhuri ya Muunganowa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alieleza kwamba dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Muungano ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na Uchumi wa Kati wa Juu ifikapo Mwaka 2050 kwa kuimarisha masuala ya Uwekezaji na mahusiano mema ya ndani wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na vipaumbele vyengine imekusudia kuleta Mapinduzi ya Kiuchumi kwa kuimarisha Uchumi wa Buluu Shirikishi.

Rais wa Zanzibar alieleza kwamba  kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi kufikia Uchumi wa Kati wa juu na hatimae kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa Nchi zilizoendelea, maendeleo na matumizi  sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano {TEHAMA} ni muhimu katika sekta zote.

Dr. Hussein Mwinyi alisema mchango wa Sekta hii katika Maendeleo ya Taifa umekuwa ukiongezeka kwa wastan wa asilimia 8% kwa upande wa Tanzania Bara kwa Mwaka katika kipindi cha Mwaka 2015 hadi 2019 na kuleta mafanikio makubwa  yanayotokana na mfumo mzuri wa kisera na Kisheria.

Alibainisha kwamba Wafanyabiashara mbali mbali pamoja na Wananchi walio wengi wanaendelea kufaidika  na maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano  katika kuendesha maisha yao jambo ambalo limepunguza gharama za kuendesha biashara kwa kutumia mfumo wa manunuzi kupitia Mtandao huo.

Mheshimiwa Dr. Hussein Mwinyi alitahadharisha kwamba  wapo baadhi ya Watendaji wamekuwa wakitumia mfumo wa Tehama  vibaya kwa kufanya uhalifu na vilivyo kinyume na maadili ya Watanzania hali inayozua taharuki  na usumbufu pamoja na kuhatarisha Amani ya Taifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliendelea kuwakumbusha Wananchi mahali popote walipo waendelee kuziunga mkono Serikali zao ili yale malengo yaliyoainishwa ndani ya Ilani na Sera katika kuwahudumia Wananchi ziweze kufikiwa vyema.

Akigusia Homa ya Malaria mbayo imekuwa tishio kwa maisha ya Jamii Rais wa Zanzibar aliwaasa Wananchi waendelee kujilinda na viashiria vyote vinavyosababisha kuenea kwa virusi vya maradhi hayo kwa kudumia usafi wa mazingira utaosaidia pia kujiepusha na maradhi mengine ya miripuko.

Dr. Hussein Mwinyi alieleza kwamba licha ya Maradhi hayo kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa kwa upande wa Zanzibar lakini bado Wananchi wana jukumu la kusaidia kuendelea juhudi hizo zilizochukuliwa na Serikali  kwa kuungwa mkono na Mashirika na Taasisi Rafiki za Kimataifa.

Alizipongeza Wizara zote mbili zinazosimamia shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa  kutoka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Dr. Hussein alisema mashirikiano ya Viongozi na Watendaji wa Wizara hizo wanayoyaonyesha  katika maandalizi ya Sherehe hizo ni kielelezo muhimu cha kudumisha udugu na Muungano ambao ni muhimu kwa pande zote mbili unaopaswa kuendelezwa katika masuala yote yanayolenga kuimarisha Muungano huo.

Akitoa Taarifa ya Mwenge Maalum wa Uhuru wa Mwaka huu wa 2021 Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mheshimiwa Leila Mohamed Muusa akikaimu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar alisema mbio za Mwenge wa Uhuru zitaendelea kuwakumbusha Wananchi juu ya umuhimu wa kupiga vita dhidi vitendo vya Rushwa, Dawa za Kulevya na Udhalilishaji.

Mheshimiwa Leila alisema Vitendo vya Rushwa ambavyo vimekuwa vikipigwa vita na hata Viongozi Wakuu wa Taifa hili waliopita vitapata Muarubaini na kuondoka kabisa pale Viongozi kwa kushirikiana na Wananchi watapojizatiti kushirikiana katika mapambano hayo.

Alielezea matumaini yake ya kufana kwa Mbio za Mwenge Maalum wa Uhuru Mwaka huu kutokana na Kazi kubwa iliyochukuliwa na Viongozi na Wataalamu katika kuwafinyanga Vijana waliopewa jukumu la kutembeza Mwenge huo katika Wilaya zote 150 za Tanzania ndani ya Siku 150.

Kwa upande wake akitoa salamu za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera,Bunge, Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista Joaquim Mhagama alisema Mbio za Mwaka huu zimeandaliwa Maalum kufikia kikomo chake Mkoani Geita Wilaya ya Chato ili kuheshimu mchango mkuu uliotolewa na Rais wa Awamu ya Tano wa Tanznia Marehemu Dr. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema Mbio za Mwenge wa uhuru Tanzania zilizorejeshwa tena Serikalini kwa zaidi ya Miaka 29 sasa zimekuwa zikiamsha ari na hamasa ya kuibuka kwa miradi ya Kiuchumi na Maendeleo katika maeneo mbali Nchini Tanzania Bara na Zanzibar,

Alisema Falsafa ya Waasisi wa Taifa la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume baada ya kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar imekuwa ikiweka alama ya Historia kutokana na ushiriki wa Wananchi kwenye Miradi ya Kiuchumi na Kijamii kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru.

Waziri Jenista Mhagama alisema Waasisi hao wawili wa Tanzania wataendelea kukumbukwa na Vizazi viliopo sasa na vile vitakavyoibuka katika Kanre zijazo kutokana na msingi waliouweka wa Kuwaunganisha pamoja Watanzania wanaoendelea kuringia Mshikamano wao ambao umekuwa kigezo ndani ya Bara la Afrika.

Mapema akitoa salamu za Mkoa Mwenyeji wa Kusini Unguja, Mkuu wa Mkoa huo Mheshimiwa Rashid Hadid Rashid alisema Mkoa huo umepata bahati ya Mwenge wa Uhuru kwa kuzinduliwa mara ya Pili kutanguliwa na ule  Mwaka 2001 katika Kijiji cha Mwera.

Mheshimiwa Hadid alisema Mkoa wa Kusini Unguja umejipanga kuendesha shughuli zake za Kiserikali katika kuwahudumia Wananchi kwa kutumia Mfumo wa Kisasa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano {TEHAMA} ukienda sambamba na Falsafa ya Mwenge wa Uhuru katika Ujumbe wake wa Mwaka huu.

Akigusia uwajibikaji wa Serikaliya Mapinduzi ya Zanzibar alisema Uongozi na Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja wanaendelea kupata faraja kutokana na kasi ya Serikali Awamu ya Nane iliyojikita kupambana na Rushwa, Uhujumu wa Uchumi na Uzembe ambapo jitihada hizo zimeanza kuleta matumaini kwa jamii.

Mbio za Mwenge Maalum wa Uhuru zitakazohusika kutembezwa katika Wilaya 150 za Tanzania Bara na Zanzibar zitafikia Kilele chake Mkoani Geita Wilaya ya Chato mnamo Tarehe 14 Oktoba 2021 ambapo Ujumbe wa Mwaka huu unaeleza Tehama ni Msingi wa Taifa Endelevu itumie kwa usahihi na Uwajibikaji.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.