Wananchi wametakiwa kujisaajili katika ushiriki wa Mashindano ya mbio za Zanzibar international marathon zinazotarajiwa kufanyika julai 18 mwaka huu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitoa wito huo alipokutana na kufanya mazungumzo na kamati ya maandalizi ya mashindano hayo walipofika Ofisini kwake Vuga Jijni Zanzibar.
Alisema kwa kuwa mashindano hayo yamepata Baraka za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi itatoa taswira njema endapo watu wengi watajitokeza kushiriki ikiwemo wenyeji na wageni kutoka mataifa mengine.
Aidha Mhe. Hemed aliipongeza kamati hiyo kwa uzalendo wao kwa kujitolea kufanya maandalizi ya mashindano hayo jambo ambalo pia litasaaidia kuitangaza Zanzibar na vivutio vyake vya kitalii.
“Mashindano haya ya Marathoni yatakapofanyika yatasaidia kwa kiasi kikubwa wataali kuvitembelea vivutio vyetu ikiwemo na maeneo ya kihistoria”. Alisema Makamu wa Pili
Mhe. Hemed aliahidi kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar itatoa kila aina ya ushirikiano katika mashindano hayo kutokana na jambo litachangia kuwaunganisha wazanzibar na wageni kutoka maeneo tofauti.
Akigusia suala la udhimini wa mashindano hayo Makamu wa Pili wa Rais alisema serikali itazungumza na makampuni mbali mbali pamoja na mashirika yaliopo Zanzibar ili kushiriki kikamilifu.
Pia Mhe. Hemed alizipongeza taasisi ambazo tayari zimeanza kujitokeza kudhamini mashindano hayo ikiwemo Benki ya NMB, Vodacom, Just Fit na mabalozi wa kuitangaza Marathoni hiyo.
Alisisitiza kwamba, serikali kwa sasa imejipanga kuimarisha na kurejesha hadhi ya michezo Zanzibar hasa katika kuamsha ari kwa vijana wake kuchangamkia fursa zinazopatika ndani yake.
Nae Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale ambae pia ni Kaimu Waziri wa Habari, vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Leila Muhamed Mussa alisema kuwepo kwa mashindano hayo ya marathon kutasaidia kuunga mkono azma ya Rais Dk. Mwinyi ya kukuza Uchumi wa Zanzibar hasa kupitia Uchumi wa Buluu ambapo sekta ya utalii ni moja kati ya maeneo ya uchumi huo.
Nao viongozi wa kamati hiyo wakiongozwa na Hassan Suleiman Zanga walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa lengo la Marathon hiyo kufanyika zanzibar ni kuhamasisha utalii hasa katika kipindi hichi cha mripuko wa maradhi ya covid 19 ambapo inaonekana sekta hiyo kususua katika mataifa mbali mbali.
Walieleza kuwa, asilimia 20 ya mapato yatakayopatikana katika mashindano hayo yatafikishwa kwa wazee wasiojiweza, watoto yatima pamoja na watu wenye mahitaji maalum ili kutoa mchango wao kwa makundi hayo maalum.
Kamati hiyo ya mashindano pia imekamisha zoezi la kumfanyia usajili Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambapo atashiriki katika mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment