Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe.Rashid Hadid Rashid akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali kuhusiana na utekelezaji wa kazi ndani ya mkoa wake kuanzia Disemba 2020 hadi Juni 2021 huko Ofisini kwake Tunguu Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
PICHA NA FAUZIA MUSSA /MAELEZO ZANZIBAR
Na Khadija Khamis-Maelezo 27/06/2021.
Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Rashid Hadidi Rashid amesema jumla ya migogoro 125 ya ardhi iliojitokeza katika mkoa wa kusini Unguja 43 imeshapatiwa ufumbuzi .
Akitoa Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kiutendaji wa Kimkoa huko Ofisini kwake Tunguu wilaya ya Kati Unguja wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema migogoro iliopatiwa ufumbuzi ni ya wilaya ya kati na kusini Unguja .
Alisema miongoni mwa migogoro iliyokuwa ikilalamikiwa na wananchi ni pamoja na ardhi moja kumilikiwa na watu wawili tofauti .
Alifahamisha kuwa ukosefu wa elimu kwa wananchi unachangia wingi wa migogoro kwa kutofahamu taratibu za kisheria kwa zile kesi ambazo zimeshatolewa hukumu na Mahakama ya Ardhi au ziko Mahakamani .
Akizungumzia ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika awamu ya nane ya uongozi kuanzia mwezi disemba 2020 hadi June mwaka 2021 amesema katika Mkoa wa kusini jumla ya miradi minane mikubwa imo katika mkoa huo
Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni Mradi wa Ujenzi wa Mahakama Kuu Tunguu uko vizuri karibuni utakabidhishwa Serikalini pamoja na Skuli ya Kibuteni yenye dahalia tayari vijana 113 wanaendelea na masomo katika skuli hiyo.
Alifahamisha kuwa mradi wa ujenzi wa hospitali ya Binguni bado haujafikia kiwango kinachotakiwa kutokana na uhaba wa fedha hivyo Serikali iko mbioni kuufanikisha .
Aidha alisema mradi wa umwagiliaji maji wa kilimo Cheju uko vizuri karibuni utakabidhishwa Serikalini wakati mradi wa Skuli ya kisongo wa elimu ya Amali bado haujakabidhiwa kutokana na matatizo baina ya Mkandarasi na Wizara wakati wowote utakabidhiwa uanze kazi .
Akielezea zaidi Mkuu huyo amefahamisha mradi wa ujenzi wa nyumba za kurekebisha tabia pamoja na mradi wa barabara ya jozani ukongoroni hadi charawe ni miongoni mwa miradi mikubwa kwa Mkoa huo.
Aidha amesema wafanyakazi wanawajibika ipasavyo katika kusimamia wizi na rushwa katika utendaji wa kazi zao hata hivyo wamefanikiwa kukusanya kiasi cha shilling bilioni mia saba kwa Wilaya ya Kati ambapo kwa Wilaya Kusini ni zaidi ya milioni mia tano zimepatikana kwa Halimashauri na Mabaraza kuanzia Desemba hadi june 2020/2021.
No comments:
Post a Comment